Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
ZANZIBAR na Comoro zimeahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria uliopo ambao una lengo la kuzidisha mashirikiano katika sekta za maendeleo kwa manufaa ya pande mbili hizo.

Ahadi hiyo imetolewa leo katika mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipofanya mazungumzo na Rais wa Comoro Azali Assoumani ambaye yupo Zanzibar kwa mapumziko.

Katika mazungumzo yao viongozi hao kwa pamoja waliahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria  baina ya pande mbili hizo ambao umeimarika kwa muda mrefu na kuleta manufaa kwa nchi na wananchi wake ambao wana udugu wa damu.

Viongozi hao walieleza kuwa licha ya kuwa ni majirani lakini pia, ni ndugu wa damu hivyo, kuna haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wao uliopo kwa manufaa ya nchi zao hasa katika kuendeleza sekta za maendeleo kwa mashirikiano ya pamoja.

Akizungumza kwa upande wake Rais Dk. Shein alimueleza Rais Azali Assoumani kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano huo na ushirikiano uliopo sambamba na kuendeleza Mkataba wa Makubalino uliosainiwa mwaka 2014 na pande mbili hizo kwa lengo la kukuza udugu uliopo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa katika Mkataba huo wa Makubaliano masuala mbali mbali yalitiliwa nguvu yakiwemo mashirikiano katika sekta ya afya, elimu, mila na utamaduni pamoja na masuala mengineyo ambayo tayari yameshaanza kufanyiwa kazi na kuleta tija.

Alieleza kuwa mbali ya uhusiano wa kimaendeleo kati ya pande mbili hizo pia, Zanzibar na Comoro zina historia katika kukuza mila na tamaduni sambamba na mafunzo hasa katika elimu ya dini ya Kiislamu ambapo historia inaonesha kwamba wananchi wa Comoro walio wengi wamepata elimu ya dini ya Kiislamu hapa Zanzibar.

Akitolea mfano maelezo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa Masheikhe wakuu wa Comoro  akiwemo Marehemu Sheikh Mwinyi Baraka walipata elimu yao ya dini hapa Zanzibar na hatimae kuwa balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar katika uhai wake hadi kufariki kwake mwaka 1988.

Kutokana na umuhimu huo Rais Dk. Shein alieleza hatua alizozichukua katika kuhakikisha katika ziara yake aliyoifanya nchini humo mwaka huo wa 2014 alipata fursa ya kulizuru kaburi la Sheikh Mwinyi Baraka ambaye alikuwa ni mwanachuoni mashuhuri.

Katika kuhakikisha Mkataba wa Makubaliano hayo yaliosainiwa katika ziara ya Rais Dk. Shein nchini Comoro mnamo mwezi Septemba mwaka 2014 yanafanyiwa kazi Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kilitiliana saini Mkataba wa Makubaliano juu ya mashiriikiano na Chuo Kikuu cha Comoro mnamo Januari 19 mwaka 2016.

Aidha, katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha Mkataba huo wa Makubaliano unatekelezwa vyema ikiwa ni pamoja na kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili nchini Comoro sambamba na kuwepo kwa kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya Chuo Kikuu cha Comoro na Chuo Kikuu cha (SUZA).

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa makubaliano hayo pia, yanaeleza jinsi Chuo Kikuu cha Comoro kitakavyoshirikiana na (SUZA) katika kutoa mafunzo ya lugha ya Kifaransa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimpongeza Rais Azali Assoumani kwa uwamuzi wake wa kuja kupumzika Zanzibar, na kumueleza kuwa Zanzibar ni salama. “Karibu sana Zanzibar jisikie uko nyumbani kwani Zanzibar ni sehemu salama ya kupumzika”,alisisitiza Dk. Shein.

Nae Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani alimpongenza Rais Dk. Shein kwa kumkaribisha vizuri Zanzibar jambo ambalo alisema huo ni utamaduni uliojengeka kwa watu wa pande mbili hizo ukiwa ni urithi wa Waasisi wao.

Rais Assoumani alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Comoro na Zanzibar zina mambo mengi ya kushirikiana licha ya yale yaliotiwa saini ambayo tayari yameshaanza kutekelezwa na kuanza kuleta manufaa.

Alieleza kuwa wananchi wa Comoro wanafarajika na uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yao na ndugu zao wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba wapo Wakomoro waliozaliwa Zanzibar wananchi Comoro na wale waliozaliwa Comoro ambao wanaishi Zanzibar.

Rais Assoumani alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina mambo mengi ya kushirikiana hasa ikizingatiwa ukaribu na udugu uliopo baina ya pande mbili hizo na kueleza kuwa kuchaguliwa kwa Rais John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa (SADC) kutazidi kujenga mustakbali mwema wa nchi mbili hizo.

“Sisi ni ndugu wa damu hivyo, kuna haja ya kufanya kazi kwa pamoja”,alisema Rais Assoumani na kusisitiza kuyafanyia kazi yale yote yaliotiwa saini katika Mkataba wa Makubaliano kati ya Zanzibar na Comoro mnamo mwaka 2014.

Katika maelezo yake, Rais Azali Assoumani alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa nchi yake pamoja na wananchi anaowaongoza wataendelea kuthamini udugu wa kihistoria uliopo na kuzidisha uhusiano na ushirikiano wao.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na mgeni wake Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Azali Assoumani wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kusalimiana leo.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na mgeni wake Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Azali Assoumani wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kusalimiana
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na mgeni wake Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Azali Assoumani baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar .(Picha na Ikulu) 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...