WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi
Kigwangalla anatarajiwa kuongoza maelfu ya washiriki wa mbio za Rock City
Marathon zinazoratarajiwa kufanyika Oktoba 20, mwaka huu kwenye viunga vya
Jengo la Biashara la Rock City Mall, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa mapema hii leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya mbio hizo, Bw Clement Mshana, ushiriki wa Waziri Kigwangalla
unaenda sambamba na ushiriki wa viongozi wengine waandamizi wa serikali kutoka
mikoa ya Kanda ya Ziwa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella ambaye
tayari amethibitisha kushiriki katika mbio za KM 42.
“Uwepo wa Waziri mwenye
dhamana na masuala ya utalii kwenye mbio hizi unatokana na yeye kuunga mkono
agenda iliyobebwa na mbio hizi ambayo mbali na kukuza vipaji vya mchezo huo ni
kutangaza utalii hususani katika ukanda
wa Ziwa kupitia mchezo wa riadha,’’Alisema
Mbio hizo
zilizoanzishwa miaka kumi iliyopita zinatarajiwa kupambwa na burudani
mbalimbali zikiwemo ngoma za asili na maonesho ya waadau mbalimbali wa utalii ikiwemo Wizara ya
Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) sambamba na wadhamini wa mbio hizo ambao ni pamoja
na kampuni za TIPER na Pepsi.
Wadhamini wengine ni
pamoja na, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Taasisi ya Taifa ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), CF Hospital, Metro FM, Mwanza Water, Pigeon Hotel, The Cask and
Grill, SDN na Kampuni ya Ulinzi ya Garda World.
“Ukanda wa Ziwa una vivutio vingi ambavyo
lazima vitangazwe kimataifa kwa nguvu kubwa zaidi na mbio hizi zimekuwa kama
chachu ya kufanikisha agenda hiyo hususani kwa mwaka huu ambapo zinatarajiwa
kuhusisha wadau wengi zaidi wa masuala ya utalii ambao pamoja na mambo mengine
watapata fursa ya kuonesha bidhaa na huduma zao kwenye viunga vya mbio hizo’’
alibainisha.
Aidha, zikiwa zimesalia
siku chache tu kabla ya kufanyika kwa mbio hizo tayari wadau mbalimbali
wanaotarajia kushiriki wameonesha kufurahishwa na zawadi zitakazotolewa kwa
washindi na washiriki zikiwemo medali na fedha taslimu zaidi ya Sh Mil 30.
“Pamoja na medali
washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake
watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, sh.mil 2/- kwa
washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu, huku washindi wanne hadi
kumi na tano nao pia wakiibuka na zawadi za medali na pesa taslimu.’’
“Kwa upande wa mbio za
Kilomita 21, pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake
watajinyakulia sh. Mil 2/- kila mmoja, sh. Mil 1/-kwa washindi wa
pili na sh. Laki 7/- kwa washindi wa tatu huku pia washindi wanne hadi wa kumi
na tano wakiibuka na zawadi za pesa taslimu na medali kila mmoja.’’
alitaja
Kuhusu mbio za kilomita
tano ambazo zitahusisha washiriki kutoka mashirika na taasisi mbalimbali
(corporates), Bw Mshana alisema inatarajiwa kuwa zitaongozwa na Mkuu wa Wilaya
ya Nyamagana Dk Philis Nyimbi sambamba na washiriki wenye ualbino ambapo zawadi
za fedha taslimu zitatolewa kwa washindi watatu wenye ualbino pekee.
“Kwa washindi wa mbio
za kilomita 2.5 zitakazohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi 10 washindi
watapatiwa fedha taslimu.’’ Alibainisha.
Akizungumzia usajili wa
mbio hizo Bw. Mshana alitoa wito kwa washiriki kuendelea kujisajili kupitia
vituo na mawakala wa mbio hizo katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma,
Pwani na Arusha
‘’Kwa sasa usajili wa
mbio hizo unaendelea kupitia vituo mbalimbali katika mikoa ya Mwanza (Rock City
Mall, Pasiansi Afro Twist Gym), Dodoma (Shabiby Bus Terminal), Dar es Salaam
(Shamo Tower, Imalaseko Super Market (Posta), Heleana Fashion – Dar Free
Market), Arusha pamoja na Bagamoyo mkoani Pwani.’’
“Pia usajili unaweza kufanyika kwa njia
ya mtandao kupitia website yetu ya Rock
City Marathon ambayo ni www.rockcitymarathon.co.tz.
’’ alitaja
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...