Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akiongea na ujumbe wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) wakati alipofanya kikao ofisini kwake Dodoma.
 Mwalikishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani nchini Michael Dunford (wa pili kulia) akiwa timu yake wakati wa mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kutafuta soko la mahindi na Naibu Waziri wa Kilimo Husein Bashe (hayupo pichani). Nawasilisha.
 Naibu Waziri wa Kilimo Husein Bashe akifuatilia mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Chakula Duniani wakati wa kikao cha kujadili upatikanaji wa soko la mahindi na mtama nchini.
Picha ya pamoja kati ya Naibu Waziri wa Kilimo Husein Bashe (wa sita toka kulia) akiwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani Michael Dunford (wa nne toka kushoto) mara baada ya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kutafuta masoko ya nafaka nchini.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekubali kuwa na ushirikiano na Wizara ya Kilimo katika kutafuta soko la uhakika la mazao ya mahindi na mtama nje ya nchi.
Kauli hii imetolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe mara baada ya kufanya mazungumzo ofisini kwake na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani Michael Dunford.

Bashe amebainisha kuwa Wizara ya Kilimo ina mkakati wa kuhakikisha mahindi na mtama unaozalishwa nchini unapata soko la uhakika ili kuinua uchumi wa wakulima
“Wizara inataka kutumia uzoefu wa Shirika la Chakula Dunia katika kuyafikia masoko ili mazao ya wakulima wetu yaweze kupata bei nzuri katika soko la Afrika” alisema Naibu Waziri

Amewahakikishia WFP kuwa wizara imejipanga kuona uzalishaji wa mahindi na mtama unaongezeka na kuzingatia kiwango cha ubora kinachotakiwa na soko la nje.
Aliongeza kuwa kwa sasa serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wamewezeshwa ili wanunue na kuhifadhi nafaka kwa wingi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

“Ni lengo la wizara kuhakikisha wakulima nchini wanaunganishwa na fursa za masoko ya mazao yao ili uchumi wa nchi uendelee kukua kwa kasi kupitia sekta ya kilimo” alisema Bashe
Naibu Waziri Bashe alisema mkakati wa wizara katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ni kuona Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inakuwa na uwezo wa kuhifadhi kisasa nafaka tani 520,000 tofauti na ilivyo sasa ambapo tani 120,000 zinahifadhiwa,hivyo kuwa na uwezo wa kuuza nje.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani Michael Dunford amesema wanahitaji kununua zaidi ya tani 50,000 za mahindi toka Tanzania kwa ajili ya kusaidia nchi za Uganda na Sudan Kusini.
Dunford alisema kutokana na uzalishaji mzuri ulipo Tanzania kwenye zao la mahindi unatoa fursa ya soko la uhakika endapo vigezo vya ubora unaotakiwa na Shirika la Chakula Duniani utazingatiwa ikiwa ni pamoja na kupunguza tatizo la sumukuvu.

Ameishauri wizara ya kilimo kutumia uzoefu na teknolojia ya kisasa uliopo WFP katika kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno ili wakulima wapate ufanisi katika uzalishaji.
“Tanzania inapoteza asilimia 30 ya mazao ya wakulima baada ya mavuno kutokana na kukosekana kwa uhifadhi bora na teknolojia ya kisasa” alisema Dunford

Katika kuhakikisha ushirikiano huu unafikiwa,Dunford alisema Shirika la Chakula Duniani linahudumia chakula kwa watu zaidi ya milioni 150 duniani wenye uhitaji katika maeneo yenye migogoro na majanga ,hivyo Tanzania inayo fursa ya kupata soko la nafaka .
Makubaliano yamefikiwa kuwa wataalam wa wizara ya Kilimo na wale wa Shirika la Chakula duniani watakutana mapema mwezi Octoba mwaka huu kukamilisha agenda muhimu za ushirikiano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...