Uwezo wa watalaam wazalendo kuwasha vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implants) watoto waliopandikizwa vifaa hivyo ambao walizaliwa wakiwa hawasikii sasa umeongezeka kufikia 100% huku kiwango cha kufanya upasuaji wenyewe kikifikia 90%.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili, (MNH) Dkt. Sufiani Baruani amesema baada ya upasuaji watoto hawa husubiri kipindi cha mwezi mzima ili waweze kuwashiwa vifaa husika. 

“Katika kuwasha vifaa hivyo, tulikua tukitegemea watalaam kutoka nje, lakini kwa sasa tunafurahi kuwa eneo hilo nalo tayari tumeliweza kwa 100% na leo tutafanya wenyewe bila kusaidiwa” amesema Dkt. Baruani. 

Ameongeza kuwa hatua hii inaashiria kuwa sasa huduma hizi nchini zitafanyika katika mfumo endelevu unaowezesha watalaam wa ndani kufanya wenyewe bila kutegemea watalaam wa nje. 

“Tangu kuanzishwa kwa huduma hii nchini Juni, 2017 wagonjwa 30 wamepandakizwa vifaa hivyo kati yao watoto ni 29 na mtu mzima mmoja. Huduma hii imekua ikitolewa kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji kutoka nchini Misri ambapo mwanzoni watalaam wazalendo walikua wakisaidia lakini hivi sasa watalaam wanafanya wenyewe kwa 90%” amesisitiza Dkt. Baruani.

Amesema upandikaji wa wagonjwa 30 uliofanyika ndani ya miezi 26 ni sawa na 60% ya wagonjwa 50  waliopelekwa nje ya nchi katika kipindi cha miaka 13 tangu Serikali ilipoanza kupeleka wagonjwa hao mwaka 2003 hadi 2016.

Amebainisha kuwa mpaka sasa, Serikali imetumia kiasi cha Tshs. 1.1 bilioni kuhudumia wagonjwa 30 kwa gharama ya Tshs. 37 milioni kwa mgonjwa mmoja na kama wangeenda nje ya nchi ingegharimu Tshs. 3 bilioni sawa na Tshs. 100 milioni kwa kila mgonjwa hivyo kuokoa Tshs. 1.89 bilioni.

Dkt. Baruani amesisitiza kuwa Hospitali imehakikisha utoaji wa huduma hizi unazingatia mahitaji na uwezo halisi wa mgonjwa anayehitaji huduma hii ambapo kwa sasa inagarimu mgonjwa kiasi cha Tshs. 37 milioni gharama hii ni kubwa kwa kuwa kifaa vya usikivu pekee yake kinagharimu kiasi cha Tshs. 31 milioni kwa mgonjwa mmoja na upasuaji Tshs. 6 milioni.
 Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Sufian Baruani(katikati) akitoa taarifa leo kuhusu uwezo wa watoa huduma wazalendo kuwasha vya vifaa vya kusikia kuongezeka hadi 100%. Pembeni yake ni Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Pua, Koo na Maskio, Dkt. Aveline Kahinga na Dkt. Shaban Mawala.
 Wa pili kushoto, aliyekaa ni Bw. Waisai Wambura (55) akifurahi mara tu baada ya kuwashiwa kifaa alichopandikizwa (cochlear implant) na kusikia tena upya sauti. Bw. Wambura alipoteza uwezo wa kusikia ukubwani sasa anaweza kusikia tena.
 Bw. Waisai Wambura akiongea jambo na waandishi wa habari mara tu baada ya kusikia tena sauti. 
Mmoja wa watoto akielekezwa kupokea sauti mara tu baada ya kuwashiwa kifaa alichopandikizwa mwezi mmoja uliopita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...