Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii

GAVANA wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) Profesa Florens Luoga amesema kuwa kutokana na juhudi mbalimbali za kuboresha sekta ya fedha, imeshuhudiwa kuwepo kwa mafanikio makubwa Sekta hiyo na imekua kwa wastani wa asilimia 3.1 ikichangia katika ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia 2.6 katika kipindi cha miaka mitano inayoishia 2018. 

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 19 wa mwaka 2019 wa Taasisi za fedha nchini, Profesa Luoga amesema taasisi hizo zimeendelea kusambaa sehemu mbalimbali nchini na mpaka sasa kuna benki za biashara na taasisi za fedha 61 zenye matawi 838 nchini.

Pia amesema , Benki Kuu imekuwa ikisisitiza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi, na hadi hivi sasa kuna jumla ya mawakala 22,481 wa mabenki ambao wanatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi, na kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na taasisi za fedha. 

Profesa Luoga amesema utoaji wa huduma za fedha kwa wananchi na watoa huduma umeongezeka ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa njia mbadala za utoaji huduma za fedha kieletroniki na kupitia simu za mikononi, hivyo kwa sasa wananchi wanapata huduma za fedha karibu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani.

Amesema kumekuwa na ongezeko la wananchi wanaotumia huduma rasmi za kifedha ambapo matokeo ya utafiti wa FinScope ya mwaka 2017 yanaonesha kuwa idadi ya watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha ilifikia asilimia 65 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 45 ya mwaka 2009. Aidha, idadi ya Watanzania walio umbali usiozidi kilometa tano kutoka katika kituo cha huduma za kifedha imezidi kuongezeka na kufikia asilimia 86 kwa mwaka 2017.

Kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha, Profesa Luoga amesema kumekuwa na mafanikio makubwa. Mfumuko wa bei umekuwa mdogo kuliko kipindi kingine chochote tangu taifa letu lilipopata uhuru mwaka 1961. Wastani wa mfumuko wa bei katika kipindi cha miaka 4 ya uongozi wako, ulikuwa asilimia 4.7 ukilinganisha na wastani wa asilimia 8.9 kwa kipindi cha miaka 4 kabla ya hapo. Aidha, mfumuko huo wa bei umeendelea kushuka hadi kufikia asilimia 3.6 mwezi Oktoba 2019. 

Wakati katika utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kumekuwa na mafanikio na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi. Ukuaji wa mikopo kwa sekta hiyo ulifikia asilimia 9.3 mwezi Septemba 2019 baada ya kuchukuliwa hatua mbalimbali kufuatia ukuaji mdogo wa wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2018 na wastani wa asilimia 2.2 mwaka 2017, kulikotokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la mikopo chechefu. 

"Riba za mikopo zimeshuka katika kipindi cha hivi karibuni kufikia wastani wa asilimia 17 kutoka zaidi ya asilimia 18 kwa kipindi cha nyuma. Pamoja na jitihada zilizofanywa na Benki Kuu katika kuhakikisha kuwa benki na taasisi za fedha zinatoa mikopo nafuu na kwa wananchi wengi zaidi, bado kumekuwa na changamoto ya utambulisho na utambuzi wa wateja (unique identification and know-your customer).

" Hali hii inasababisha mabenki kuweka riba za juu kwenye utoaji wa mikopo na hivyo kutoa mikopo kwa wateja wachache. Tunatambua jitihada zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kutoa vitambulisho vya taifa na tunaamini kwamba kuongezeka kwa upatikanaji wa vitambulisho vya taifa kwa Watanzania wengi zaidi, hasa walioko vijijini kunaweza kuchangia kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu zaidi kwa wananchi na wazalishaji wengine."amesema Profesa Luoga

Amesema Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani bilioni 5.4 mwezi wa Oktoba 2019, kiasi ambacho kinatosheleza kuagiza bidhaa kutoka nje kwa zaidi ya miezi 6. na shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu mbalimbali duniani imeendelea kuwa tulivu.

Profesa Luoga amesema Sekta ya fedha imeendelea kuwa himilivu kama kwani taarifa zinaonyesha kuwa mabenki yana mitaji na ukwasi wa kutosha unaowiana na viwango vilivyowekwa kisheria. Uwiano wa mtaji wa msingi wa sekta ya kibenki ukilinganishwa na jumla ya rasilimali zilizopo ulikua kwa asilimia 16.6 Septemba 2019, ikilinganishwa na kiwango cha chini cha kisheria cha asilimia 10. Uwiano wa ukwasi ulikua kwa asilimia 31, ikilinganishwa na kima cha chini cha kisheria cha asilimia 20.

Amesema hali hiyo imechangia ongezeko la utoaji wa huduma za fedha nchini. Aidha, Benki Kuu imeendelea kusimamia sheria na taratibu katika kuimarisha utulivu wa sekta ya fedha. 

Pia amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya fedha, zipo changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hii. Kwanza, mabenki machache kushindwa kufikia matakwa ya kisheria ya uendeshaji, hivyo kuilazimu Benki Kuu kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzishauri benki hizo kuungana, kuongeza mtaji, na pale inapobidi kuzifunga. Changamoto nyingine ni ukuaji mdogo wa mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi, ambapo Benki Kuu ilichukua hatua mbalimbali na kuwezesha kukabiliana na hali hiyo na kuanza kuleta matokeo chanya kuanzia mwaka 2018.

Amesema Benki Kuu imechukua hatua kadhaa zilizosababishwa na kuongezeka kwa mikopo chechefu ambapo hatua ni Kuanzishwa kwa kanuni za utendaji za huduma za kibenki (code of conduct) ambazo zinatoa mwongozo na maadili yanayopaswa kufuatwa na mabenki na watoa huduma za fedha pamoja na wafanyakazi wao, ikiwa ni pamoja na mwongozo wa utoaji mikopo na benki zimeelekezwa kutumia Mfumo wa Kutunza Kumbukumbu za Wakopaji (Credit Reference System) ambapo taasisi za fedha zinatakiwa kupata taarifa za mkopaji kutoka katika mfumo huo kabla ya kutoa mkopo. 

Pia uanzishwaji wa Kanzidata ya Masijala ya Dhamana (Collateral Registry) umefikia hatua nzuri na utakapokamilika, taarifa za dhamana zote ambazo zimetumika kwenye mikopo zitahifadhiwa na kupatikana kwa wakopeshaji. Hii itaondoa uwekezekano wa matumizi ya dhamana moja kwa mkopo zaidi ya mmoja bila taarifa ,na uanzishwaji wa bima ya kilimo kwa ajili ya kulinda mikopo ya sekta ya kilimo na hivyo kuwa chachu ya kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wakulima. 

Amesema katika kuhakikisha malipo ya miamala ya fedha yanafanyika kwa urahisi, haraka, uwazi na kuongeza ufanisi kwa kupunguza gharama zinazohusiana na kufanya miamala, Benki Kuu ya Tanzania ilianza kuandaa mfumo mpya wa malipo ya papo kwa hapo Tanzania “Tanzania Instant Payment System” mwezi Februari 2019.

Profesa Luoga amesema mfumo huu utasaidia kuziunganisha benki na taasisi zingine zinazotoa huduma za fedha katika kufanya malipo mbalimbali ya fedha ya papo kwa hapo kwa gharama nafuu. Mfumo huu ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2020, utasaidia pia kufikisha huduma mbalimbali za malipo ya fedha kwa wakati muafaka.

Aidha, mfumo huu utasaidia kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika kufanya malipo kwa kuwa watoa huduma za fedha watakuwa tayari wameunganishwa eneo moja. Hivyo, mwananchi bado ataweza kutumia simu yake ya mkononi kupata huduma za benki bila tatizo hata kama hakuna tawi la benki lililo karibu.

"Kama nilivyoeleza awali, katika siku mbili za mkutano huu tutajadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta ya fedha nchini, hususan namna sekta ya fedha inavyoweza kuchangia kukuza uchumi wa viwanda na shughuli nyingine kwa maendeleo ya uchumi. Mkutano huu pia utatoa fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika matumizi ya teknolojia na jinsi inavyoweza kuendeleza sekta ya fedha. Tunashukuru kuwa tumepata watoa mada wenye weledi kutoka ndani na nje ya nchi ambao wapo tayari kutupatia uzoefu wao."amesema Luoga.

Pamoja na mambo mengine Profesa Luoga amesema Sekta ya fedha nchini imepitia mabadiliko mbalimbali ya kisera, kisheria na kimuundo. Mabadiliko hayo yalihusisha mabadiliko ya sera na sheria ambayo yaliruhusu soko huria katika sekta ya fedha. Vilevile, Serikali imekuwa ikifanya mapitio ya sekta ya fedha na kutoa miongozo mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa sekta hii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...