Na Chalila Chibuda
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kwa waangizaji wa bidhaa na mawakala wa forodha nchini ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa bila kuathiri taratibu na sheria za nchi. 

Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Upimaji na Ugezi wa shirika hilo, Johanes Maganga, alisema washirika hao watapatiwa kuhusiana na taratibu za uingizaji wa bidhaa nchini pamoja na usajili wa maghala ya kuhifadhi bidhaa za chakula na vipodozi.

Maganga alitaja maeneo mengine ambayo walipatia elimu kwamba ni   kuhusu taratibu za kufanya maombi kwa njia ya mtandao (OAS) pamoja na kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, hususan kwenye masuala ya viwango na mifumo ya udhibiti ubora.

Wadau hao walipatiwa elimu hiyo jijini Dar es Salaam jana kupitia semina waliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). 

Kwa mujibu wa Maganga wengine walioshiriki semina hiyo ni wawakilishi kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), wawakilishi kutoka Shirikisho la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) na wadau wengine.

Maganga alisema, ili kutimiza majukumu ya shirika hilo ni muhimu kwa umma wa Watanzania kwenda sambamba na mikakati mingine ya kitaifa. 

Alisema shirika hilo limeendelea kutoa semina kama hizo kwa waagizaji wa bidhaa mbalimbali zitokazo nje na mawakala wa forodha katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga.

"Lakini tumepanga kufanya semina kama hii katika Mkoa wa Mbeya hivi karibuni," alisema. Alifafanua kwamba kwa kuzingatia kifungu cha 36 cha sheria ya viwango Na: 2 ya mwaka 2009, Serikali ilipitisha kanuni ya udhibiti wa shehena kupitia notisi ya Serikali Na: 405 ya Desemba 25, 2009.

Alisema kanuni hizo ziliipa TBS mamlaka ya kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia nchini kabla ya kusambazwa kwenye soko la ndani.

Kwa mujibu wa Maganga, Februali mwishoni, mwaka 2012 ndipo shirika lilianzisha mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini (PVoC) kama mpango wa kudhibiti ubora wa bidhaa katika nchi zinakotoka, ambao unasaidia kutatua changamoto zinazokuwepo wakati bidhaa zinapokuwa zinakaguliwa baada ya kufika nchini.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya mifumo ya uondoshaji wa shehena bandarini kwa kutumia mfumo wa kielektroni, hasara  ambazo wafanyabiashara walikuwa wanapata kutokana na kuharibiwa kwa bidhaa zinazopatikana kutokidhi viwango, hasara kwa Serikali kupitia matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa hizo na athari kwa mazingira wakati wa uteketezaji wa bidhaa zilizofeli vipimo.  

Akitoa mada kwenye semina hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Bidhaa baada ya kuwasili nchini, Athuman Kissumo, aliwaeleza washiriki kuhusiana na faida za uamuzi wa Serikali kurejesha TBS majukumu yaliyokuwa yakisimamiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Hiyo ni kutokana na mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo yameleta mabadiliko katika sheria ya viwango Na: 2 ya mwaka 2009, ambapo majukumu ya kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi yanafanywa na shirika hilo.

Alitaja huduma zinazotolewa na shirika hilo kwa sasa kuwa ni usajili wa jengo, kusimamia masuala ya usalama na ubora wa chakula na vipondozi na upimaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi kwa lengo la kudhibiti ubora.
Majukumu mengine ni utoaji wa leseni au cheti cha TBS kwa bidhaa za chakula na vipodozi na usajili wa bidhaa za vyakula na vipodozi vinavyotoka nje ya nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...