*Lengo ni kujipatia chakula kisicho na maradhi yatokanayo na ulaji wa vyakula vyenye kemikali 

Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii

SHIRIKA la kuendeleza Kilimo hai Tanzania(TOAM) limeeleza kwa kina kuhusu faida zinapatikana kwa kujihusisha na kilimo hicho huku likitoa rai kwa Watanzania kuhakikisha wanajihusisha nacho ili kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla na kuepukana na kula vyakula vyenye kemikali.

Akizungumza wakati wa semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu kilimohai, Mshauri wa Kilimohai kutoka TOAM Costantine Akitanda amesena ipo haja ya watanzania kuwekeza nguvu zao kwenye kilimo hicho.

"Tunapozungumzia kilimohai tunamaanisha ni kilimo ambacho kinaendeshwa kwa kutumia uasilia na sayansi.Uzuri wa kilimo hiki kinalipa na mazao ya organic yanasoko la uhakika.TOAM kwa kutambua faida za kilimo hicho katika maeneo mbalimbali nchini tumeendelea kuwahamasisha wakulima kulima kilimo hiki na tumekuwa tukiwatambua kwa kuwasajili kwa wale wanaokidhi vigezo na tutaendelea na jukumu letu,"amesema Akitanda.

Kuhusu faida za kilimohai, Akitanda amesema zipo nyingi mojawapo ni kwamba kilimo hicho ni rafiki wa mazingira na kubwa zaidi hata mazao yatokanayo a kilimo cha aina hiyo hayana madhara kiafya kwani uzalishaji wa mazao hautokani na mbolea za viwanda na kimekali.

"Wanaojihusisha na kilimo hiki ndani ya mashamba yao kila kitu kinapatikana humo, kama anahitaji mbolea basi itatokana na mbolea ya mifugo ambayo mara nyingi iko shambani.Kama atahitaji dawa ya kufukuza wadudu shambani nayo itatokana na mimea iliyomo humo humo.Hivyo ni kilimo ambacho hakitumii dawa na kemikali.

"Wanaokula vyakula ambavyo asili yake ni organic kwa sehemu kubwa hawana matatizo ya kiafya kama wanaokula vyakula vyenye kemikali. Pia kilimo cha organic mazao yake yana thamani kubwa ukilinganisha na mazao yasiyo ya kilimo hai,"amesema.

Akitanda ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kilimo hicho shirika lao limeweka nguvu ya kuhamasisha, kuelimisha, kushauri na kueleza namna bora ya kukifanikisha.

Kuhusu sera,Akitanda amesema sekta ya kilimo hao inatambuliwa na Serikali kwa kuwepo na sera na miongozo na ndio maana hata wao wamekuwa na uwezo wa kuendelea kukisimamia na kukiendeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo hai ndani ya nje ya Tanzania.

"Serikali ilishaweka sera kwa ajili ya sekta hii ya kilimo hai , ndio maana TOAM tumekuwa huru kuhamasisha na kusimamia kilimo hiki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.Kwa kuwa zipo sera inayotuongoza hata Serikali imetoa kipaumbele, kuna vituo vya utafiti kuhusu kilimo hai ambavyo pia vinazalisha mbegu asili na tunashirikiana vizuri tu,"amesema.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kwa sasa nchi nyingi za Afrika zimekuwa na changamoto ya kuwepo kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo mengi yanatokana na ulaji wa vyakula vyenye kemikali na kutoa mfano wa ugonjwa kansa, hivyo ameshauri ili kuepukana hali hiyo umefika wakati wa kujikita katika kilimo hai.

Kuhusu waandishi wa habari walioko katika semina hiyo Akitanda amesema ili kuhakikisha taarifa za kilimo hao zinafika kwa uhakika kwa wananchi wameamua kutoa elimu kuhusu kilimo hicho kwa waandishi wa vyombo vya habari hasa kwa kutambua nafasi waliyonayo katika jamii kuhusu masuala yanayohusu jamii ikiwemo ya sekta ya kilimo.

"Tunaamini baada ya kukutana na waandishi wa habari na kupeana mafunzo kuhusu kilimo hai, kwanza mtakuwa bega kwa bega kushirikiana nasi na pili mtatua mabalozi wazuri wa kilimo hiki,"amesema Akitanda.

Wakati huo huo amesema Jauari mwakani kunatakuwa na maonesho yanayohusu kilimo hai ambapo wakulima zaidi 12,000 watakutana mkoani Kilimanjaro.Pia kabla ya maonesho hayo kuna mikutano mingine kadhaa itafanyika mwaka huu ikiwa ni mchakato wa kuelekea katika maonesho hayo ambapo watanzania wataoneshwa namna kilimo hai kinavyoendeshwa na faida zake.

Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano kutoka Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa(FAO) Emmanuel Kihaule ametumia nafasi hiyo keueleza kuwa kilimo hicho ni muhimu na matumani yao baada ya waandishi kupata mafunzo hayo watatumia kalamu zao kuleta mapinduzi makubwa katika sekta inayohusu kilimo hicho kwa ujumla.

Pia amesema katika kuhakikisha kilimo hai kinasonga mbele, FAO pamoja na mambo mengine wamekuwa wakiangalia sera, mipango na mikakati iliyopo kuhusu kilimo hicho.Mengine ni kufuatilia uzalishaji ambapo katika hilo wamejikita kuangalia namna gani jami imejikita kushghulika na kilimo.

Kihaule amesema FAO inaangalia pia uongezaji wa thamani ya mazao ya organic pamoja na usimamizi wa rasilimali za asili ikiweko ikolojia ambayo maana yake rahisi ni sawa na kusema mahusiano ya binadamu na mazingira.

"Tunayo maswali ya kujiliuza kama leo hii ndani ya miaka 40 hata mito ambayo ilikuwa inatoa maji kutokana na uwepo wa ikolojia sasa imekauka, je baada ya miaka 500 tujiulize hali itakuaje? Tumekuwa na viwavijeshi na aina nyingi ya wadudu waharibifu wa mazao yawapo shambani lakini ukweli ni kwamba kuna tatizo la uharibifu wa ikolojia, hivyo tunahimiza kila mmoja wetu sasa aone umuhimu wake.Kila kiumbe ambacho unakiona shambani au katika mazingira yanayokuzunguka wanafaida zake.Lima shamba lako bila kuharibu ikolojia hii,"amesema Kihaule.
 Moja ya shamba ambalo linalimwa kwa mfumo wa kilimohai linavyoonekana baada ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenda kujifunza kwa vitendo kuhusu kilimo hicho mkoani Kilimanjaro.Mafunzo hayo yameandaliwa na TOAM kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa( FAO)
Mwanafunzi wa kidato cha pili James Lemy Temba anayeishi Kijiji cha Uru Shimbwe akiwa shambani kwao.Kwa mujibu wa baba mzazi wa James , Lemy Temba amesema kijana huyo anamuandaa katika kulima kilimohai ambalo yeye ameririthi kwa baba yake mwaka 1979 na hivyo naye anajiandaa mtoto wake ambaye ndio wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto wake tisa.
Baadhi ya waandishi waliopata fursa ya kujifunza kuhusu kilimohai wakiwa  nyumbani kwa moja ya wakulima wa kilimo hicho mkoani Kilimanjaro .Waandishi hao walikwenda kujifunza kwa vitendo kilimo hicho
Waandishi wa habari, ofisa wa TOAM, FAO , viongozi wa Kata ya Uru Shimbwe wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakulima wa kilimohai mkoani Kilimanjaro .Waandishi hao walikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo hai baada ya kuelezwa kwa nadharia faida za kilimo hicho na umuhimu wake kwa Watanzania

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...