Ndugu Wanahabari, 

Kama mnavyofahamu Serikali ilipiga marufuku uingizaji, uzalishaji, usafirishaji, na matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini tangu tarehe 01 Juni, 2019. 

Chimbuko la katazo hili lilitokana na changamoto za kiafya na mazingira zitokanazo na mifuko ya plasitiki ambazo ni pamoja na: Kudumu katika mazingira 

kwa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 500 na hivyo kuleta athari za muda mrefu; Kusababisha vifo vya mifugo, wanyama na viumbe wa baharini wanapokula na kumeza mifuko ya plastiki; Kuchangia uchafuzi wa mazingira kutokana na kuzagaa ovyo katika mazingira; na Kuziba mitaro ya maji ya mvua, miundombinu ya maji na majitaka na kusababisha mafuriko na kuenea kwa magonjwa ikiwemo malaria na kipindupindu. 

Katika kuratibu katazo hili Ofisi ya Makamu wa Rais imeunda kikosi kazi chenye jumla ya wajumbe 32 kwa nia ya kufuatilia kwa kushirikiana na vyomo vingine vya Serikali, utekelezaji wa Sheria na changamoto za katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki. 

Kufuatia katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki, pamekuwepo na fursa mbalimbali za kuwekeza katika kuzalisha na kuingiza nchini mifuko mbadala wa plastiki ikiwemo mifuko ya karatasi, nguo, katani pamoja na mifuko ya non- woven. Wadau wengi wamejitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko husika. Kabla ya katazo, katika kipindi cha mwezi Januari-Mei, 2019 jumla ya tani 197.8 za mifuko ya non-woven ziliingizwa nchini .Aidha, katika kipindi cha mwezi Juni – Oktoba, 2019 jumla ya tani 757.1 za mifuko mbadala ziliingizwa nchini. 

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto mbalimbali zimejitokeza ikiwemo wimbi la uingizaji wa mifuko mbadala aina ya non-woven ambayo haikidhi mwongozo wa viwango vilivyowekwa na TBS na pia; matumizi ya vifungashio vya mifuko laini ya plastiki (plastic tubings) kama vibebeo vya bidhaa mbalimbali kama vile nyanya, karoti na njegere; na Uingizaji wa magazeti yaliyotumika kwa ajili ya kufungashia bidhaa katika maeneo ya masoko, maduka na maeneo mengine ya biashara. Hali hii ni makosa kisheria kuingiza nchini bidhaa ambazo hazikidhi matakwa ya kisheria pamoja na kubadili matumizi ya vifungashio kufanya vibebeo vya bidhaa. 

Mwongozo wa Viwango vya vya ubora wa mifuko ya non-woven umekwishatolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na umeainisha kuwa mifuko hii inapaswa kuwa na sifa zifuatazo: 
Uzito usiopungua GSM 70 (Gram per Square Metre) 
Iwe inaweza kurejelezwa (Recyclable) 
Ioneshe uwezo wa kubeba (Carrying capacity) 
Iwe na anuani ya mzalishaji au nembo ya biashara 
Iwe imethibishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) 

Hata hivyo kumekuwepo na waingizaji na wazalishaji wanaokaidi kwa makusudi matakwa ya viwango hivi hali ambayo inasababisha wazalishaji wa mifuko inayokidhi viwango kukosa soko na kukosesha Serikali mapato yatokanayo na uzalishaji wa bidhaa husika, kutishia ajira katika viwanda hivyo vya ndani, uharibifu wa mazingira na ukwepaji wa kodi utokanao na bidhaa kutotambulika na hivyo kuathiri mapato na uchumi wa nchi kwa ujumla. 

Katika jitihada za kudhibiti hali hii, shehena za mifuko mbadala isiyokidhi viwango vya ubora zimekamatwa katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, NEMC kwa kushirikiana na TBS wameendesha ukaguzi katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata mifuko ya Non-Woven isiyokidhi viwango zaidi ya pieces milioni 2 na rollers zaidi ya 200 kwa ajili ya kutengeneza non-woven. 

Mifuko hiyo imezuiliwa kuingia sokoni na hatua za kisheria zinaendelea. Vilevile, mifuko laini ya plastiki (plastic tubings) pieces 9,600 zimekamatwa Mwanza zikiwa kwenye magunia 8. Napongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka mbalimbali za Serikali ikiwemo NEMC, TBS na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti wimbi la uingizaji wa mifuko mbadala aina ya non- woven isiyokidhi viwango.

 Hata hivyo, nasisitiza ukaguzi uendelee kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini hususan kwa wazalishaji wa mifuko laini ya plastiki (plastic tubings), masokoni na maduka makubwa ili kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo. Vilevile, napenda kuwashukuru watanzania wote kwa kushiriki kikamilifu na kutoa taarifa katika kutekeleza katazo hili la Serikali. 

Agizo! Naelekeza NEMC, TBS pamoja na kikosi-kazi cha kitaifa washirikiane kwa karibu na Kamati za ulinzi na usalama za mikoa, wilaya na mitaa nchini kuendelea kufanya kazi bila kuonea mtu yeyote katika kudhibiti matumizi ya mifuko mbadala aina ya non-woven na kudhibiti uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya non-woven isiyokidhi vigezo vinavyokubalika kisheria. 

Aidha, viko viwanda vinavyozalisha kwa kificho mifuko laini ya plastic na kuingiza sokoni kwa magendo, ufuatiliaji ufanywe na kuwabaini wazalishaji hao na hatua zichukuliwe dhidi yao zikiwemo kuteketeza bidhaa hizo ili iwe fundisho kwa wengine. 

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE 

WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...