Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

SHAHIDI wa nane katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Bernad Nyambali, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa maandamano ya wafuasi wa Chadema yalitokana na hotuba zilizotolewa wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu  Dk.Zainabu Mango mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, shahidi huyo amedai kauli zilizotolewa na viongozi hao zilihamasisha watu waandamane kutoka eneo la mkutano wa kampeni  kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

Nyambali amedai maneno yaliyokuwa yakitamkwa yalichochea chuki kati ya wananchi dhidi ya serikali na vyombo vya dola hivyo, wafuasi wao walipata hisia hasi na kusababisha kuandamana.

Shahidi  Nyambali ambae wakati wa tukio alikuwa msaidizi wa mkuu wa upelelezi mkoa wa Kinondoni amedai, maandamano hayo pia yalisababisha athari mbali mbali ikiwemo kusababisha kifo cha  binti Akwilina Akwilini ambae matokeo ya uchunguzi yalionyesha kuwa alifariki kutokana na jeraha la risasi ambayo alipigiwa akiwa eneo la Mkwajuni ambayo ndio ilikuwa center ya maandamano.

 Ameendelea kudai kuwa baadhi ya watu waliumia kwa kurushiwa na kupigwa mawe ambapo kati ya hao  maaskari wawili waliumia baada ya kupigwa mawe na waandamanaji  ambao ni CP Fikiri wa kituo cha polisi Osterbay na Koplo Hakimu.

Akijibu swali la Dr Mango  namna alivyohusika na upelelezi juu ya kifo cha Akwilina, shahidi a amedai kuwa, hakuhusika katika upelelezi wa tukio la kifo cha Akwiline Akwilina,  upelelezi wa tukio hilo ulifanywa na timu nyingine ya upelelezi.

Akielezea tukio hilo, shahidi Nyambali amedai February 16,mwaka 2018 akiwa katika shughuli zake za za kiupelelezi eneo la Kinondoni Hananasifu, alisikia kelele za kuashiria vurugu kutokea upande wa Barabara ya Kawawa lakini wakati akitafakari alipigiwa simu na Mkuu wa Upelekezi wa Mkoa wa Kinondoni, SSP Mungu Maluku na kumuagiza aelekee Barabara ya Kawawa kwa kuwa kulikuwa na watu wanaandamana.

Amedai, alipofika eneo la tukio alikuta kuna kundi kubwa la watu wanaokadiriwa kuwa 350 hadi 500 waliokuwa wakiandamana kuelekea eneo la Mkwajuni huku wakionekana wanajazba  na wakibishana na Polisi ambao  walikuwa wakiwataka kutawanyika.

Amedai watu hao walikuwa wanajibu kuwa hawaondoki wawaue huku miongoni mwao walikuwa wamebeba mawe, fimbo na kutanda barabara nzima huku wakiimba nyimbo za kuhamasishana.

Amesema, alienda moja kwa moja hadi kituo cha daladala cha mwendo kasi na kukuta viongozi kadhaa wa jeshi la polisi wakiongozwa na ASSP Gerlad Ngichi  ambapo walikuwa wakiwataka  waandamanaji kutawanyika na muda ule walikuwa wamefikia hatua ya kufyatua mabomu.

"Niliweza kuwatambua baadhi ya watu niliokuwa nawajua ambao walikuwa mbele kabisa kama vile, Freeman Mbowe, John Mnyika, Vincent Mashinji na Halima Mdee".

Shahidi Gerlad amedai baada ya waandamanaji kutawanywa barabara ilikuwa imetapakaa mawe, fimbo, chupa za maji huku meza ambazo zilikuwa zikitumiwa na wafanyabiashara pembeni ya barbara zilibinuliwa kutokana na vurugu zilizotokea na maduka yalifungwa.

"Baada ya maandamano yale kutawanywa na hali kuwa shwali nilianza upelelezi wangu wa kuweza kubaini watu (RAIA) ambao wanaweza kufaa kuwa mashahidi katika kesi ya maandamano  ambao waliweza kuona namna maandamano hayo yalivyokuwa yakifanyika.

Mbali ya Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Taifa, Dk.Vincent Mashinji ,  Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika,  Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji na Mbunge wa Kawe  Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...