Na Stella Kalinga, Simiyu

Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali itachimba visima kumi vya maji mara moja katika eneo la Mto Semu Kijiji cha Magwila wilayani Meatu na kujenga mtandao wa bomba kutoka katika visima hivyo mpaka mjini Mwanhuzi wilayani humo Mkoani Simiyu, ili kukabiliana na adha ya maji kwa wananchi baada ya kukauka kwa bwawa la Mwanyahina.

Prof. Mbarawa amesema hayo jana Novemba 19, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Mwanhuzi mara baada ya kutembelea na kuona Bwawa la Mwanyahina lililokauka ambalo ndiyo chanzo kikuu cha maji katika Mji huo na eneo la Mto Semu kilipo kisima kinachotumiwa sasa, ambapo watu wanachota maji kwa magari na kuwauzia wananchi mjini Mwanhuzi.

“ Mhe.Rais amenielekeza kwamba tutachimba visima kumi haraka kutoka kule ambako maji yanachotwa sasa, tutajenga mtandao wa bomba kutoka kwenye visima mpaka hapa mjini, ili maji yale yatolewe visimani na kuletwa kwenye mfumo wa maji wa hapa mjini,” alisema Mbarawa.

Katika hatua nyingine Mbarawa ameelekeza Wataalam wa Bonde la Ziwa Victoria kufanya utafiti katika eneo hilo ili kujua wingi wa maji na kuwahakikishia wananchi kuwa kwa sasa Wizara ya maji imetoa maboza makubwa matatu kwa ajili ya kusaidia kubeba maji kutoka kisima na kusambaza kwa wananchi, huku akiagiza ukarabati wa Bwawa la Mwanyahina kufanyika kwa kutoa tope lililojaa kwenye bwawa hilo.

Awali akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani amesema Bwawa la Mwanyahina limekauka kutokana na kujaa tope na ukame uliotokea wilayani humo katika msimu wa mvua wa mwaka 2018/2019.

Aidha, Dkt. Chilongani ameomba Wizara ya maji iweze kutoa kipaumbele kwa miradi yote ya maji iliyosanifiwa iweze kutekelezwa katika Wilaya ya Meatu, ili kuongeza hali ya upatikanaji wa maji vijijini na mjini.

Kwa upande wao wananchi wa Mji wa Mwanhuzi wameishukuru Serikali kwa kukubali kuwachimbia visima ambavyo vitawasaidia kuondokana na adha maji baada ya Bwawa la Mwanyahina kukauka na kusababisha wao kununua ndoo moja ya lita 20 kwa shilingi 100 hadi 200.

“Sasa hivi tunauziwa ndoo ya lita ishirini kwa shilingi 200, tunaishukuru Serikali kuona kilio chetu, pia tunamshukuru Waziri wetu wa Maji kwa mpango aliokuja nao wa kutuchimbia visima na kutuletea maji hapa mjini, tunaomba mpango huu ufanyike haraka, ili tuondakane na shida ya maji tuliyonayo sasa,” alisema Mariam Kashinje mkazi wa Mwanhuzi.

“Binafsi namshukuru Mbunge wetu kwa kutoa gari lake ambalo linatoa huduma ya maji bure, pia tunamshukuru Mhe. Diwani wetu Zakaria kuruhusu watu kuchota maji kwenye kisima chake na kubeba kwenye maboza na sisi wananchi tunanunua; lakini nimefurahishwa sana na mpango wa Waziri wa Maji aliyesema Mhe. Rais anataka tuchimbiwe visima naamini tatizo hili litaisha,” alisema Mboi Ngidinga.
 Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa(mwenye miwani katikati) akipata maelezo kuhusu kisima kilichopo eneo la Mto Semu kijiji cha Magwila wilayani Meatu, ambacho kinatumiwa kutoa huduma kwa sasa kwa wananchi wa Mji wa Mwanhuzi baada kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina ambalo ndiyo chanzo kikuu cha Maji katika Mji wa Mwanhuzi.

 Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani  (kushoto) akimuongoza Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa(wa tatu kulia) kuelekea katika kisima kilichopo eneo la Mto Semu kijiji cha Magwila wilayani Meatu Novemba 19, 2019, ambacho kinatumiwa kutoa huduma kwa sasa kwa wananchi wa Mji wa Mwanhuzi baada kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina ambalo ndiyo chanzo kikuu cha Maji katika Mji wa Mwanhuzi.

 Mbunge wa Jimbo la Meatu Mhe. Salum Khamis (mwenye kofia) akimuonesha jambo Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa(mwenye miwani kulia)alipotembelea kuona eneo la chujio la Maji katika Mji wa Mwanhuzi wilayani Meatu Novemba 19, 2019.

 Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani  (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa(wa pili kulia) kuhusu Bwawa la Mwanyahina chanzo kikuu cha Maji katika Mji wa Mwanhuzi ambalo limekauka kwa sasa, wakati wa ziara yake Novemba 19, 2019.

 Sehemu ya Bwawa la Mwanyahina chanzo kikuu cha Maji katika Mji wa Mwanhuzi ambalo limekauka kwa sasa ambalo Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa ameagiza lifanyiwe ukarabati kuondolewa tope.
 Baadhi ya wananchi wa Mjini Mwanhuzi wilayani Meatu wakipata huduma ya maji kutoka kwenye magari yanayosomba maji kutoka katika Kisima baada ya changamoto ya maji katika mji huo iliyosababishwa kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina.
 aadhi ya wananchi wa Mji wa Mwanhuzi wakiwa katika foleni ya kupata huduma ya maji kutoka kwenye magari yanayosomba maji kutoka katika Kisima baada ya changamoto ya maji katika mji huo iliyosababishwa kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina.
Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa(wa tatu kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya  Meatu, Mhe. Joseph Chilongani moja ya gari litakalotumika kwa dharura kusomba maji kutoka kisima kilichopo eneo la mto Semu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kabla ya kuchimbwa kwa visima kumi , wakati wa ziara yake Novemba 19, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...