Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai akiongea na viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (hawapo pichani) walipotembelea ofisini kwake Wilayani Kongwa Novemba 19, 2019. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa , Deogratius Ndejembi.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa , Deogratius Ndejembi akiongea na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilayani humo pamoja na viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora waliotembelea ofisini kwake Novemba 19, 2019.
Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiagana na Viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kongwa ambayo inaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Deogratius Ndejembi (wa kwanza kulia anayewatazama)
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akimtambulisha mmoja wa wananchi wanaishi Wilayani Kongwa aliyejitokeza katika ofisi hizo kuwasalimia viongozi wa tume.

******************************

Na Mbaraka Kambona,

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai ameihakikishia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuwa itaipatia kila aina ya ushirikiano itakayohitaji kutoka kwa taasisi ya Bunge.

Ndugai alieleza hayo mapema leo (Novemba, 19, 2019) alipokutana na Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu aliyemtembelea katika ofisi yake ya jimbo iliyopo Wilayani Kongwa jijini Dodoma.

Akiongea katika kikao hicho, Ndugai alimueleza Mwenyekiti kuwa tume ni taasisi muhimu katika kusimamia na kuhamasisha masuala ya haki za binadamu nchini.

“Tume ni taasisi muhimu ambayo imepewa dhamana ya kusimamia haki za binadamu nchini, nawapongeza kwa kazi nzuri mnazozifanya japo mnachangamoto nyingi katika kutekeleza kazi zenu”, alisema Ndugai.

Ndugai aliendelea kueleza kuwa anatambua eneo ambalo tume inalifanyia kazi ni gumu kwa kuwa linahusiana na masuala ya usimamizi wa haki za watu, na kuwataka changamoto hizo zisiwakatishe tamaa,pale watakapokuwa na jambo lolote wasisite kuwasiliana na ofisi ya Bunge ili kushirikiana kuzitatua.

“Najua katika utekelezaji wa majukumu yenu mtakutana na changamoto nyingi hususani migogoro ya ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji naamini mtaisaidia serikali katika kuipunguza kama sio kuimaliza kabisa”aliongeza Ndugai.

“Naamini mtaenda kushughulikia pia migogoro ya wafugaji wanaokaa karibu na maeneo ya hifadhi, haiwezekani na haiingii akilini mifugo ikiingia katika hifadhi adhabu yake ni kunyang’anya mifugo yote ya mwananchi, nadhani hii sio sawa wala sio haki, nendeni mkayashughulikie haya”alisisitiza.

Aidha, Ndugai alimueleza Mwenyekiti wa tume kuwa wasisite kupeleka mapendekezo yoyote pale watakapoona kuna sheria ambazo wataona ni kandamizi waziwasilishe na kushirikiana na Bunge katika kuzirekebisha.

Naye Mwenyekiti wa tume , Jaji Mwaimu alimueleza Spika Ndugai kuwa dhamana waliyopewa na Mheshimiwa Rais John Magufuli ni kubwa na hivyo wanaahidi kuitendea haki kwa kufanya kazi kwa bidii ili kusaidia kutimiza ndoto ya nchi ya kufikia uchumi wa kati.

“Sisi kama viongozi wa tume, tunaunga mkono jitihada za serikali katika kukomboa wananchi kiuchumi, tunachokiomba kutoka kwenu na wadau ni ushirikiano kwani tukishirikiana kwa pamoja tutaweza kufanikisha jitihada hizo” alisema Jaji Mwaimu.

Mwenyekiti huyo wa Tume alikwenda kumtembelea Mheshimiwa Ndugai katika ofisi zake za jimbo Wilayani Kongwa jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha ikiwa ndio mara yake ya kwanza tangu alipoapishwa Novemba 4, 2019.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti aliongozana na Makamu Mwenyekiti, Mohamed Khamis Hamad, na Makamishna wengine watano ambao ni Mheshimiwa, Dkt. Fatma Rashid Khalfan, Mheshimiwa Thomas Masanja, Mheshimiwa Amina Talib Ali na Mheshimiwa Nyanda Josiah Shuli.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...