Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MTANZANIA mwenzangu kabla ya kuendelea na hiki ambacho nataka kukieleza kwa siku ya leo , naomba nitumie nafasi hii kukusalimia.Asalaam Eleikum, Bwana Yesu Asifiwe, Bwana awe nawe, Mambo vipi baharia wangu , natumai unaendelea vema ndugu mtanzania.

Nimetoa salamu zote hizo kwa kuamini kila mmoja atajibu anayooona inamfaa, hata hivyo kwa ujumla pamoja na salamu zote ambazo nimezitoa maana yake ibaki moja tu nayo ni kutoa salamu kwako.Natumai umeitikia na baada ya hapo niendelee na maelezo yangu.

Sina uhakika kama ambacho nitaekeleza kitaeleweka kwa msomaji , hata hivyo naomba Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo unijaalie busara na hekika ili ujumbe wangu ueleweke.Eee Mwenyezi Mungu naomba unipe ujasiri wa kuandika maelezo ambayo hayatakuwa magumu kueleweka. Mungu wa Said Mwishehe umekuwa ukinikubalia kwa kila niombalo kwako.Natumai na hili ambalo nimeomba nalo umenikubalia.

Iko hivi; kuna mambo mengi ya kujifunza katika maisha.Yapo ya kujifunza darasani, yapo ya kujifunza kupitia vitabu vilivyoandikwa na wasomi wa kada tofauti, kuna kujifunza kupitia jamii inayokuzunguka.Pia kuna kujifunza kupitia kwa wengine wenye uelewa katika jambo fulani na kuna kujifunza kupitia viongozi wanaokuongoza.Ndio !Na kama kuna aina nyingine ya kujifuza baki nayo.Ila yote iwe kujifunza tu.

Hadi hapo naamini tunakwenda sawa.Sina shaka nawe hata kidogo kuwa kuanzia hapo juu hadi hapa ulipofika umenielewa .Tuendelee na majadiliano.Kwanza meza mate na kisha tuendelee. Jamani binafsi naomba nikiri kuwa kupitia kwa Rais Dk.John Magufuli kuna mengi najifnza kutoka kwake. Ndio! Unashangaa nini?Najifuza mengi tu na kama hutaki basi jinyonge ingawa usipokufa kesi itabaki kuwa ya kwako ya kutaka kujia.Mimi simo kwenye hilo.

Kuna mambo ya kukaa nayo kimya lakini kwenye hili la kujifunza kutoka kwa Rais wangu mpendwa Dk.Magufuli ni muhimu nikaweka wazi yapo mengi najifunza na nitaendelea kujifunza siku hadi siku.Najifunza namna ambavyo anavyowaongoza Watanzania zaidi ya milioni 55 kwa weledi mkubwa.Najifunza alivyomnyenyekevu kwa anaowangoza .Najifunza namna ambavyo Rais anavyosimamia suala la kuhamasisha uzalendo miogoni mwa Watanzania.

Kwa Rais Magufuli najifunza namna ambavyo Watanzania tunakiwa kusimama imara kutetea raslimali za nchi yetu.Najifunza namna ambavyo Rais Magufuli pamoja na madaraka makubwa aliyonayo bado ameendelea kuwa mnyenyekevu kwa wananchi wake.

Hakika kuna mengi najifunza kutoka kwa Rais.Naamini wengi tunajifunza kutoka kwake.Ukweli ndio huo, sote tunajifunza .Kama unabisha nyoosha mkono juu kisha fanya kama unajikuna nikuone.Huna ujanja wa kunyoosha kidelo juu maana ukweli sote tunaendelea kujifunza.

Pamoja na kujifunza katika maeneo ambayo nimeyataja hapo juu, nirudie tena Rais Magufuli ametoa somo kubwa kwa Watanzania. Somo lenyewe ni hili la kusamehe kwani amethibitisha kuwa yeye ni mwenye kusamehe kwa vitendo kwa wale walimkosea.

Jamani hapa naomba tuelewane kidogo , tukubali kuna watu wengi wametofautiana kwa namna moja au nyingine huko mtaani lakini hawataki kusameehana.Wanaona kusamehe sio sehemu ya maisha yao.Wamebaki wanakunjiana ndita hadi uso unaota makunyanzi a.k.a mikunjo. Kila mmoja anabaki na kinyongo dhidi ya aliyemkosea.Haya mambo ya kutosameehana yapo kwenye ngazi ya mtu mmoja mmoja na hata kwenye familia.Unabisha?Acha ubishi kama sio wewe hutaki kusamehe basi kua ndugu yako hataki kutoa msamaha kwa aliyemkosea.Wenyewe wanasema akimwaga mboga, wewe unamwaga ugali.

Hakika Rais Magufuli ametoa somo la kujifunza , nalo ni kusamehe.Kwani uongo? Juzi tu hapa Rais ametangaza kuwasamehe wabunge Januari Makamba wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga na William Ngeleja wa Jimbo la Sengerema mkoani Mwanza. Wawili hao walimkosea Rais Magufuli kwa kumsema vibaya kupitia simu zao za mkononi.Kama unavyojua mambo ya kukua kwa tekolojia ya habari na mawasiliano.Sauti za wawili hao zikadakwa na kusambazwa mtandaoni.

Ukweli walichafua hali ya hewa lakini tunaambiwa kila siku kuwa hakuna binadamu aliyekamilika bali mkamilifu ni Mwenyezi Mungu peke yake.Kwa kuwa Januari Makamba na Ngeleja waliona makosa yako, wakaamua kuomba msamaha kwa Rais.

Hivyo wakati Rais Magufuli anazungumza kwenye mkutano wa wakandarasi na wahandisi uliofanyika siku za karibuni jijini Dar es Salaam alitangaza kuwasemehe wabunge hao.Rais alisema amejiridhisha kwa asilimia 100 sauti hizo zilikuwa za kwako.

Akawaza namna ambavyo adhabu itakuwa kali wakipelekwa Kamati Kuu ya CCM.Akaamua kuwasamehe.Tena akaeleza kusamehe kunauma lakini ni vema akatoa msamaha kwa wabunge hao kwani wamekiri na kuomba msamaha. Hongera Rais wangu kwa kutoa msamaha na umma wa Watanzania ukasikia.

Ni nadara sana kuona kiongozi mwenye nafasi ya aina yako akakubali kusamehe kwa waliomkosea.Kuna mifano mingi ya watu wambao wamekosea huko nyuma na hawakuwahi kusamehewa.Kwa leo si wakati wake.Nambuka Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi alisema kila kitabu na zama zake.Kwa kweli zama hizi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.Magufuli kuna mengi tunajifunza.Ametufundisha umuhimu wa kusamehe aliyekukosea.

Hakuishia hapo kwa Januari Makamba na Ngeleja peke yake, bali ni jana tu ya Septemba 10 , Rais Magufli ametoa msamaha kwa mbunge wa Mtama Nape Nnauye.Nape naye anahusishwa na kumsema vibaya Rais Magufuli baada ya sauti yake kusikika akizungumza kwenye simu.

Nape katika sauti yake ambayo nayo ilisambaaa katika mitandao ya kijamii alisikika akitoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais wetu mpendwa. Hata hivyo Rais Magufuli hakuzungumza lolote baada ya Nape sauti yake kusikika kwenye mitandao.

Rais aliamua kukaa kimya na hapa kuna kitu cha kujifunza.Nacho ni kuwa kimya jambo linapotokea kwani hakuna sababu ya kuhangaika kulijibu.Ametumia hekina na busara kubwa kama kiongozi wa nchi yetu, Tunafahamu Rais alikaa kimya kwa kipindi chote na jana alipoamua kulizungumzia suala la Nape na sauti yake alisikika akisema amemsamehe kwani mbunge huyo bado ni kijana.

Hakusita kueleza hatua mbalimbali ambazo Nape alipita kabla ya kufika kwake.Nape amehangaika sana kutafuta nafasi ya kumuona Rais.Alilazimika kwenda kuomba msaada wa mzee Philip Mangulla, mzee Apson na Mama Maria Nyerere. Kote huko alikwenda ili wamsaidie kupata nafasi ya kumuona Rais.

Pamoja na mambo mengine Rais hakusita kueleza kuwa alivyokuwa anatumiwa meseji za kuombwa msamaha na Nape.Tena meseji nyingine zilikuwa zinatumwa saa nane usiku.Na Rais amekiri kwa namna ambavyo alikuwa anasoma meseji za Nape za kuomba msamaha amejiridhisha kuwa ni kweli anajutia kosa alilofanya na sasa amemsamehe kutoka kwenye moyo wake.

Akatumia nafasi hiyo kumtaka aende akafanye kazi za kuwatumia wananchi wa jimbo lake , familia yake na watanzania.Hongera Rais somo ambalo nalipata si kumsamehe Nape, Januari Makamba au Ngeleja bali najifunza hata ukiwa kwenye nafasi bado unapaswa kusamehe tena ikiwezekana samehe saba mara sabini. Mwito wangu kwa Watanzania tujifunze kusamehe kama ambavyo Rais wetu anavyosamehe. Si dhambi kujifunza jambo jema na Rais wetu ameonesha njia.

Pia ushauri wangu , linapotokea jambo hakuna sababu ya kukimbilia kulizungumza maana unaweza kuzungumza ukapatia na unaweza kulizungumza ukakosea.Tuwe makini.Nakumbuka kwenye hili sakata la sauti za kumsema vibaya Rais kuna wana CCM na viongozi mbalimbali walianza kutoa matamko.Wakati wao wanatoa matamko Rais amebaki kimya tu, anatafakari kimya kimya kama hajui kinachoendelea.

Kuongeza kwa matamko kulisababisha Katibu Mkuu wa CCM DkBashiru Ally kutoa tamko la kuonya yoyote atakeyezungumzia suala hilo na kutoa tamko atachukuliwa hatua.Kweli kukawa kimya na ukimya huo leo umekuja na jibu ambalo nalo ni msamaha kati ya waliokosa na aliyekosewa.

Inatosha kwa leo , nikutakie kazi njema na tuendelee kuijenga Tanzania yetu ambayo haipatikani mahali kokote duniani zaidi ya Tanzania.Naipenda nchi yangu, naipenda Serikali ya Awamu ya tano na kubwa zaidi nampenda Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya Watanzania wote.

Simu 0713833822

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...