Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.
Baadhi ya wananchi na wanufaika wa TASAF wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Hayupo pichani) katika ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF wa Kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa, Bi. Mariana Aidani Mkwaila akitoa shuhuda ya namna alivyonufaika na ruzuku anayoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Mnufaika wa TASAF wa Kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa, Bi. Elizabeth Damiani akitoa shuhuda ya namna alivyonufaika na ruzuku anayoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akiagana na mmoja wa wanufaika wa TASAF wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa mbele ya nyumba inayojengwa na mnufaika huyo kupitia ruzuku anayoipata.
Wananchi na wanufaika wa TASAF wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Hayupo pichani) uliofanyika katika kijiji hicho kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.

………………..


Na James K. Mwanamyoto-Nyasa

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeahidi kuzinufaisha kaya zote maskini nchini baada ya kuridhishwa na namna wananchi katika vijiji vilivyonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini walivyoboresha maisha yao na kujikwamua katika lindi la umaskini liliokuwa likiwakabili.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati akizungumza na wanufaika na wananchi wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango huo wilayani humo.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, iwapo wanufaika wasingetumia ruzuku vizuri kuboresha maisha, Serikali isingesita kusimamisha utekelezaji wa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

“Hongereni wanufaika wa TASAF kijiji cha Nangombo na maeneo mengine kwa kutumia ruzuku kuboresha maisha yenu, kujenga nyumba bora, kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi,” Mhe. Mkuchika amepongeza.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imeridhika na mafanikio yaliyopatikana, hivyo itaendeleza vita dhidi ya umaskini, lengo likiwa ni kuboresha maisha ya kaya zote maskini nchini.

Akiwasilisha taarifa ya kijiji cha Nangombo kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Joseph P. Ngogi amesema watoto 66 wa shule wananufaika na ruzuku inayotolewa hivyo imeongeza mahudhurio shuleni na kliniki kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, aidha kaya 65 zimeboresha makazi yao kwa kujenga ama kukarabati na kuezeka kwa bati.

Mmoja wa wanufaika wa Mpango wa TASAF kijiji cha Nangombo, Bi. Mariana Mkwaila amesema ruzuku anayoipata imemuwezesha kuwanunulia watoto wake sare za shule, viatu na madaftari ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba kubwa ambayo anatarajia kuizeka kwa bati hivi karibuni.

Naye, Bi. Elizabeth Damian amesema, alikuwa akiishi maisha ya kimaskini kwenye nyumba ya nyasi kabla ya kuingizwa kwenye Mpango, lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kufuga kuku, mbuzi na kufyatua tofali zilizomuwezesha kujenga nyumba iliyoezekwa kwa bati.

Mhe. Mkuchika amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...