Na Karama Kenyunko, globu ya jamii.

MAHAKAMA ya Rufaa imebariki maamuzi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoelekeza serikali kubadilisha kifungu cha 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa kuwa vinakiuka Katiba ya Tanzania.

Vifungu hivyo, vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 lakini mtoto wa kiume ameruhusiwa kuoa akiwa na miaka 18 hivyo, sheria haiweki usawa kati ya watoto hao na kwamba ni ya ubaguzi na ni kinyume na Ibara ya 13 na ya 12 ya katiba inayozungumzia usawa.

Hukumu hiyo imetokana na Serikali kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa mwaka 2016 ambao ulibatilisha kifungu cha Sheria ya Ndoa kinachoruhusu ndoa za utotoni.

Rufaa hiyo imesikilizwa na Jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija, Winfrida Korosso na Dk Mary Lavira ambapo miongoni mwa sababu za serikali za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu ni kwamba mahakama ilikosea kutoa uamuzi huo kwa sababu ililenga kuwasaidia kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ngono na kupata watoto nje ya ndoa.

Pia walidai mtoto wa kike anakua mapema kabla ya mtoto wa kiume.
Akisoma uamuzi uliotolewa na majaji hao, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Eddie Fussi amesema watoto wote ni sawa bila kujali jinsia na kwamba sheria hiyo haiwezi kumkinga mtoto wa kike kwa kumruhusu kuolewa kwa madai huko kuna ulinzi zaidi wakati kuna madhara makubwa kwake.

Amesema miongoni kwa madhara ambayo mtoto wa kike akiolewa chini ya umri wa miaka 18 ni mimba za utotoni, magonjwa na unyanyasaji wa kijinsia.Pia sheria mbalimbali zinakataza mtoto wa chini ya umri wa miaka 18 kuingia mkataba wowote hivyo ni pamoja na mkataba wa ndoa kwa sababu ni mgumu zaidi.

"Mahakama inaelekeza kifungu cha 13 na 17 vinakiuka katiba ya Tanzania hivyo, serikali ifuate maelekezo ya Mahakama Kuu ya kubadilisha vifungu hivyo," alisema Fussi.

Kesi hiyo ya kikatiba ilifunguliwa na Mwanaharakati wa Haki za Binadamu na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...