Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa matumizi ya gesi asilia katika kiwanda cha Lodhia, kilichopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani, Septemba 24, 2019.

Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa wamiliki wa kiwanda cha kufua vyuma cha Lodhia, kilichopo Mkuranga, Pwani, kabla ya kuzindua rasmi matumizi ya gesi asilia katika kiwanda hicho, Septemba 24, 2019.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua kiwanda cha kufua vyuma cha Lodhia, kilichopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani, kabla ya kuzindua matumizi ya gesi asilia kiwandani hapo, Septemba 24, 2019.

Na Veronica Simba – Pwani
WAZIRI ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),  inatarajia kukusanya kati ya shilingi milioni 85 hadi 120 kwa mwezi, sawa  na shilingi bilioni 1.02 hadi 1.4 kwa mwaka kutokana na matumizi ya gesi asilia katika kiwanda cha Lodhia kilichopo Mkuranga, ambayo hadi sasa ni futi za ujazo laki mbili kwa siku.

Hayo yamebainishwa Septemba 24, 2019 wakati Waziri wa Nishati Dk.  Medard Kalemani, alipozindua matumizi ya gesi asilia katika kiwanda hicho  cha kufua vyuma ambacho awali kilikuwa kikitumia mafuta mazito.

Mbali na makusanyo hayo kwa serikali; kwa upande wa kiwanda, kupitia matumizi ya gesi asilia, kimeweza kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa zake kwa zaidi ya asilimia 40 ikilinganishwa na gharama zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya mafuta mazito.

Akizungumza baada ya kukagua shughuli za kiwanda hicho pamoja na kufanya uzinduzi husika, Waziri alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) pamoja na wataalamu wa Wizara, kufanya mapitio ya bei za gesi viwandani ili ziwawezeshe wawekezaji kuzalisha kwa tija.

“Mje na bei muafaka ambazo haziathiri uwekezaji wa TPDC na haziathiri uwekezaji wa wenye viwanda lakini pia zisiathiri mapato ya serikali,” alisisitiza.

Akifafanua zaidi, Waziri alisema bei ya sasa inaanzia Dola 4.7 hadi 7.72 kwa uniti moja, ambayo imekuwa kikwazo kwa wawekezaji.

Aidha, Waziri aliiagiza TPDC na kampuni yake tanzu ya GASCO, kukamilisha zoezi la ukusanyaji takwimu kwa ajili ya usambazaji wa gesi wilayani Mkuranga ndani ya kipindi cha miezi miwili ili ziwezeshe kubaini mahitaji ya gesi viwandani katika wilaya hiyo na kuvisambazia nishati hiyo
 kwani manufaa yake ni makubwa.

Waziri pia alieleza kuwa serikali inafanya mapitio ya bei za umeme ili kuzirekebisha na kwamba bei hizo zitapungua, hususan baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya uzalishaji umeme, ukiwemo wa Julius Nyerere, Rufiji.

Aidha, aliwataka wadau wa sekta za gesi na mafuta, kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la kupitisha mabomba ya gesi katika maeneo yao. “Msidai fidia kwakuwa nasi hatutozi gharama za kuunganisha. Hivyo nanyi, msilete vikwazo.”

Katika hatua nyingine, Waziri aliuagiza uongozi wa TANESCO wa Wilaya, Mkoa na Makao Makuu, kukipatia kiwanda cha Lodhia megawati nane zaidi za umeme kama kilivyoomba ili zifike 14 kufikia mwisho wa mwezi huu.

Alisema hakuna sababu ya kushindwa kutekeleza agizo hilo maana kuna umeme wa kutosha. Sambamba na hilo, aliagiza pia kusiwe na mgao wa umeme wilayani humo kwani kuna umeme wa ziada.

Kuhusu usambazaji umeme katika mitaa na vijiji vya wilaya hiyo, Waziri aliitaka TANESCO kuhakikisha vijiji vyote 88 vya wilaya hiyo vinaunganishiwa umeme kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mkuranga, Mkuu wa Wilaya hiyo, Filberto Sanga aliishukuru serikali na kupongeza jitihada za wizara ya nishati katika kusambaza nishati ya umeme na gesi kwa wananchi.

Aliomba wilaya yake ipewe kipaumbele kwa kupatiwa umeme zaidi kutokana na uwepo wa viwanda vingi. Mkurugenzi Mtendaji wa Lodhia, Sailesh Pandit, alisema Wizara ya Nishati, kupitia TPDC na TANESCO imekuwa ikiwapa ushirikiano mkubwa katika

kuongeza tija ya uzalishaji wao kwa kuwapatia nishati wanayoihitaji pasipo vikwazo. Aliwaasa wamiliki wengine wa viwanda, kutumia gesi asilia kwani inapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji.

Kiwanda kingine ambacho kimeunganishiwa gesi asilia wilayani humo ni cha Goodwill Ceramics kilichopo kijiji cha Njopeka. Zoezi la kuunganisha wateja wengine linaendelea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...