Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, akionesha mabibo aliyoyaokota kwenye shamba la mfano la korosho lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo Kijiji cha Masigati, wilayani Manyoni wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua shamba hilo jana.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, akiweka mabibo hayo kwenye mfuko akisaidiwa na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Aderaide Rweikiza.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi na  Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Aderaide Rweikiza wakiokota  mabibo katika shamba hilo. 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, akiokota mabibo kwenye shamba hilo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi  amekagua shamba la mfano la korosho lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo Kijiji cha Masigati, wilayani Manyoni na kueleza kuwa  linaendelea vizuri.

Akizunguza na waandishi wa habari jana wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya kukagua shamba hilo Dkt. Nchimbi alisema linaendelea vizuri na kuwa linaleta matumaini makubwa.

"Hivi sasa mabibo yameanza kuanguka na watu wanayaokota ni dalili nzuri ya maendeleo ya shamba letu na kazi inayoendelea katika shamba hili ni kufanya usafi tayari kwa msimu huu" alisema Nchimbi.

Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa katika msimu huu wanatarajia kupanda ekari zote 12,000 kwani mbegu zipo tayari na zipo za kutosha.Akizungumza na wananchi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo waliokuwepo katika shamba hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida Oktoba 4, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza  Dkt. Nchimbi kwa kulibeba wazo la kuanzisha shamba hilo na kuhakikisha linatimia.

“Nimpongeze Mkuu wa Mkoa wa kulibeba jambo hili, lakini nikuombe wewe na viongozi wenzako mhamasishe wengine walime zaidi zao hili kwa sababu korosho ni zao kubwa duniani na tena zao hili lina bei nzuri kimataifa,” alisema.

Alisema anatambua kwamba timu ya wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele, Mtwara imeshawasili Manyoni ili kufanya utafiti za zao hilo na jinsi linavyoweza kuzaa mara mbili kwa mwaka.

“Kwa kawaida, mkorosho mmoja hutoa kilo 40 za korosho kwa msimu mmoja, kwa hiyo kwa misimu miwili mtapata kilo 80. Ninawasii limeni korosho kwa ajili ya watoto wenu ambao wako darasa la pili au la tatu. Mkulima ukianza kuvuna, utaendelea kuvuna kwa miaka 20 mfululizo na kwa hiyo hao watoto hawatahitaji kulipiwa ada wakiwa chuo kikuu sababu korosho itakuwa inawalipia,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakulima wanaolima zao hilo wilayani Manyoni, waunde Ushirika wao ambao utawasaidia kuagiza dawa kwa pamoja ama kuuza kwa pamoja.Hivyo, alimwagiza Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo,  Yusta Philipo ahakikishe anasimamia jambo hilo kuanzia sasa.
Akitoa taarifa juu ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Kanda ya Kati, Ray Mtangi alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa kilimo cha korosho unajumuisha mashamba makubwa mawili ambapo shamba la Misigati lina ukubwa wa ekari 7,000  na lile la Mikwese lenye ukubwa wa ekari 5,000.

Alisema watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifika shambani hapo ili  wajifunze mbinu mpya za kuzalisha korosho kwenye maeneo yao. “Wiki mbili zilizopita, Mheshimiwa Spika na madiwani wa Kongwa walipita hapa ili kujifunza zao hili,” alisema.Pia alisema Halmashuri yao imetenga eneo la ujenzi wa viwanda na kwamba hadi sasa wanazo ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.

Mapema, Waziri Mkuu alikagua shamba hilo na kujionea hali halisi ya shambani ikoje. Pia alioneshwa mabibo na korosho ambazo zimevunwa kutoka kwenye shamba hilo la mfano, kutoka  kwenye mashamba ya wakulima ambao walipanda miche tangu januari mwaka jana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...