Na Mwandishi Wetu 
MKURUGENZI wa Shirika la Vijana la TAYOA Peter Masika amesema kuwa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana na hivyo ni muhimu kuwapa nafasi ya kuonesha na kuendeleza vipaji vyao ili kutengeneza ajira kwao na kwa wengine. 

Pia ni vema wakapewa fursa ya kuonesha kazi zao za kiubunifu kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwani hiyo itawapa hamasa ya vijana kupenda kujitegemea, uzalendo, maendeleo na kuongeza kasi ya mafanikio ya kuondokana na umaskini wa kipato na usio wa kipato kwa kufanya kazi kwa juhudi ili kuleta maendeleo yao na ya jamii zao kupitia Vijanatz Talent Show. 

Masika amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa shukrani zake kwa vyombo vya habari nchini kwa mchango wao mkubwa ukiwemo wa kuandika habari za TAYOA na hatimaye kufanikiwa kuendelea kutekeleza malengo yake na hasa ya kuhakikisha kijana wa kitanzania anajitambua, anajiendeleza, anatafuta fursa za kujiajiri pamoja na kutoa elimu inayohusu afya. 

" TAYOA tumekubaliana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuhamasisha vijana kujitegemea na kujifunza kutoka kwa vijana wengine waliofanikiwa katika mazingira magumu zaidi ya wanayoishi. Nia ya shirika letu ni kuibua vipaji vya vijana na kuwasaidia kufikia ndoto zao kupitia teknolojia na mabadiliko ya fikra, tabia, uongozi, uzalendo, ujasiriamali ili waweze kutengeneza ajira mpya au wawe wanaajirika. 

"Pia kupitia Vijanatz Talent Show, TAYOA inatatafuta vijana wenye vipaji vya ubunifu, mawazo yenye tija kwa Taifa na ulimwengu na sio kulenga tasimia ambazo zimezoeleka kwenye utafutaji wa vipaji has kwenye sanaa ya musiki na filamu,"amesema Masika. 

Ameongeza kwamba ili kuondokana na mkwamo wa kimaendeleo ni lazima sekta binafsi na ya umma zifanye kazi kwa pamoja kuibua na kuvikuza vipaji vya ubunifu na kuvibadilisha kuwa fursa na ajira. Alieleza Mungu huwaga vipaji kwa uwiano katika nchi zote duniani. 

"Hivyo ni juu yetu sisi waafrika kuwatambua wale wenye vipaji, tuwapende na kuwaendeleza ili wawe chachu na watengeneze fursa mpya na ajira kwa wengine, kwani kama wote tungekuwa wakurugenzi, je ni nani angeandaa chakula au kulima mazao ya vyakula,"amefafanua. 

Hata hivyo ameeleza kufurahishwa na moyo ulionyesha wahariri kwa kukubali kutoa kipaumbele kwenye habari za vipaji ambayo vinaweza kutengeza ajira zinazowalenga vijana na kuleta maendeleo tokana na ndoto zao. Alisema kupitia maonyesho mbalimbali ya vipaji vya vijana (Vijanatz Talent Show), asasi ya TAYOA ikishirikiana na wahariri wanategemea kufungua hazina ya vipaji iliyo ndani ya vijana wa kike na wa kiume kupitia Tehama, fikra chanya, malezi bora na tabia nzuri. 



“Mashindano hayo ya vipaji vya vijana Tanzania yatazingatia kanuni zifuatazo; moja, kujenga uwezo wa ubunifu kwa vijana kwa kuwawezesha waone changamoto zinazowazunguka kama fursa na hivyo kuwashaa tamaa ya kupata maendeleo kupitia ubunifu na mawazo chanye ili kubadilisha hali inayowazunguka. Pili, kuzingatia weledi katika shughuli zote wanazofanya ikiwemo kuhakikisha wanafanyakazi kwa bidii, uaminifu, uzalendo na kwa ufanisi na ufasaha kwa kila fursa wanayoipata. 

"Tatu, kuwawezesha vijana kuondokana na mazingira hatarishi kwa kuwajengea uwezo wa kutumia rasilimali binafsi na za kijamii na kubadili mitazamo isiyo na tija Nne, kuimarisha uwajibikaji kwa kuwawezesha kutimiza majukumu yao huku wakizingatia uaminifu, uadilifu na uwazi. Tano, kukuza ushirika wa vijana kwa kuhamasisha ushirikiano kati ya vijana wenye vipaji na wenzao ili kutengeneza fursa na ajira mbalimbali kwenye mazingira wanayoishi,"amesema. 

Kuhusu maono ya TAYOA ,Masika amesema ni kuona vijana wa kike na kiume wenye uwezo wa kujimudu na kujitejemea ambao wanaoishi maisha bora na wenye afya njema. Katika miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, shirika hilo limeweza kutoa huduma ya ushauri wa kiafya kwa vijana na watu wazima wapatao milioni 3.5 kupitia huduma za simu za bila malipo kwenda namba 117. 

Pia amesema asasi hiyo imekuwa ikitoa huduma za upimaji wa virusi vya Ukimwi na uwezeshwaji kiuchumi ikiwalenga wasichana na wavulana balehe hasa wanaotoka maeneo ya vijijini na kusisitiza TAYOA imewajengea uwezo wa kutumia Tehama kwa manufaa chanya kupitia tovuti ya vijanatz ambayo hutoa mafunzo na taarifa za ajira kila siku ambazo pia zinapatiakana kupitia simu za kiganjani. 

Hata hivyo amesema kutokana na kupungua kwa hamasa ya usomaji kwa vijana, TAYOA imejikita kutengeneza taarifa za kitaalam na mafunzo kupitia sauti na picha zilizorekodiwa katika studio zake na kuzitumia katika kuwajengea vijana uwezo, stadi mbalimbali na taaluma muhimu katika maisha yao. 

"TAYOA inaamini kwa kupitia fursa hii mpya ya Vijanatz Talent Show, vijana wa kike na kiume wataonyesha vipaji vyao vya kiubunifu ambavyo vinatatua matatizo yanayowazunguka na kuleta mapinduzi makubwa kwa kizazi kijacho cha vijana kwa Afrika inatarajiwa kuwa na nguvu kazi ya vijana kubwa Zaidi duniani kwa miaka ijayo. 

"Kupitia makubaliano ya ushirikiano TAYOA na wahariri watafuatilia vipaji hivyo vya vijana na kuonyesha jinsi juhudi binafsi na moyo wa kupenda kujitegemea unavyoweza kutatua matatizo na kutengeneza fursa za ajira na utajiri kwa jamii yetu ambapo vijana wataweza kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia, kuwa kati ya nchi zinazojitegemea na zenye mchango maalum duniani kupitia rasilimali watu na asilia. 

"Kwa sasa asasi ya TAYOA inatekeleza miradi miwili ambapo mradi moja unawalenga vijana wa kike katika wilaya kumi za mikoa ya Morogoro(Ulanga, Kilombero na Malinyi), Dodoma (Kondoa, Kongwa, Bahi na Mpwapwa) na Singida Singida MC, Singida DC nas Iramba),"amesema Masika 

Ameeleza kuwa kama sehemu ya utekelezaji wa mradi TAYOA inatarajia kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wasichana walio katika umri wa kubalehe na wanawake vijana 11,000 kutoka kaya masikini zilizopo chini ya TASAF. Katika wilaya hizi wasichana wengine zaidi ya 113,445 watafikiwa na huduma mbalimbali za afya na kinga dhidi ya VVU na UKIMWI. Mradi huu unatekelezwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee wa watoto na AMREF kwa ufadhili wa Global Fund. 

Amefafanua kuwa katika mikoa saba ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Kagera, Simiyu, Mara na Kigoma, TAYOA inafanya kazi Kwa kushirikiana na Intrahealth chini ya udhamini wa watu wa Marekani kupitia CDC kutekeleza afua zinazolenga kutoa huduma za tohara kwa wanaume hususani wale wenye umri kati ya miaka 25 hadi 29. Mwaka huu TAYOA ina lengo la kufikia jumla ya watu 48,000. Huduma za Tohara zinalenga kupunguza uwezekano wa wanaume kupata maambukizi ya VVU. 
Mkurugenzi wa Shirika la Vijana la TAYOA Peter Masika(anayepiga makofi) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa TAYOA Balozi Charles Sanga, baadhi ya wahariri na vijana wakati wa uzinduzi wa programu ya kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana nchini.
Mkurugenzi wa Shirika la Vijana la TAYOA akizungumza wakati wa kikao maalum cha kutoa shukrani kwa vyombo vya habari kutokana na mchango wao mkubwa wa kuandika habari za shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Vijana la TAYOA Balozi Charles Sanga akifafanua jambo na hasa kuhusu umuhimu wa vijana kutengeneza mazingira ya kutumia fursa zilizopo nchini kujitegemea na kujenga utamaduni wa kuwa wazelendo kwa nchi yetu.
Mkurugenzi wa Shirika la Vijana la TAYOA Peter Masika akifafanua jambo wakati wa kikao hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...