Na Said Mwishehe, Michuzi Tv


Mmoja ya wanakwaya ya Gethmane ya Kanisa la SDA Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam akikabidhi zawadi kwa mgonjwa wa Fistula ambaye anatakiwa matibabu katika Hospitali ya CCBRT .Kwaya hiyo unaotarajia kuzindua DVD mbili Oktoba 13 mwaka huu ambapo tukio la leo ni sehemu ya kuelekea katika uzinduzi huo

WAIMBAJI wa kwaya ya Gethmane ya Kanisa la Waadventista wasabato (SDA) Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam wametoa misaada kwa wagonjwa Fistula waliopo katika Hospitali ya CCBRT ikiwa ni sehemu ya kuonesha matendo ya huruma kwa wenye uhitaji.

Kwaya hiyo ikiongozwa na Masunya Anthony ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la SDA Mtaa wa Kinondoni, Mzee wa Kanisa Emmanuel Mgonja pamoja na Mlezi wa kwaya hiyo wametoa msaada huo leo hospitalini hapo ikiwa ni sehemu ya kuelekea Oktoba 13 mwaka huu ambapo kwaya hiyo inatarajia kuzindua DVD mbili katika ukumbi wa Uhuru JKT Mwenge jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza mbele ya wagonjwa hao wa fistula, madaktari na wauguzi, waimbaji wa kwaya hiyo wamesema wanatambua umuhimu wa kutoa msaada kwa jamii yenye uhitaji na ndio maana wamefika katika hospitali hiyo na kutoa japo kidogo ambacho wamejaaliwa kuwa nacho.

Akizungumzia msaada huo, Mwalimu wa kwaya hiyo Stella Malingoza amesema kuwa, mwaka huu kwaya hiyo imetimiza miaka 10 na wanajiandaa kuzindua DVD zao mbili Oktoba 13 mwaka huu hivyo wameona ni vema kabla ya kufanyika kwa uzinduzi wakatoa msaada huo ambao ni sabuni, mafuta ya kupakaa, dawa ya meno na miswaki.

"Kwaya yetu ya Gethmane tumekuwa na utamaduni wa muda mrefu wa kujitoa kwa misaada ya aina mbalimbali, tunaweza tusiwe tumetoa msaada mkubwa lakini kile ambacho tunakipata huwa tunakipeleka kwenye jamii ambayo ina uhitaji.Hivyo tumekuja CCBRT kwa ajili kuwaona mama zetu na dada zetu wenye kusumbuliwa na ugonjwa fistula na kadri tutakavyopata tutarudi kwao na kwa wengine.

"Thamani ya msaada wote ambao tumeutoa katika wodi hii ya wagonjwa fistula una thamani ya zaidi ya Sh.milioni 2.4.Tunajua wanakabiliwa na changamoto nyingi na wanamahitaji mengi lakini hiki kidogo ambacho tunacho tumeona tuwaletee na kuwakabidhi,"amesema Stella.

Pia ametumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa Watanzania bila kujadili itikadi za dini kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya Oktoba 13 ambayo itakuwa siku maalumu ya uzinduzi wa nyimbo zao mpya ambapo watazindua DVD na hakutakuwa na kiingilio.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa hilo Masunya Athony ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa watu wanapokuwa wagonjwa wakati mwingine inakuwa ngumu kupata neno la Mungu kwa usahihi, hivyo kwa kutambua hilo wameona Kanisa la SDA Mtaa wa Kinondoni linawajibu wa kuwafikia wagonjwa na kuzungumza nao ikiwa pamoja na kufanya maombi.

Amesema wanachokifanya hata Bwana Yesu amewahi kuyafanya na hivyo wao wameona ni vema wakahusika katika kusaidia mahitaji ya watu na hasa wenye kusumbuliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za maradhi na kuongeza kuwa kwaya hiyo kwa nyakati tofauti imekuwa karibu na jamii kwa kufanya matendo yaliyo mema.

Wakati huo huo Mzee wa Kanisa hilo Emmanuel Mgonja amesema kuwa wanapokwenda kutimiza miaka 10 ifikapo Oktoba 13 mwaka huu ambapo wameona ni vema wakashiriki kuwaona wagonjwa na kuwasaidia kwa kile kidogo walichonacho.

"Kabla ya kufanyika kwa uzinduzi wa DVD mbili siku hiyo ya Oktoba 13 mwaka huu tumeona ni vema tukaja hapa kwa ajili ya kuwasalimia wagonjwa hawa wa fistula, kushirikiana nao kwa kufanya maombi na kisha kutoa msaada huu ambao tumekuja nao,"amesema Mgonja.

Awali Muuguzi katika Hospitali ya CCBRT ambaye anahudumia wagonjwa wa Fistula Theodora Masako amesema kuwa ugonjwa huo unatibika lakini changamoto iliyopo wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa huo wamekuwa wagumu kufika hospitali kupata matibabu kwasababu mbalimbali ikiwemo kuhofia gharama za matibabu na wengine kuamini wamepata tatizo kwasababu ya imani za kishirikina.

"Tumekuwa tukitoa elimu kuhusu ugonjwa huu ambao hauna uhusiano na ushirikina, na wala matibabu yake hayana gharama yoyote ile na hapa kwetu tunatoa matibabu bila malipo.Hata hivyo tutumie nafasi hii kuishukuru kwaya hii ya Gethmane kwa kutambua umuhimu wa kutoa msaada wao kwa ajili ya wagonjwa hawa ambao tunawahudumia hapa hospitalini kwetu,"amesema Masako.

Amesema wagonjwa wanapoona wanatambelewa wanafarijika na kupata moyo kuwa wapo watu ambao wanawathamini na kuwajali kwani moja ya changamoto ya ugonjwa huo, wengi wao wamekuwa wakitengwa na jamii na wakati mwingine hata na familia zao.
 Mmoja ya wanakwaya ya Gethmane akikabidhi Zawadi kwa mgonjwa wa fistula katika Hospitali ya CCBRT leo baada ya kwaya hiyo kufika kwa ajili ya kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa hao
 Mmoja ya mlezi wa Kwaya ya Gethmane ya Kanisa ya SDA Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam akitoa msaada kwa mgonjwa wa Fistula katika Hospital ya CCBR leo jijini
 Muuguzi katika Hospitali ya CCBRT Theodora Masako akizungumza na wagonjwa wa fistula baada ya Kwaya ya Gethmane kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa msaada kwa wagonjwa hao ikiwa ni muendelezo wa matukio kuelekea Oktoba 13,mwaka huu ambapo watafanya uzinduzi wa DVD mbili katika Ukumbu wa Uhuru JKT Mwenge
 Baadhi ya wagonjwa wa fistula katika Hospitali ya CCBRT wakiwasikiliza viongozi na wana kwaya wa Gethmane ya Kanisa la SDA Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam
 Wanakwaya wa Gethman kutoka Kanisa la CDA Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam  wakiimba moja ya nyimbo zao wakati walipowatembelea wagonjwa wa Fistula waliopo Hospitali ya CCBRT .Kwaya hiyo pamoja na kuimba mbele ya wagonjwa hao wametoa msaada wa vitu mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 2.4
 Mchungaji wa Kanisa la SDA Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam Masunya Anthony akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya Kwaya ya kanisa hilo inayofahamika kwa jina la Gethmane kutembelea wodi ya wagonjwa fistula katika Hospitali ya CCBRT na kutoa msaada wenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 2.4.Wengine kwenye picha hiyo ni baadhi ya waimbaji wa kwaya hiyo ambayo inatarajia kuzindua albam zake mbili Oktoba 13 mwaka huu katika Ukumbu wa Uhuru JKT Mwenge

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...