Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma

Serikali imesema kuwa Idhaa ya External Service iliyokuwa inarushwa na Radio Tanzania Dar es Salaam ilianzishwa mahususi wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na michezo Juliana Shonza alipokuwa akijibu swali Na. 38 na Mbunge Taska Restituta Mbogo (Viti Maalum) alilotaka kujua ni kwa nini TBC ilifuta kipindi cha External Service kilichokuwa kikitangaza taarifa ya habari kwa Lugha ya Kiingereza na kwa kutangaza taarifa ya habari kwa Kiswahili tu tunawanyima wageni fursa ya kujua kinachoendelea nchini.

Miongoni mwa mataifa yaliyonufaika na Idhaa ya External Service ya Radio Tanzania Dar es Salaam ni nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika ya Kusini.

Naibu Waziri Shonza amesema kuwa viongozi wa wapigania uhuru katika nchi hizo waliishi na kuratibu harakati za ukombozi katika nchi zao kutokea Tanzania ambapo walirusha matangazo ya Radio ya kuhamasisha wananchi wao kushiriki katika mapambano hayo kupitia idhaa hiyo ya External Service na haikuendelea kurusha matangazo yake baada ya nchi hizo kupata uhuru.

“Ni kweli kwamba kwa kutangaza taarifa ya habari kwa lugha moja ya Kiswahili kunawanyima wageni fursa ya kujua masuala mbalimbali yanayoendelea hapa nchini.

Lakini yapo magazeti mbalimbali yanayochapisha habari hizo hizo zinazotokea nchini kwa lugha ya Kiingereza ambapo inawarahisishia kupata habari hizo kupitia magazeti ya Daily News, The Guardian pamoja na The Citizen.”

Aidha, Naibu Waziri Shonza aliongeza kuwa kwa sasa TBC kupitia stesheni ya TBC International inayopatikana katika masafa ya 95.3, hutangaza kwa lugha ya Kiingereza hatua inayowafanya wageni kuendelea kupata habari na taarifa za mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.

Zaidi ya hayo, Naibu Waziri Shonza alisisitiza kuwa TBC1 na TBC Taifa zinarusha baadhi ya vipindi kwa Kiingereza ikiwemo vipindi vya “This Week in Perspective” na “International Sphere” na TBC Taifa ina vipindi “Breakfast Express”, “Daily Edition”, “Day Time” na Overdrive kwa Kiingereza ambapo vipindi hivi huzungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi pamoja na kijamii.

Akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Wabunge Kakoso Selemani (Mpanda Vijijini), Deogratias Ngalawa (Ludewa) na Sikudhani Chikambo (Viti Maalum) kuhusu usikivu wa TBC, Naibu Waziri Shonza amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kupanua usikivu maeneo yote nchini ambapo usikivu umeongezeka kutoka wilaya 87 mwaka 2017 sawa na asilimia 54 ambapo hadi Machi 2019 wilaya 102 zimefikiwa na matangazo ya radio ambayo ni sawa na asilimia 63.

Maeneo ambayo Serikali imefanyia marekebisho ni pamoja na ujenzi wa vituo vitano katika wilaya za mpakani za Rombo, Tarime, Kibondo, Kakonko, Namanga, Nyasa hadi Mbambabay umekamilika ambapo wilaya za Ruangwa, Lushoto na Mtwara ambazo usikivu wake ulikua hafifu umeimarika na mkakati wa Serikali ni kujenga mitambo ya Redio katika mikoa ya Katavi, Simiyu, Unguja, Pemba, Njombe, Songwe na Lindi.

Kuhusu makakati wa kukuza Kiswahili kama moja ya lugha nne rasmi za nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Naibu Waziri Shonza amesema kuwa Baraza la Kiswahili la Taifa kupitia mkakati wake wa miaka mitano 2015/2016 hadi 2019/2020 limejizatiti kutumia fursa hiyo likilenga kuimarisha fani ya tafsiri na ukalimani kutoka na kwenda Kiswahili pamoja na kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo na matumizi ya Kiswahili Afrika ya Mashariki, Afrika na duniani kote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...