Na Karama Kenyunko, globu ya jamii.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ifikapo Novemba 21, mwaka huu kuleta mahakamani uthibitisho wa maendeleo ya afya ya Lissu.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefikia hatua hiyo baada ya kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu kusimama kusikilizwa kwa takribani miaka miwili kwa sababu mshtakiwa huyo anaumwa yuko Ubelgiji.

Mapema, wakili wa Serikali, Estazia Wilson alidai mahakamani hapo kuwa, kesi hiyo leo ilikuja kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi wa shahidi wa upande wa mashtaka lakini haiwezi kuendelea kwa sababu mshtakiwa Lissu hayupo.


Mdhamini wa mshtakiwa huyo, Robert Katula alidai Lissu bado anaumwa yuko nje ya nchi.Kufuatia taarifa hiyo, hakimu Simba amemuamuru mdhamini tarehe ijayo ya kesi afike na uthibitisho wa maendeleo ya mshtakiwa na kesi imeahirishwa hadi Novemba 21 mwaka huu.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Alidai mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...