Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akimsikiliza mkazi wa Kijiji cha Losinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Martha Kuzilwa (94) ambaye ameporwa shamba lake. 

*****************************

Mkazi wa Kijiji cha Losinyai Kata ya Oljoro Namba 5 Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Martha Kuzilwa (94) amemshukuru Rais John Magufuli kwa kuingilia kati mgogoro wa shamba lake lenye ukubwa wa ekari 300 iliyoporwa na vigogo wa kijiji hicho na kuagiza arudishiwe. 

Kuzilwa amemshukuru Rais Magufuli baada ya Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti kufika nyumbani kwake na kumpa maagizo ya Rais Magufuli kuwa atapewa eneo lake lililoporwa.

Awali, Mnyeti alisema amefika nyumbani kwa Kuzilwa baada ya Rais Magufuli kumuagiza amsikilize na kumpa haki yake. Mnyeti alisema baada ya kuwepo mgogoro wa muda mrefu baina ya Kuzilwa na wavamizi hao wa ardhi alipeleka kilio chake kwa Rais Magufuli ambaye ameagiza apatiwe shamba lake. 

“Nimefika hapa nimemsikiliza huyu mama na viongozi wa kijiji wamekiri shamba ni lake hivyo namuagiza mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula, ikifika ili jumamosi ijayo akamkabidhi rasmi shamba lake,” alisema Mnyeti. 

Hata hivyo Kuzilwa alimshukuru Rais Magufuli kwa kuagiza arejeshewe shamba lake ekari 300 alilokuwa analimiliki tangu mwaka 1990 kisha akaporwa na kutishiwa maisha.

Alisema kila mara amekuwa akitishiwa maisha yake na watu watatu waliopora eneo lake la ekari 300 na kumuachia ekari 50 pekee. 

Pia, alimshukuru Mnyeti kwa kufika eneo hili na kumsaidia baada ya agizo la Rais Magufuli kwani hati zote anazo za kuhakikisha shamba hilo ni lake kihalali. “Mimi ni mwanachama wa CCM tangu enzi ya TANU hawa watu walikuwa wanataka kuniua sababu ya kunidhulumu shamba langu ambalo nimepata kihalali japokuwa kuna vigogo walikuwa wanawasaidia,” alisema. 

Alisema baadhi ya wavamizi wamejenga nyumba kwenye shamba hilo ambalo alilipata kihalali na ana hati halali za umiliki wake. 

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula aliahidi kutekeleza agizo hilo kwa kumkabidhi shamba hilo jumamosi ijayo baada ya kumalizika kwa ziara ya mkuu huyo wa Mkoa. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...