Na: Moshy Kiyungi, Tabora.


Jose Chameleone yaelezwa kuwa ndiye anayeongoza kwa utajiri miongoni mwa wanamuziki nchini Uganda, akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia shilingi bilioni 1.5 kwa fedha za Tanzania.

Aidha anamiliki mijengo ya bei mbaya ya kukodisha (Apartments),iitwayo Daniella Villas, jijini Kampala na studio yake iitwayo Leon Island.


Mwanamuziki huyo ametajwa na takwimu za kifedha kuwa ana utajiri wa zaidi ya dola za Marekani milioni 5.Katika orodha ya mali zake, pia anamiliki ufukwe uitwao Coco Beach, uliopo Barabara ya Entebbe nchini humo.

Jose Mayanja Chameleone, pia ana mikataba minono na kampuni zinazomtumia kutangaza bidhaa na huduma zake.Moja kati ya mikataba yake iliyowahi kumtajirisha ni ile ya MTN na simu za Android.

Jose Chameleone ambalo ni jina la kisanii, alipozaliwa mwaka 1976, wazazi wake walimpa jina la Joseph Mayanja, ambalo siyo geni miongoni mwa wapenzi na washabiki wa muziki wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Chameleone alianza muziki mwaka 1996, kipindi hicho akiwa ‘DJ’ katika ukumbi wa usiku wa Missouri uliopo Kampala.Moja kati ya nyimbo zake za kwanza ulikuwa wa "Bageya", aliomshirikisha msanii kutoka Kenya, Redsan.

Albamu yake ya kwanza ilitolewa nchini Kenya mwaka wa 1999. Tangu wakati huo aliachia albamu kadhaa zikiwa pamoja na "Bageya" ya mwaka wa 2000, "Mama Mia" ya mwaka wa 2001, "Njo Karibu" mwaka wa 2002, "The Golden Voice" ya mwaka wa 2003, "Mambo Bado" ya mwaka wa 2004 na "Kipepo" ya mwaka wa 2005.


Aidha alishirikiana kufana kazi mwanamuziki mwenzake Bebe Cool, lakini baadaye waliibuka kuwa na upinzani mbaya.Mtindo wa muziki anaocheza Chameleone ni mchanganyiko wa utamaduni wa Kiganda, rumba ya Kati ya Afrika, Zouk na ragga.

Jose Chameleone ni mwanachama wa Jamii ya Mwanamuziki, muungano wa wanamuziki ambao hutumia umaarufu na mali zao kusaidia kuondoa umaskini na kujenga kampeni za mwamko wa Virusi Vya Ukiwi VVU.

Amezitembelea nchi nyingi za ng'ambo kufanya maonesho zikiwemo Marekani, Uingereza, Sweden na nyingine nyingi.

Ikumbukwe kuwa wimbo wa Kipepeo ulikuwa haukauki vinywani mwa watu wazima pamwe na watoto wadogo, wakisikika wakitamka Kipepo, Kipepeo, wimbo ambao ulitungwa na kuimbwa na mwanamuziki huyo Jose Chameleon.

Aidha alifanya ‘kufuru’ baada ya kuachia vibao vya Jamila, Bei Kali, Mama Rhoda na nyingine nyingi vilivyo muongezea umaarufu zaidi.Ngoma zake zingine ambazo zimewahi kutikisa kwenye soko la muziki Barani Afrika ni ‘Wale Wale’, ‘Nkoleki’, ‘Vale Vale’, ‘Dorotia’, ‘Tubonge’, ‘Agatako’ na ‘Pam Pam’.


Mpaka mwaka 2013, tayari alikuwa na albamu 12.

Miongoni mwa matukio yaliyowahi kumpa umaarufu mkubwa ni kuvunja rekodi ya kuingiza mashabiki wengi kwenye Uwanja wa Kriketi wa Lugogo nchini Uganda.Katika onesho hilo lililopachikwa jina la ‘Tubonge Live’, takribani washabiki 40,000 walizama ndani kushuhudia.

Licha ya kufanya vizuri nchini mwake, kazi za Chameleon zimekuwa zikitesa nje ya mipaka ya nchi hiyo.Jose Mayanja kutokana na utajiri alionao, amekuwa akiishi maisha ya kifahari, ambapo mwenyewe alithibitisa kuwa muziki unalipa.

Kali zaidi ni pale aliponunua jozi mbili za viatu vya kisasa vilivyomgharimu kiasi cha zaidi ya milioni 40.Chameleone na familiya yake wanaishi kwenye jumba lao la kifahari lenye gharama za takriban shilingi milioni 17, nje kidogo ya jiji la Kampala.

Aidha anamiliki Coco Beach, iliyopo ufukweni mwa Ziwa Victoria, kukiwa na vivutio vya burudani vyenye thamani shilingi milioni 27.Jose pia anamiliki magari ya kifahari aina ya Cadillac Escalade, BMW, Premio, Toyota Ipsum, Landcruiser VX, Mercedes Benz yenye thamani shilingi milioni 270.

Chameleone amewekeza kwenye miradi mingine mikubwa inayomuongezea kipato ikiwa ni pamoja na kumiliki mjengo wa kupangisha ‘Apartment’ katika mji wa Arizona, nchini Marekani, jumba la kifahari katika vilima vya Sekuku jiji la Kampala na nyumba nzuri sana aliyoinunua kwa bei ‘ndefu’ mjini wa Kigali, Rwanda.

Jose Chameleone mwaka 2013, alitajwa kuwa mmoja kati ya wasanii sita matajiri Afrika.Awali wasanii Bebe Cool na Navio, walijitangaza kuwa ndiyo matajiri nchini Uganda. Chameleone baada kusikia habari hiyo ndipo alipoibuka na kuanza kuanika mali zake.

Jose alikerwa zaidi aliposikia watu wanasema kuwa aliongopa kutamka kuwa alimpa mkewe gari aina ya Range Rover katika sikukuu ya Wapendanao.“Haijalishi mimi kumnunulia Daniella Range Rover, lakini yeye ana lake na langu lipo. Watu wanapaswa kuamini kuwa mimi ni mwanamuziki tajiri na mwenye mali kibao,” alijigamba Chameleone.

Akifanya mahojiano na kituo kimoja cha redio, Chameleone alikanusha tetesi kuwa Range Rover walilodai ni lake, lilikuwa la promota wa muziki aitwaye Sipapa.

Jinsi mafanikio yake yalivyokuwa yakitiririka mithiri ya maji mtoni, nguli huyo aliwahi kutuhumiwa kwamba hutumia nguvu za giza katika kutengeneza utajiri aliona hatimaye kupandisha umaarufu wake.

Mahasimu wake walidai kuwa utajiri na umaarufu wake barani Afrika umetokana na ‘ndumba’.Aliyekuwa wa kwanza kumtuhumu Chameleone kutumia nguvu za giza ni mkali wa muziki wa raga, Badman Denzo.
Badman alisema Chameleone amekuwa ‘akinyunyiza’ ili kufanikisha malengo yake kimuziki.

Nyota huyo alidai kuwa Chameleone amekuwa akitembelea Tanzania mara kwa mara kwa lengo la kukutana na waganga wake.Badman aliyasema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha NBS.

Nyota huyo aliyewahi kutamba na kibao ‘Big Mouth By Far’ alimtaja Chameleon pale alipoambiwa amtaje msanii mmoja anayetumia nguvu za giza.“Nina uhakika Chameleone anatumia uchawi, huwa anapata mambo hayo kutoka Tanzania, niliwahi kumkuta Dar es Salaam”. alidai Denzo.

Chameleon aliposikia shutuma hizo, alikanusha vikali huku akisistiza kuwa ni jitihada zake binafsi ndiyo msingi wa mafanikio yake.Jose aliongeza kusema kwa waliomtaja kuwa ni mchawi, walilenga kumchafua na kulifuta jina lake kwenye soko la muziki.

Chameleon ambaye ni kaka wa mastaa wa muziki Uganda, Palaso na Weasel, alisema yeye ni muumini mzuri wa dini ya Kikiristo, si rafiki wa shetani na kuongeza kuwa uchawi hauna ‘dili’.

Jose Chameleone aliwahi kuwepo kwenye orodha ya Wanamuziki matajiri Afrika, akiwa ni mwimbaji pekee aliyeiwakilisha Uganda kwenye hiyo orodha hiyo.Sehemu ya utajiri wake unatoka kwenye biashara za nyumba na viwanja, pia mauzo ya simu za mkononi zenye jina lake na makampuni makubwa ya kibiashara.

Jose aliazimia kufanya onesho kubwa December 2014, ambalo kiingilioni kilikuwa shilingi milioni moja za Uganda. Katika onesho hilo gari lake jipya aina ya Range Rover ya mwaka 2013, lilonekana kwa mara ya kwanza.


Mwanamuziki huyo Jose Chameleone, alinunua jozi moja ya viatu kwa kulipa dola elfu 12 na nusu. Wakati huohuo wengine wakadai eti anajionyesha kuwa ‘anazo’.Lakini Chameleone alisema ameamua kuizawadi miguu yake!
Alifafanua kuwa anarudishia shukran miguu yake kwa kusimama naye na kumuwezesha kufika alipo sasa.

Mwimbaji huyo wa wimbo wa ''Wale wale, waliobarikiwa na mungu'', alisema siyo majivuno kamwe bali ni njia yake ya kumshukuru Mungu kwa kumjalia na kumpa uwezo kama huo.

Wimbo huo tayari umetazamwa na watu zaidi ya milioni moja laki tatu katika mtandao wa Youtube.

Alipokuwa ziarani nchini Kenya, aliwaacha watu vinywa wazi baada ya kuweka mtandaoni picha ya viatu vyake aina ya Nike Air Mag, ambavyo jozi hiyo alinunua kwa dola 12,500 za Kimarekani.

Ilifahamika kuwa Chameleone kanunua viatu kwa jozi moja kwa pesa sawa na milioni moja na laki tatu za Kenya au karibu milioni 26 za Tanzania.

Tambo za Chameleone zilipelekea baadhi ya mahasidi wake kumnanga eti nafuja pesa.

Lakini mwenyewe aliwapa ushauri kuwa ikiwa wao hawawezi kutoa dola elfu 12 mia tano kununua kiatu, basi waende kwa Wachina wanaouza viatu bei rahisi sana...wasimuonee sooo, wakanunue viatu saizi yao mali ya Wachina.

Mwenyewe alisema anajipa raha, ''jifurahishe ungali hai'', Chameleone alijigamba.Chameleone alikumbusha kuwa miaka zaidi ya minane iliyopita, angelikuwa Kiwete kutokana na ajali mbaya.“Sasa nimepona na pesa ziko kwanini nisiishukuru miguu yangu?

Ikumbukwe kwamba Jose Chameleone alijirusha kutoka ghorofa ya tatu katika hoteli ya Impala jijini Arusha, na kusababisha kuumia vibaya ikiwa ni pamoja na kuvunjika miguu yote.Walinzi wa hoteli hiyo walikimbilia eneo aliloangukia baada ya kusikia kishindo, wakamkuta akiwa hawezi kuinuka.

Hata hivyo haikueleweka mara moja sababu zilizomfanya mwanamuziki huyo kujirusha.Baada ya tukio hilo wenyeji wake ambao walikuwa ni Clouds FM redio, waliokuwa wamemualika kwa ajili ya shughuli ya Fiesta ya Tanga, walilazimika kufanya utaratibu wa kumpeleka hospitali.

Taarifa zilipomfikia baba yake huko Uganda, alikodi Ndege ambayo ilituwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro International Airport (KIA), kwa ajili ya kumbeba Jose Chameleon, akapelekwa kwao Uganda ambako alilazwa.

Kuumia kwa Chameleone kulisababisha ashindwe kufanya onesho katika tamasha hilo, ambako kulikuwa na Wasanii wengi wa Tanzania, yeye ndiye angelikuwa mgeni rasmi.Jose Chameleone amekuwa akitunga na kuimba nyimbo nyingi kwa lugha za Kiswahili, Luganda na Kiingereza.

Jose anaelezwa kuwa amebadilisha sura ya muziki nchini mwake Uganda, hususan kwa kufanya muziki wa asili kukubalika kwa sehemu nyingi ulimwenguni.

Baadhi ya mambo yanayothibitisha utajiri wa nyota huyo ni makadirio ya ujumla ya utajiri wake unaofikia Shilingi bilioni 1.5 kwa fedha za Tanzania.

Pamoja na utajiri huo, alisema bado anazisaka pesa, kwani bila ya kuwa na tamaa ya kusaka mafanikio zaidi, ndoto huenda zisitimie.

Mayanja alisisitiza kuwa, baada ya kumiliki nyumba, magari na akaunti iliyonona benki, sasa ana ndoto za kumiliki Chopa yake ‘Helikopta’.

Sababu ni kwamba amekuwa akikodi Chopa mara kadhaa kwenda katika matamasha au kama alivyofanya wakati alivyomuoa mkewe Daniela Atim.

Jose Chameleone anaweza kuonekana jeuri na mtata mbele ya mashabiki wake, lakini kuna kitu kimoja ambacho wengi wanaweza wasiwe wanafahamu.

Chameleone ni baba anayeipenda familia yake anayewajibika kuiweka katika mazingira mazuri kadri awezavyo.Chameleone ana mke na watato wanne. Mtoto wa kwanza ni wa kike anaitwa Ayla Mayanja Onsea, aliyempata wakati akiwa kwenye mahusiano na Dorotia.

Katika ndoa yake na Daniella, wamepata watoto watatu, Abba Marcas Mayanja akiwa wa kwanza kwenye ndoa yao, Alfa Mayanja na Alba Shyne Mayanja.

Kati ya watoto hao walinaswa na mitandao ya kijamii wakiendesha gari la kifahari katika jiji la Kampala licha ya umri wao kuwa mdogo.

Mwaka 2005 na 2006 Jose alitayarisha mlio wa mziki ambao ni utunzi wa msanii wa Tanzania,Mheshimiwa Mbunge Joseph Haule, maarufu kwa jina Professor J. Wimbo huo unaitwa “Nikusaidieje”.

Jose Chameleone akatumia ujanja kwa kuiba beat ile, akaitumia kwenye muziki wake wa Bombo Crat, ambayo ilifanya vyema nchini Uganda.

Baada ya mwenye mali Porofessor J. kugundua kuwa umeibwa, akawasiliana na Chameleone. Majibu ya aliyopewa ni kumuomba msamaha akaahidi kulipa dola za Kimarekani 2400.Machi 2017 watayarishaji filamu wa nchini Marekani, katika filamu moja wakaomba kutumia beat ya P-funk Majani ya ‘Nikusaidieje’. Lakini wakataka kwanza wawasiliane na mhusika wa wimbo huo. Sintofahamu zikajitokeza za nani aonwe kati ya Jose Chameleone wa Bombocrat, au Profesa J. wa ‘Nikusaidieje’.

Baada ya Chameleone kubaini kuna ‘dili’ hilo, alikwea Pipa kwenda Marekani, akakutana na wahusika, wakasaini mkataba wa maisha, kwamba atalipwa milele kutokana na mauzo ya filamu ile.

Jose alipewa kianzio cha malipo cha dola za Kimarekani 50,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 120 za Tanzania.

Jose Chameleone aliingia katika orodha ya wanamuziki walioibukia katika siasa baada ya kutangaza rasmi kuwa atawania kuwa Meya.
Mayanja alitangaza nia ya kushindana na Erias Lukwago kugombea kiti hicho cha Umeya wa jiji la Kampala.

Hivi karibuni Chameleone alijiunga na Harakati ya nguvu za watu “People Power Movement”. Kundi linaloongozwa na mwanamuziki mwenziye aliyeibukia katika siasa, Bobi Wine.Huyu ndiye Joseph Mayanja ‘Jose Chameleon’

Kila la heri katika harakati zako za muziki na siasa.Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0784331200, 0736331200 na 0767331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...