Mratibu wa Kitengo cha Kifua Kikuu na Ukoma kutoka hospitali ya wilaya
ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Dkt. Mkasange Kihongole amewatahadharisha
wananchi katika wilaya hiyo kuacha kunywa maziwa ya Ng’ombe holela
kutoka kwa wafugaji wanaoingia katika maeneo yao na kwamba Maziwa hayo
yanaweza kuwa na vimelea ambavyo ni chanzo kikubwa cha kuenea kwa
Ugonjwa wa Kifua kikuu kwa lugha ya kitaalamu ‘BOVINE TUBERCULOSIS’
Dkt Kihongole ametoa kauli hiyo jana ,wakati akiongea na wakazi wa
kijiji cha Semeni kata ya Mtina katika uzinduzi wa kampeni maalumu ya
uhamasishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa
wananchi wa kata hiyo,
Dkt. Kihongole alisema licha ya wilaya ya Tunduru kuwa na maambukizi
makubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu, hali hiyo inachangiwa pia na
unywaji holela wa maziwa ya Ng’ombe yasiyopimwa ambayo ni hatari zaidi
kwani usababisha kwa kiwango kikubwa kuenea kwa ugonjwa huo unaotajwa
kuwa ni kati ya magonjwa kumi yanayoongoza kuuwa Watu wengi Duniani.
Kwa mujibu wa Kihongole,siku za hivi karibuni kumekuwa na mwingiliano
mkubwa wa wafugaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo wanaoingia
kutoka mikoa mingine hapa Nchini, wakiwa na Ng’ombe ambao hawajapimwa
jambo linalo changia kuongezeka kwa maradhi ya kifua kikuu pale
wananchi wanapokunywa maziwa ya Ng’ombe wasiopatiwa tiba sahihi.
Alisema, ndiyo maana Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau
wengine ikiwemo Global Fund imeanza kuchukua hatau ya kutokomeza
Ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 na kusisitiza kuwa, ni muhimu jamii
kuchukua tahadhari kuhusiana na ugonjwa wa Kifua kikuu.
Kihongole alitaja makundi yaliyo katika hatari ya kupata maradhi hayo
ni Wazee kwani kadri Binadamu umri unavyokuwa mkubwa kinga za mwili
zinapungua,watoto walio chini ya umri wa miaka mitano,wasafiri,watu
walio katika msongamono kama vile wafungwa na wale wanaoishi kwenye
nyumba ambazo hazina hewa na mwanga wa kutosha kwani wadudu wa kifua
kikuu upendelea kuishi kwenye giza .
Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu ni hatari zaidi kuliko Ukimwi,kwa
sababu mgonjwa mmoja anaweza kuambikza watu kumi na tano kwa wakati
mmoja na Tb inayoogoza kuambukiza kwa haraka ni Tb ya mapafu ambayo
mtu anapata kupitia mfumo wa Hewa.
Kihongole alitaja dalili za mtu aliyeambukizwa Tb ni kukohoa kwa wiki
mbili au zaidi,kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku,kupungua
uzito,kupoteza hamu ya kula, na kwa watoto wadogo kuchelewa
kukua,kulia lia na kuwa na homa za mara kwa mara.
Dkt Kihongole,amewakumbusha wazazi na walezi kuwa na utaratibu wa
kupeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya
uchunguzi wa Afya zao mara kwa mara,badala ya kuamini mambo ya
kishirikina ambayo usababisha kupoteza maisha ya watu wengi hasa
watoto wadogo.
Kwa upande wake,Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru
Renatus amewataka watu wanaofanyiwa vipimo na kubainika kuwa na
vimelea vya ugonjwa wa Tb ni vema kuhakikisha wanamaliza
dozi(Dawa)wanazopewa na kuepuka kukatisha dawa kwani ni hatari sana
kwa Afya zao na watu wengine.
Aidha,ameitaka jamii kuwaibua watu wanaohisiwa kupata ugonjwa huo na
magonjwa mengine yanayoambukiza na kuwafikisha katika vituo vya
kutolea huduma ili kupata tiba itakayowasaidia kuwa na Afya njema na
uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Taifa.
Amewakumbusha akina mama pindi wanapoona dalili za ujauzito ni vema
kwenda kliniki haraka na wenza wao kupata ushauri wa wataalam na
kuhakikisha wanatumia zahanati na vituo vya Afya kujifungulia badala
ya kubaki nyumbani kwani ni hatari kwa afya zao na watoto wakati wa
kujifungua.
Hata hivyo,mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Hamza Malembo ameiomba
Serikali kupeleka Dawa na vifaa tiba vya kutosha ili kuwasaidia
kwani baadhi ya Zahanati hasa zile za maeneo ya pembezoni zina
upungufu mkubwa na wanapofika vituoni wanaelekezwa kwenda kununua
kwenye maduka ya watu binafsi,jambo linalowakatisha sana tamaa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...