ILITANGAZWA siku za karibuni kuwa Tanzania imepanda toka nafasi ya 144 hadi ya 141 katika taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu ubora wa mazingira ya kufanya biashara. Hii inaifanya Tanzania kuwa nafasi ya nne katika eneo la Afrika ya Mashariki ukitazama nchi 190 duniani ambazo ripoti hiyo imeziainisha.

Zipo sababu mbalimbali ambazo zimechangia maendeleo haya kutoka katika sekta binafsi na juhudi za serikali katika kusaidia ukuaji wa sekta hiyo. Juhudi hizo zimesaidia si tu kukua kwa biashara lakini pia zimefanya mazingira ya kufanya biashara nchini kuwa na unafuu.

Tukichukulia kwa mfano sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi ambayo kwa muda mrefu imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi nchini. Unafahamu kwamba mpaka kufikia mwaka 2016 sekta hiyo imechangia karibu dola za Kimarekani bilioni 2.5 katika uchumi wa Tanzania? Hii ni sawa na shilingi za Kitanzania trilioni 5.75 au asilimia 5.2 ya pato la taifa.

Tafiti nyingi za kiuchumi zimeendelea kuweka bayana ushahidi wa wazi kuhusu umuhimu wa sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi na ni kwa sababu hii kama taifa hatuna budi kuendelea kuhakikisha kwamba sekta hii inalindwa na kusaidiwa kukua vizuri.

Wabobezi wa uchumi wanasema kuwa mojawapo ya njia za kuboresha sekta hii ni kuunganisha makampuni ambayo yako sokoni. Hivi sasa kuna kampuni sita za mawasiliano ya simu za mkononi nchini ikiwa yamepungua kutoka saba ya awali baada ya kampuni ya Smart kuondoka.

Namba hii japo imepungua moja lakini inaelezwa kuwa ni kubwa kwa aina ya soko lililopo nchini. Jambo hili lina athari hasi kwa maendeleo ya sekta hii na hata uwekezaji wenye tija ambao ungeweza kuboresha sana huduma.

Licha ya tatizo hilo, mwanga umeanza kuonekana. Kampuni ya Tigo Tanzania imeungana na kampuni ya Zantel. Hii inaonyesha makampuni yameanza kuelewa umuhimu wa kuungana na kuwekeza vyema zaidi kupanua huduma. Mbali na kuwa ni jambo la afya kwa sekta na uchumi lakini pia ni muhimu zaidi kwa wateja. Mapema mwaka huu wa 2019 Wakurugenzi wa Tigo na Zantel walipokuwa wakizungumza na jarida maarufu duniani la Forbes walikaririwa wakieleza ni kwa namna gani muungano wa kampuni hizo mbili utaboresha huduma na ubunifu katika soko na kuongeza wateja wengi zaidi.

Ama kwa hakika ni jambo jema kuona sekta ya mawasiliano inavyouinua uchumi wetu. Sekta ya mawasiliano yenye muungano wenye tija kama ule wa Tigo na Zantel itakuwa na mchango mkubwa zaidi kwa ukuaji wa uchumi wetu sambamba na kuwapa watumiaji wa simu za mkononi nchini kile kilicho bora.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...