Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola Akizungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Matai, Wilayani Kalambo, Mkoa wa Rukwa, jana. Lugola ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo, kuwasaka na kuwatia mbaroni wabakaji wanne waliokimbilia nchini Zambia.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimuhoji Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa, Deokresi Mkandala, kuhusu watuhumiwa wanne wa ubakaji waliokimbilia nchi jirani ya Zambia. Lugola alitoa siku saba kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo, kuwasaka na kuwatia mbaroni watuhumiwa hao.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola Akizungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Matai, Wilayani Kalambo, Mkoa wa Rukwa, jana. Lugola ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo, kuwasaka na kuwatia mbaroni wabakaji wanne waliokimbilia nchini Zambia. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

…………………….

Na Felix Mwagara, MOHA, Rukwa.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa, kuwasaka na kuwatia mbaroni wabakaji wanne waliokimbilia nchini Zambia.

Lugola alisema wabakaji hao lazima wakamatwe na waletwe nchini kwasababu Jeshi hilo lina mbinu zote za kuwasaka wahalifu hao wanaodaiwa kukimbia kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa baada ya kubainika kufanya uhalifu huo Wilayani Kalambo.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mji wa Matai wilayani Kalambo Mkoani humo, Lugola alisema Wilaya hiyo inakabiliwa na matukio mengi ya ubakaji ambapo mpaka sasa Polisi tayari imewatia mbaroni wabakaji 11 na bado hao wanne wanaendelee kutafutwa ili wakamatwe.

Lugola alisema kero alizopewa na wananchi hao katika mkutano wa hadhara zikiwemo ubakaji kuwa juu pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi kuachishwa masomo kwa ajili ya kufanyishwa kazi wakiwa na umri mdogo, pamoja na wanafunzi kubakwa na kupewa mimba.

“Haiwezekani wahalifu waichezee Serikali ya Rais Dkt. Magufuli, lazima wakamatwe, wasakwe kwa nguvu zote, na mnipe taarifa mtakapowatia mbaroni watuhumiwa hao,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa, wahalifu mbalimbali wakiwemo majambazi, kutokana na uimara wa Jeshi la Polisi wamesambaratishwa na wanaendelea kusakwa katika kona zote nchini mpaka jambazi wa mwisho atakapotiwa mbaroni.

Aidha, Lugola aliwataka wananchi kutoa taarifa kwake na kwa viongozi wa Polisi wa Wilaya na Mkoa endapo kuna mwananchi atabambikiziwa kesi au kuombwa rushwa wakati anamuombea dhamana ndugu yake.

Lugola alikiri kuwepo kwa baadhi ya polisi wanaoendelea kuwaomba rushwa wananchi ili wapate dhamana pamoja na kubambikiwa kesi.

“Ndugu wananchi, hili nilishaliagiza na pia naendelea kuliagiza, ni marufuku kwa askari polisi yeyote atakaye muomba rushwa mwananchi ili ndugu yake apewe dhamana, dhamana ni haki ya mwananchi, na uikiingia polisi bure na kutoka ni bure,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alisisitiza kuwa, dhamana zitolewe saa 24 nchini bila wananchi kuombwa rushwa ya aina yoyote, na kuonya kuwa askari atakayepuuza agizo hilo, ataondolewa ndani ya Jeshi la Polisi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kalambo, Deokresi Mkandala alipokea maagizo ya Waziri Lugola likiwemo la kuwasaka wahalifu hao waliokimbilia nchini Zambia na kuahidi kuyafanyia kazi.

Waziri Lugola anaendelea na ziara yake Mkoani Rukwa kutatua kero mbalimbali za wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika Wilaya zote mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...