Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge ametoa wito kwa wafanyabishara jijini humo kuhakikisha wanachangamkia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha ili waweze kunufaika na ongezeko kubwa la fursa za kibiashara zinazoibuka katika jiji hilo ambalo ni makao makuu ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huyo wakati wa hafla ya jioni ya Uzinduzi wa Klabu ya wafanyabiashara ya Benki ya NBC ya mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi wa jiji hilo Bw Godwin Kunambi mbali na kuipongeza benki hiyo kwa mabadiliko makubwa ya kihuduma alisema ipo haja ya makusudi kwa wafanyabiashara wa jiji hilo kuitumia vema benki hiyo ili kupata nguvu ya kiuchumi itakayowawesha kufaidi vema fursa ya mabadiliko ya ukuaji wa uchumi katika jiji hilo.

“Dodoma kwasasa kuna utekelezaji wa miradi mikubwa mingi ikiwemo barabara, Stendi ya mabasi ambayo ni kubwa zaidi Afrika Mashariki, upanuzi wa uwanja wa ndege, ujenzi wa viwanja vya mapumziko ambayo vitachochea mzunguko mkubwa wa pesa na ongezeko la watu. Hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara kushirikiana vema na benki kama NBC ili kukuza mitaji itayowawezesha kufanya uwekezaji utakaowanufaisha na mabadiliko hayo,’’ alibainisha.

Alitolea mfano umuhimu wa wafanyabiashara hao kuwekeza kwenye sekta ya usafiri ambapo kwasasa serikali jijini humo ipo kwenye mpango wa kuondoa gari ndogo za abiria maarufu kama vipanya kwenye mizunguko ya mjini ili kutoa fursa kwa gari kubwa ‘coaster’ kufanya kazi hiyo.

Akizungumza kuhusu uanzishwaji wa Klabu hiyo, Mkuu wa Kitengo cha wateja wa Kati na Wadogo wa benki ya NBC, Bw Evance Luhimbo alisema pamoja na mambo mengine klabu hizo zinalenga kutoa mafunzo kwa wateja wa benki hiyo kuelewa mabadiliko ya uboreshwaji wa huduma za za benki hiyo, kuwakutanisha pamoja wajadili fursa za kibiashara sambamba na kuwajengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kibiashara ikiwemo masuala ya kodi na taratibu za kijiunga na taasisi wadau biashara ili ziwasaidie.

“Benki ya NBC kwasasa ipo kwenye mabadiliko makubwa ya kihuduma kwa wateja wateja wetu na ili mabadiliko haya yaweze kuwafikia wateja wetu ni vema kuwa nao karibu zaidi. Mbali na benki kuwajengea uelewa kama hudua zetu na taasisi wadau ikiwemo Chemba ya biashara, viwanda na kilimo (TCCIA)na Baraza la. Uwezeshaji (NEEC)na nyingine nyingi pia tumekuwa tukipokea maoni kutoka kwa wateja wetu yanayotuwezesha kubuni huduma zinazoendana na uhalisia wa mahitaji yao ya kifedha,’’ alisema.

Awali wakiwasilisha mada kwenye kongamano la uzinduzi wa Klabu hiyo muwakilishi wa TCCIA, Bw Patrick Magai na muwakilishi wa NEEC Bi Nyakao Mturi walitoa wito kwa wafanyabiashara wadogo kuunganisha nguvu ya kimitaji ili wapate nguvu ya pamoja itakayowawezesha kushiriki fursa kubwa za kibiashara ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao Bw Ponsian Rweyemela ambaye ni mfanyabiashara jijiji humo pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji pia aliiomba benki hiyo pamoja na taaisisi nyingine za kifedha kuongeza idadi ya mashine za kuweka na kutolea fedha (ATM) ilikuendana na ukuaji wa jiji hilo pamoja na ongezeko la watumiaji wa mashine hizo.
Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Bw Godwin Kunambi(kulia-mbele) akifurahia uzinduzi wa rasmi wa Klabu ya wafanyabiashara ya Benki ya NBC ya mkoa wa Dodoma uliofanyika katikati ya wiki jijini humo. Wengine ni baadhi ya wateja na maofisa wa benki hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya wateja wa kati na wadogo Bw Elibariki Masuke.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...