‘Malkia wa Mipasho’ Khadija Kopa

Na Moshy Kiyungi,Tabora.

Sifa za ‘Malkia wa Mipasho’ Khadija Kopa zimezagaa kila kona katika nchi zilizo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na nchi za Falme za Kiarabu, kufuatia uimbaji wake mwanana wa taarab.

Mama huyu ni mwimbaji, mtunzi na mtayarishaji wa rekodi nyimbo za taarabu pia ni mfanyabiashara maarufu.

Khadija Kopa amejizolea sifa lukuki akiwa na kikosi hicho kwa kuimba nyimbo zenye mipasho, inayopendwa na wapenzi na washabiki wa muziki wa taarab humu nchini.

Mara baada ya kuzaliwa mwaka 1963, Kisiwani Zanzibar, alipewa jina la Khadija, akiwa ni mtoto wa kipekee katika familia ya Omar Abdallah Kopa.

Alivyojiunga Culture Musical Club.

Siku moja alikuwa amekaa nyumbani kwao huku akiiga kuimba wimbo, akapita babu yake aliye katika kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar. Babu huyo akamsifia ya kwamba anajuwa kuimba.

Baada ya sifa hizo, Kopa akajiona anatosha kujiunga katika kundi kubwa la muziki huo, akachukuwa hatua ya kuandika barua pasipo kumshauri babu yake, akaipeleka kwenye uongozi wa Culture Musical Club akiomba ajiunge nao.

Alikubaliwa na kuweza kufanya kazi ya kuimba nyimbo za taarab tangu mwaka 1990, katika kundi lake la kwanza la Culture Musical Club ya mjini Zanzibar.

Wakati akiwa Culture Musical Club, umaarufu wake ulionekana baada ya kuimbaji kwa mahiri mkubwa kupitia sauti yake maridhawa.

Kopa aliimba vibao vya kama vile “Kadandie”, “Daktari” na “Wahoi”, alivyoviimba akiwa katika kikundi cha Culture Musical Club, ambavyo vilimpa umaarufu mkubwa visiwani Zanzibar na Pemba.

Sifa zake zikatambaa hadi Tanzania bara, ambako uongozi wa TOT Plus, ulifanya mchakato wa kumfuata Khadija Kopa visiwani Zanzibar, wakamuomba ajiunge na kikundi hicho.

Sababu kubwa ilikuwa ni kukipa sura na mwonekano mpya, tofauti na tasnia ya taarab iliyozoweleka Tanzania Bara.

Khadija Omar Kopa aliamua kuhamia jijini Dar es Salaam baada ya kushawishiwa na uongozi wa Tanzania One Theatre (TOT), kujiunga nacho, kikiongozwa na Kapteni mstaafu John Damian Komba mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Awali baadhi ya washabiki wa muziki huo hususan katika jiji la Dar es Salaam, hawakuwa wakifahamu uwezo wake katika kuimba. Waliomuona kama mwimbaji wa kawaida, tofauti na mashabiki wa taarab wa visiwa vya Zanzibar, jina la Khadija Kopa lilikuwa kubwa mno.

Kopa licha ya kuimba taarab, amekuwa mstari mbele katika uimbaji wa kwaya ya TOT, akishirikiana vyema na Kapteni mstaafu John Komba (marehemu) pamoja na waimbaji wengine wa TOT wakiwamo akina Abdull Misambano, Mwanamtama Amir na Gasper Mapunda.

Nguli huyu hujichanganya kupiga muziki na baadhi ya bendi za muziki wa dansi, ambazo humualika kuongeza sauti nyororo katika nyimbo zao.

Mfano wa karibu ni pale aliposhirikiana vyema na wanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu, wakatengeneza video ya wimbo wa ‘Chanzo ni Wanaume’. Kopa ameonekana akiimba kwa kupokezana na waimbaji wa bendi hiyo Jose Mara na Kharid Chokoraa.

Adiha aliwahi kushirikiana na msanii wa Bongo fleva, Diamond Platnumz, aliyekuwa kiongozi wa kundi la taarab la Jahazi, Alhaj Mzee Yusuph.

Khadija pia amepata kushirikiana na waimbaji wengine wa kike kama vile Mwanamtama Amir, marehemu Leila Khatib na wanaume kama akina Abdul Misambano na Ali Star ‘Sharo Babu’.

Waliporomosha nyimbo ambazo zilitamba miaka hiyo kupitia mashairi maridadi yaliyotungwa na kuimbwa na nguli hao.

Kopa ni mama mwenye watoto wanne na wajukuu wawili, pia hujishughulisha masuala ya siasa ambapo alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya CCM.

Historia ya Khadija Kopa katika muziki inaeleza kuwa alikuwa akipenda kuimba tangu akiwa mdogo. Kopa alisoma masomo ya Koraan kwenye madrasa mjini Zanzibar, ambako alikuwa akighani sana Kaswida.

Mambo ya siasa aliyaanza wakati alipokuwa akiandaliwa katika kundi la watoto Young Pioneer, upande wa kwaya.

Kopa alipokuwa shule ya msingi, alikuwa akiimba na kucheza kwenye kundi la ngoma za utamaduni na kwaya. Shule yao ilikuwa bingwa kwa kwaya visiwani humo.

Muonekano wa Kopa

Kwa umbo, Khadija Omar Kopa ni mnene ‘Shibonge’ mwenye rangi nyeusi yenye mng’ao wa kumeremeta.

Licha ya kuwa na umbile hilo, ni mwepesi wa kuzunguusha maungo yake atakavyo awapo jukwaani.

Kopa anaweza kuwashukia washabiki, akanengua nao huku akiwaachia vibwagizo kemkem ukumbini.

Sauti ya Khadija Kopa haiigiki kwamwe, ni ya aina yake yenye mikwaruso fulani, wakati akiimba.

Aidha macho yake yenye mvuto yaliyotulia kwenye paji lake la uso ukiwa na tabasamu tele muda wote utadhani hajui kitu kinachoitwa kukasirika.

Khadija Kopa anao uwezo mkubwa wa kujibu ‘mapigo’ kwenye nyimbo zake dhidi ya mahasimu wake. Pia anaweza kuongeza vionjo vya ‘mipasho’ katika wimbo, kufuatia tukio lililopo ukumbini pasipo kuwaarifu wasanii wenzake jukwaani

Sifa hizo ndizo zilizomfanya mwanamama huyo apachikwe jina la ‘Malkia wa Mipasho’ nchini, ambapo yaelezwa kuwa waliompa jina hilo hawakubahatisha, walitambua vyema kwamba uwezo wake katika tasnia hiyo ni mkubwa.

Kopa akiwa TOT Plus mwaka 1992, alidhihirisha kwamba hawakukosea kumfungia safari hadi Visiwani humo, baada ya kung’ara kwa vibao kama “TX mpenzi”, “Ngwinji”, “Wrong Namba”, “Mtie kamba mumeo” na nyinginezo.

Miaka miwili baadaye, Khadija Kopa alikorofishana na uongozi wa TOT Plus, baada ya yeye na mwimbaji mwenzake, Othman Soud wakaamua kuondoka kinyemela na kwenda Dubai ambako walishiriki kuanzisha kundi la East African Melody.

Baada ya kurejea nchini kutoka Dubai, Khadija Kopa alilazimika kujiunga na kikundi cha Muungano Cultural Troupe kwa kuwa uongozi wa TOT uligoma kumpokea.

Kujiunga kwa Khadija na Othman Soud katika kikundi cha Muungano, kulisababisha kuwepo kwa ushindani mkali kati ya vikundi hivyo viwili.

Baadaye vikundi hivyo vikawa vikifanya maonyesho kadhaa ya pamoja kwa ajili ya kuonyeshana nani mkali.

Akiwa Muungano, Khadija aling’ara kwa vibao vyake murua kama vile “Homa ya Jiji”, “Kiduhushi” na “Umeishiwa”.

Pia kulizuka ushindani mkali kati yake na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’, ambaye alichukuliwa na TOT, kutoka Muungano Cultural Troupe kwa lengo la kuziba pengo lake.

Akizungumza mjini Dar es Salaam hivi karibuni, Khadija Kopa alikiri kwamba asingeweza kufika mahali alipo bila ya kupata msaada mkubwa kutoka kwa Othman Soud.

“Othman ndiye aliyekuwa mtunzi wa nyimbo zote nilizokuwa nikimba tangu nikiwa Culture na TOT.

Hata TOT waliponifuata Zanzibar, niliwaambia kwamba nisingeweza kujiunga na kikundi hicho bila ya Othman Soud, bila yeye nisingeweza kufanya lolote la maana,” alisema Khadija Kopa.

Kwa sasa, Othman ni askari wa Jeshi la Magereza visiwani Zanzibar.

Uamuzi Othman Soud kuacha kujihusisha na muziki wa taarab, kulimuathiri kwa kiasi kikubwa Khadija Kopa, ambapo alilazimika aanze kuchacharika na kutunga nyimbo zake mwenyewe.

Khadija Kopa alikiri kuwa ushindani wa kimuziki uliokuwepo kati ya TOT na Muungano Cultural Troupe, ulisaidia kwa kiasi kikubwa kuinua hadhi ya muziki huo.

Alisema haitatokea kwa vikundi viwili vya taarab nchini kuwa na ushindani kama huo.

“Kila tulipofanya maonyesho ya pamoja, kumbi zilifurika, iwe Dar es Salaam, Morogoro au Mwanza, mashabiki walikuwa wakifurika ukumbini kutushuhudia.

“Ni ushindani uliosababisha mashabiki wetu wajenge uhasama mkubwa, lakini sisi wasanii tulikuwa kitu kimoja. Wengine walidhani mimi na Nasma tulikuwa na uadui kutokana na nyimbo tulizoimba, kumbe tulikuwa marafiki wakubwa na tulisaidiana kwa kila hali,”alisisitiza Khadija Kopa.

Amekiri kuwa ushindani wa taarab umepungua katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwepo kwa utitiri wa vikundi vya muziki huo.

Aidha, alisema maonyesho ya vikundi hivyo vimekuwa vikifanyika muziki kuanzia Jumatatu hadi Jumapili, hivyo kuwafanya wasanii wake kuchoka na kukosa ubunifu.

“Kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa baadhi ya vikundi vya mitaani vimekuwa vikiimba nyimbo za vikundi vingine katika maonyesho yao, ambayo yamekuwa yakifanyika bure hadi mashabiki wanachoka.

“Utakuta kikundi kimoja kinafanya onyesho mtaa huu, kingine kinafanya onyesho mtaa wa pili. Huyu akisikia mwenzake amekwenda kufanya maonyesho Lindi na mwingine naye anakwenda huko huko”, alifafanua Khadija Kopa.



Ushoga na taarab.

Akizungumzia madai ya kuwepo kwa uhusiano kati ya muziki wa taarab na Ushoga, Khadija alisema si kweli kwa sababu kumjua shoga kunahitaji ushahidi wa uhakika.

“Ushoga ni nafsi ya mtu kupenda kitu, si maumbile au mwonekano wake,”alisisitiza mwanamama huyo.

Mwimbaji huyo alieleza kusikitishwa kwake kwa tabia ya baadhi ya mashabiki wa muziki huo, hasa wanawake, kucheza kwa kukata viuno na pia kuvaa mavazi yanayowaonesha wakiwa nusu uchi.

Alisema japokuwa kukata viuno ni asili ya Mwafrika, lakini uvaaji wa mavazi ya nusu uchi si wa kistaarabu, umepitiliza na unachangia kushusha hadhi ya muziki huo na kuufanya uonekane kuwa wa kihuni.

“Tatizo hili halipo kwenye muziki wa taarab pekee, hata hip hop muziki wa dansi na bongo fleva, utakuta wacheza shoo wa kike wamevalishwa nguo za nusu uchi. Mbona wanaume hawavai nguo za aina hiyo”. Alihoji msanii huyo.

Amesema imefikia hatua hivi sasa, mzazi hawezi kutazama televisheni akiwa na watoto wake, vinginevyo analazimika kuwa na ‘remote’ mkononi ili kukitokea tukio la aibu, aweze kuzima televisheni mara moja ama kukimbilia nje ili kuepuka aibu.

Khadija amekiri kuwa umaarufu kwa wasanii ni mzuri, lakini wakati mwingine umekuwa ukiwasababishia madhara ya aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuzushiwa mambo ya uongo.

“Binafsi niliwahi kuzushiwa kwamba nilimuua mwanangu Omar Kopa, eti nijiongezee umaarufu baada ya kuonekana amenizima.

Hata Leila Khatib alipokufa, niliambiwa kwamba mimi ndiye niliyemuua!”alizungumza kwa uchungu Khadija Kopa.

Aliongeza kuwa, mbaya zaidi siku ambayo Leila alizikwa, hakuweza kuhudhuria kwenye mazishi kutokana na yeye kufiwa na bibi yake, hali iliyozidisha uvumi huo.

“Ukiwa msanii mzuri, unageuzwa kama Malaika mtoa roho. Msanii mwenzako akiumwa, unaogopa hata kwenda kumuangalia,” alisema.

Khadija amekielezea kifo cha aliyekuwa mkurugenzi wa kikundi cha TOT Plus, Kepteni mstaafu, John Komba kuwa ni pigo kubwa katika fani ya sanaa nchini.

Amesema si rahisi kwa pengo la Kepteni Komba kuzibika kutokana na vipaji alivyokuwa navyo, isipokuwa anaweza kutokea msanii atakayeleta ahuni.

“Kuziba pengo lake si rahisi, litabaki kama lilivyo,”alisisitiza msanii huyo, ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa TOT.

Kopa alisema kinyume na uvumi kuwa kundi la TOT taarab limesambaratika, siyo kweli bado lipo na linaendelea kuwakonga nyoyo za wapenzi mashabiki wake.

Amesema TOT ni kikundi kikubwa kinachokuwa katika shughuli nyingi zikiwemo siasa wakati mwingine hata za serikali.

Mwimbaji Khadija Kopa ametamka kuwa anao mipango ya kutoa albamu yake ya kibinafsi, tayari wimbo wake “Mji ni Chuo Kikuu” unachezwa na vituo vingi vye redio.

“Katika TOT tumetoa albamu hivi juzi juzi. Hii yaitwa Fullstop, tunajitayarisha kufanya mkanda wa video. Lakini mimi mwenyewe nataka kutoa albamu yangu Mji ni Chuo Kikuu. Itakuwa na nyimbo nne ambazo baadhi nimewashirikisha Fatma Issa na Saada Mohamed” alisema Khadija Kopa.

Aidha amewataka wapenzi wa muziki wa taarab wasiwe wepesi wa kutaka kusikiza nyimbo zilizotengezwa vichochoroni na watu wasiowajali waimbaji halisi.

Kila kazi ina mafanikio, miongoni mwa mafanikio aliyoyapata Khadija kutokana na muziki huo, ni pamoja na kutembelea nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani.

Pia amefanikiwa kuanzisha kundi lake linalojulikana kwa jina la Ogopa Kopa Classic Music.

Kundi hilo linaundwa na wasanii wasiozidi 10, akiwemo mtoto wake wa mwisho wa kiume, anayefahamika zaidi kwa jina la Black Kopa.

Moja ya malengo yake ni kurekodi upya nyimbo zake zote alizowahi kuziimba akiwa katika vikundi mbalimbali.

Khadija iwapo mipango yake hiyo itafanikiwa, anatarajia kuanzisha miradi mbalimbali ya kikundi kwa lengo la kuwaongezea wasanii mapato.

Pia amepanga kuwashawishi wasanii wake wajiunge na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kujiwekea akiba kwa maisha yao ya baadaye.

Khadija hakuwa tayari kuzungumzia kwa kirefu ndoa yake na mumewe, aliyefariki mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, ambaye inadaiwa alikuwa na umri mdogo kuliko yeye.

Ndoa yake

Alisema halikuwa jambo la ajabu kwake kuolewa na mwanaume mwenye umri mdogo kwa sababu hata Mtume Muhammad SAW na mkewe Khadija, walifunga ndoa wakiwa wanatofautiana umri kwa miaka mingi.

“Mume wangu alikuwa anajuwa kunitunza, nikienda kwenye maonyesho alikuwa akinifuata, tunarudi nyumbani pamoja, sijui kama naweza kumpata mume mwingine bora kama yeye. Kama atajitokeza, itabidi nimchunguze sana,”alisema Khadija huku akitabasamu.

Khadija ametoa mwito kwa wasanii wa muziki wa taarab kuwa na umoja kama ilivyo kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ikiwa ni pamoja na kurekodi nyimbo pamoja.

“Inasikitisha kuona sisi wasanii wa muziki wa taarab, hatuna uwezo wa kufanya hivyo. Bongo fleva wanaungana na kuimba pamoja, lakini sisi hatuna uwezo huo. Mbaya zaidi hatuna mapromota na mameneja wa kutuvusha kutoka hapa tulipo,”alilalamika.

Taarab Nairobi.

Licha ya kuhusishwa kuwa muziki wa taarab ni mhsusi kwa wakazi wa Pwani, miaka ya hivi karibuni muziki huo umeibuka kuwa maarufu mno jijini Nairobi nchini Kenya.

Unapotaja taarab jijini humo, mtaje pia Khadija Kopa ambaye mashairi yake huwaacha mashabiki wake wakipagawa.

‘Malkia wa Mipasho’ anashabikiwa mno kwa nyimbo zake za kuwapa vidonge vyao, kila anapotangaza kuandaa shoo jijini Nairobi, tiketi huuzwa na kuisha kabla ya siku ya tamasha.

Alipokuwa na tamasha jijini Nairobi hivi karibuni, mama huyo alivutia mno na mashabiki wa rika tofauti ambao si kawaida kwao kufika katika matamasha. Tamasha hilo lililodhaniwa na Wakongwe hasa wale wa Pwani.



Ulanguzi wa kazi zao.

Mwimbaji huyu mwenye jina kubwa Afrika Mashariki, amelalamikia kuhusu ukosefu wa ushirikano wa kutosha kutoka kwa mashabiki ambao kwa kawaida wanapenda kununua kanda zilizo kughushiwa, zile zilizonaswa na walanguzi na badala yake kuziacha za wasanii halisi.

“Tunatengeneza nyimbo zetu halafu sisi wenyewe hatufaidiki, watu wanaingilia kazi zetu. Kwa mfano mimi nimeanza kuimba muda mrefu sasa, lakini bado kazi zangu hazijaniletea faida”, alilalamika Kopa.

Khadija Omar Kopa ndiye aliyeviporomosha vibao kadhaa vikiwamo vya “Y2K”, “Utaishia Kunawa”, “Top In Town”, “Full Stop”, “Full Kujiachilia”, “Gendaeka”, “Mambo iko Huku”, “Nalijua Jiji” ni miongoni mwa zingine nyingi.

Mwisho.

Mwandaaji wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0767331200 na 0713331200.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...