Na Karama Kenyunko, Michuzi Blog.

UPANDE wa Mashitaka katika kesi ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado inaendelea kuwatafuta washitakiwa wanne wanaodaiwa kumteka Mfanyabiashara, Mohammed Dewji maarufu MO.

Awali Mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala ambaye ni raia  wa Afrika Kusini.

Mshitakiwa mmoja ambaye ni dereva taksi na Mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb (46) tayari alishafikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amemueleza Hakimu Shaidi kuwa upelelezi wa kesi hiyo  haujakamilika na kwamba walitoa  hati ya kuwakamata washitakiwa hao, lakini bado hawajawapata hivyo wanaendelea kuwatafuta na wataieleza mahakama hatua waliyofikia.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Utetezi,  Robert Mtakula ameuomba upande wa mashitaka kuongeza jitihada za kuwatafuta kwa kuwa mshitakiwa mmoja yupo ndani kwa muda mrefu.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30, 2019.

Washitakiwa hao wakikamatwa wataunganishwa katika kesi hiyo kujibu mashitaka mawili ya  kumteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari na kuongoza genge la uhalifu.

Mapema ilidaiwa Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, mwaka huo huo, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum  wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Pia inadaiwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

MO alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...