Na.Joseph Lyimo

WADAU na wanachama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) wametakiwa kuwa makini, watulivu, na wavumilivu wakati huu kukiwa na mgogoro wa kiusajili na kikatiba wa taasisi hiyo. 

Mwenyekiti wa MVIWATA Mkoani wa Arusha, John Safari ameyasema hayo wakati akisoma taarifa ya MVIWATA ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro na bodi ya wadhamini juu ya mgogoro huo. 

Safari alisema Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania ni shirika la wanachama lililoanzisha mwaka 1993 na wakulima wakiwezeshwa na Chuo Kikuu cha Sokione ili kutetea maslahi ya wakulima wadogo na waweze kunufaika na shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na mtandao wao. 

Alisema MVIWATA ilisajiliwa mwaka 1995 chini ya sheria ya vyama (Society Ordinance Act) kwa usajili namba SO 8612 na Mwaka 2000 ilisajiliwa Bodi ya Wadhamini ili kukidhi matakwa ya kisheria. Mwaka 2007 MVIWATA ilipata cheti cha ukubalifu (Certificate of compliance) chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiseriali na kusajiliwa kwa namba 1930.

Alisema MVIWATA ilipitisha azimio na kuliweka kwenye katiba linalotaka kuundwa kwa mitandao ya kati na kuisajili katika ngazi mikoa na wilaya lengo kubwa lilikuwa ni kuimarisha nguvu ya MVIWATA, kusogeza madaraka kwa wanachama, kuimarisha ushirikishwaji na kuboresha huduma kwa wanachama. 

“Katika mikoa ambayo usajili umefanyika, mafanikio yamejionesha wazi, mwaka 2016, serikali kupitia wizara husika ilifanya uhakiki wa asasi za kiraia na kushauri mitandao ya MVIWATA kusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kama Chama cha Kijamii,” alisema Safari.

Alisema sababu kubwa kwa nini MVIWATA isajiliwe kama Chama cha Kijamii ni kuwa, MVIWATA ni chombo kinachoundwa na wanachama na hao hao wanachama ndiyo wanufaikaji wa shughuli na huduma za MVIWATA. Hii ndio tofauti inayoifanya MVIWATA isifae kusajiliwa kama Shirika lisilo la Kiserikali (NGO).

“Kwa mujibu wa sheria ya mashirika yasiyo ya Kiserikali, Na. 24/2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho na marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Na. 3/2019 na kwa kuwa malengo ya MVIWATA ni kuwanufaisha wanachama wake, tumeshauriwa tena na wataalam katika ofisi za usajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kusajili MVIWATA chini ya Sheria ya Vyama vya Kijamii (Societies Act) Sura 337 ya Sheria za Tanzania,” alisema Safari.

Alisema pamoja na ushauri makini uliotolewa na wataalam wa wizara husika, suala hilo bado limeleta mivutano baina ya MVIWATA Taifa (Bodi ya Wakurugenzi), Mitandao ya Kati iliyosajiliwa na wanachama. Mivutano hii imesababisha Halmashauri ya MVIWATA kuunda Kamati kwa lengo ya kuangalia mivutano hii na changamoto zake na kutoa ushauri wa nini kifanyike.

“Jambo la kusikitisha ni kwamba, baada ya Kamati kufanya kazi yake, mambo yafuatayo yamejitokeza na yanaendelea kujitokeza:
Muda wa kamati kufanya kazi (siku 7) ulishapita na kamati haijapewa nafasi haijawasilisha taarifa kwa Halmashauri ya MVIWATA, hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu ucheleweshwaji huu,” alisema Safari. 

Alisema kikao cha Halmashauri ya MVIWATA hakijaitwa kupokea taarifa ya Kamati. Pia, hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu sababu za kutofanya hivyo.
Kutofanyika kwa Mkutano Mkuu wa MVIWATA ambao awali ulipangwa kufanyika tarehe 9 – 11 Oktoba 2019. 

Alisema hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya kuahirishwa kwa mkutano huu na sababu za kuahirisha.Badaya yake, sasa inafanyika mikutano ya upotoshaji katika mikoa mbalimbali inayofanywa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na Watumishi kwa lengo la kupotosha ukweli kuhusu usajili unaopaswa kwa MVIWATA na kujenga mgawanyiko kati ya mitandao iliyosajiliwa na ambayo haijasajiliwa.

Kuendelea kusambazwa kwa taarifa za uongo kwamba mitandao ya kati iliyosajiliwa ina nia ya kujitenga na MVIWATA (mtandao wa kitaifa) jambo amblo si kweli Kuendelea kushinika mabadiliko ambayo hayatokani na wanachama na yaliyo kinyume na dhana na makusudi ya kuanzishwa kwa mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania.

Kuleta mgawanyiko na kutengeneza matabaka ndani ya mtandao kitu kinachoondoa umoja ambalo ni kusudui la msingi kwa ajili ya kujenga taasisi yenye nguvu yenye sauti ya pamoja Kuonekana dhahiri kwa dhamira ya kufuta mitandao ya kati ya MVIWATA kunakojionesha katika mapendekezi ya Bodi ya Wakurugenzi yaliyowasilishwa kwa Halmashauri.

“Jambo hili linaongeza mashaka kwamba kuna baadhi ya watu wachache wanataka kumiliki mtandao badala ya wanachama wenyewe na kutokana na changamoto hii na kile kinachoendelea sasa, tunapenda wanachama wa MVIWATA kote nchini, wadau wetu na umma uelewe kwamba:
MVIWATA ni moja na itaendelea kuwa moja katika muundo wake wa kimtandao unaoanzia kwenye vikundi, Mitandao ya Msingi, Mtandao ya Kati na Mtandao wa Taifa,” alisema. 

Alisema ieleweke wazi kuwa, muundo huu haufanyi na haujawahi kufanya uwepo wa MVIWATA nyingi bali umewezesha ukuaji wa MVIWATA na kuimarisha sauti ya pamoja.

Alisema wanachama na Mitandao ya Kati ya MVIWATA imekusudia kufanya usajili wa MVIWATA kama chama cha Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kubakiza madaraka kwa wanachama ambao ni wakulima wadogo.

Alisema wanachama wasikubali upotoshaji unaofanyika sasa katika mikutano inayoendelea maeneo mbalimbali na kwamba wanachama wanapaswa kuhoji uhalali wa mikutano hiyo inayofanyika sasa na kuuliza kwa nini haikuwa inafanyika huko nyuma. 

Alisema ni vyema ikaeleweka wazi kwamba, mikutano inayoendelea sasa kupotosha ukweli kuhusu wapi MVIWATA ijisajili ni matumizi mabaya ya fedha ambazo zingefaa kufanya shughuli za utetezi wa maslahi ya wakulima. 

Alisema kama bodi ina nia ya dhati ya kufanya maboresho, inapaswa kuruhusu mjadala mpana wa wanachama unaowapa fursa ya kusikiliza mawazo na hoja za pande zote ili wanachama wafanye uamuzi sahihi wenye taarifa za kutosha.

Alisema waelewe wazi kwamba Mitandao ya Kati iliyosajiliwa, haina nia wala kusudi la kujitenga, kujiondoa ama kukiuka katiba ya MVIWATA, badala yake inasimama kidete kutetea maslahi ya wanachama na azma ya kuundwa kwa mtandao.

“Ieleweke pia kwamba, Mtandao huu ni wa wanachama, unaomilikiwa na wanachama na kuongozwa na wanachama wenyewe na sio watumishi wake, na kitendo chochote cha kuruhusu baadhi ya watumishi kuchukua madaraka ya uongozi wa mtandao, kunaleta hatari ya ustawi na lengo la mtandao, hatukubaliani na mabadiliko ya mfumo na muundo wa shirika ikiwa ni pamoja na kuondoa usajili wa ngazi za kati,” alisema.

“Hatukubaliani na muundo wa mabaraza na mikutano ya wanachama ambayo inaondoa nia ya uanzishwaji wa mtandao na kupora madaraka ya wanachama, hatuna imani na Bodi ya Wakurugenzi kwa kuleta mabadiliko yanayopora madaraka ya wanachama, kubadili dhana ya mtandao na kutaka kuondoa mtandao kwenye makusudi ya kuundwa kwake,” alisema. 

Alisema kutokana na maelezo hayo hapo juu, wao viongozi na wanachama wa Mitandao ya Kati iliyosajiliwa, wanaomba wasajili katika wizara husika kuchukua hatua za haraka kutatua mgogoro huo na wanawaomba wanachama na wadau wao kuwa makini, watulivu na wavumilivu wakati mgogoro huu unapotatuliwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...