Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutoanza kampeni kabla ya muda uliopangwa.

Mhe Jafo ameyasema hayo wakati akitangaza tarehe ya kuanza kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea watakaoshiriki uchaguzi huo ambapo fomu hizo zitaanza kutolewa kesho Oktoba 29 hadi Novemba 4, mwaka huu.

Amesema ni suala la kawaida kwa wagombea kusindikizwa na wafuasi na wapambe wao kwa mbwembwe lakini akasisitiza zisiwe kwa staili ya kufanya kampeni.

" Kanuni zetu hazisemi mtu aende kuchukua fomu peke yake, huwezi kumzuia mtu kwenda kuchukua fomu kwa staili anayoitaka lakini staili hiyo isiwe ya kampeni, wagombea wanaweza kwenda na ndugu na jamaa zao lakini niwakumbushe wasifanye kampeni kwa kuwa muda bado haujatangazwa rasmi," Amesema Waziri Jafo.

Kuhusu hofu ya baadhi ya maeneo kutokua na watendaji watakaosimamia uchaguzi, Mhe Jafo amesema changamoto hiyo ishafanyiwa kazi kwa baadhi ya Maafisa Tarafa kuteuliwa lakini pia kama ulivyo utaratibu sehemu ambayo haina mtendaji yupo ambaye atakaimu.

" Kwa mujibu wa kanuni zetu suala la uchukuaji fomu litaanza kesho Oktoba 29 na litakoma Novemba 4, hiki ni kipindi muhimu sana kwa wagombea kwani zoezi hilo litadumu kwa siku Saba.

Lakini pia nimetoa ufafanuzi na muongozo kuwa siku ya kuchukua fomu siyo hiyo Oktoba 29 tu Bali mgombea anaweza kuchukua fomu hata tarehe 30 kikubwa ni asipitishe Novemba 4 awe ameirudisha," Amesisitiza Waziri Jafo.

Amesema anaamini kuwa watanzania wote wenye sifa za kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi huu watajitokeza kuchukua fomu kwani huu ndio muda wa kuweza kufanya hivyo kupitia vyama vya vya Siasa vyenye usajili wa kudumu.

Amewataka wagombea na viongozi wao wa vyama kuzingatia kanuni na taratibu za uchaguzi hasa katika suala la kuchukua na kurudisha fomu ili kusije kuleta mkanganyiko hapo baadae.

" Nichukue fursa hii kuwashukuru sana Watanzania toka tumeanza zoezi la kujiandikisha hadi sasa tunavyoenda kwenye hatua ya kuchukua fomu wameendelea kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwenye kila hatua. Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye haki ya msingi ya kushiriki uchaguzi huu anashiriki bila kuwepo kwa malalamiko yoyote," Amesema Jafo.

Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ndio Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi huo ambao itafanyika Novemba 24 mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akitangaza tarehe ya kuanza kuchukua fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu. Fomu hizo zitaanza kutolewa kuanzia kesho Oktoba 29 hadi Novemba 4 mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...