Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Jasson Rweikiza (Mb) akifungua kikao kazi cha kamati yake naviongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora chenye lengo la kupokea mrejesho wa matumizi ya TEHAMA katika shughuli zinazofanya na TASAF uliowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga kwenye Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma jana.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakifuatilia mada kuhusu matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga kwenye Ukumbi wa Bunge jijini Dodo
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Rehema Migilla (Mb) akichangia hoja kuhusu mada ya matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga kwenye Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga akitoa ufafanuzi wa hoja zilizowasilshwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwanne Mchemba (Mb) akifunga kikao kazi cha kamati yake na viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora chenye lengo la kupokea mrejesho wa matumizi ya TEHAMA katika shughuli zinazofanya na TASAF uliowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga kwenye Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma jana.

……………………..

Na. James K. Mwanamyoto – Dodoma

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umepongezwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa kupata mafanikio ya kulipa ruzuku kielektroniki kwa wakati, ufanisi na uwazi kwa kaya maskini katika maeneo 16 ya majaribio nchini ambapo ufanisi wa kuzihudumia kaya hizo umeboreka kwa kiasi kikubwa.

Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa kamati hiyo kwa nyakati tofauti wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mara baada ya mrejesho wa matumizi ya TEHAMA katika shughuli zinazofanya na TASAF kuwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo Bw. Ladislaus Mwamanga kwenye Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Bw. Mwamanga amesema, malipo kwa njia ya kielektroniki katika maeneo 16 ya utekelezaji ambayo ni sawa na asilimia 10 ya walengwa yameongeza ufanisi na uwazi katika malipo, yanakwenda moja kwa moja kwa mlengwa aliyekusudiwa, yanawezesha uhakiki wa malipo kwa urahisi na kwa wakati, yanaongeza muda wa kufanya shughuli za maendeleo kwa walengwa, yanatoa fursa kwa walengwa kupata huduma bila usumbufu na yameipunguzia TASAF gharama za kuwasilisha ruzuku kwa walengwa.

“Asilimia 95 ya walengwa wanalipwa kwa njia ya mtandao kupitia simu za viganjani na asilimia 5 ya walengwa wanalipwa kupitia akaunti za benki”, amefafanua Bw. Mwamanga.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Angelina Malembeka (Mb) ameipongeza TASAF kwa ufuatiliaji mzuri wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Nchini hususani kwenye eneo la malipo kwa njia ya kielektroniki, hivyo kusaidia kuondoa udanganyifu uliokuwa ukifanywa kipindi cha nyuma na baadhi ya watendaji na walengwa wasio na uadilifu.

Naye, Mhe. Mwantum Haji ameipongeza TASAF kwa kufanya kazi vizuri na weledi hususani kwenye Mfumo wa Kupokea na Kushughulikia Malalamiko ya Walengwa ambapo wametoa elimu ya kutosha kwa walengwa kiasi cha kuwahamasisha kuutumia ipasavyo ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo ya malipo kwa njia ya kielektroniki na kuitaka TASAF kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuzikwamua kaya maskini kiuchumi.

Kwa upande wake, Mhe. Saada Mkuya (Mb) ameipongeza TASAF kwa utendaji kazi mzuri kwani faida ya utekelezaji mzuri wa mpango hauzinufaishi kaya maskini pekee bali ni msaada kwa Serikali katika jitihada zake za kuwawezesha wananchi wake kukua kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi na jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ameitaka TASAF kutumia vema mifumo ya TEHAMA kuongeza ufanisi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwanne Mchemba (Mb) amempongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika na Naibu waziri wake, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa usimamizi mzuri wa majukumu yanayotekelewa na TASAF.

Mhe. Mchemba amempongeza pia Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga kwa kutekeleza vema maagizo na ushauri ya kamati yake na hatimaye TASAF kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kupitia Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo imekuwa na manufaa kwa walengwa na tija kwa Serikali katika kusimamia malipo ya fedha za ruzuku kwa walengwa.

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa imeridhishwa na utendaji kazi wa TASAF kupitia mifumo ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na na malipo kwa njia ya kieletroniki uliofanyiwa majaribio kwa mafanikio katika maeneo 16 ya utekelezaji ambayo ni Arusha jiji, Unguja, Ilala Manispaa, Temeke manispaa, Kigoma Manispaa, Bahi, Urambo, Songea manispaa, Bagamoyo, Mkuranga, Kilwa, Kisarawe, Muheza, Siha na Mpanda mji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...