Na, farida Saidy, Morogoro
Zoezi la kupiga kura kuchagua wenyeviti wa Vijiji, Mitaa, na Vitongoji limefanyika kwa Amani Mkoani Morogoro ambapo Halmashauri sita kati ya tisa zimeshiriki katika zoezi hilo lililofanyika Nchini kote Novemba 24, 2019 huku zaidi ya wakazi laki moja Mkoani humo wakitajwa kushiriki zoezi hilo.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoani Morogoro Jacob Kayange wakati akitoa taarifa za awali kuhusu mwenendo wa zoezi hilo Mkoani humo.

Kayange amebainisha kuwa Halmashauri zilizoshiriki katika zoezi hilo ni pamoja na Halmashauri ya Mji Ifakara, Kilombero, Ulanga, Morogoro, Kilosa na Manispaa ya Morogoro huku Halmashauri ya wilaya Gairo, Mvomero na Malinyi hazikushiriki uchaguzi huo kwa sababu ya wagombea wake kupita bila kupingwa baada wagombea wengine kukosa sifa za kushiriki uchaguzi huo.

“Mkoa wetu wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa inayoshiriki zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa linalofanyika leo Novemba 24 mwaka huu, na katika Mkoa wetu Halmashauri sita kati ya tisa ndizo zitakazoshiriki katika zoezi la kupiga kura na Halmashauri tatu hazitoshiriki …..”, alisema Kayange.

Kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pamoja na vituo vingi kukutwa havina wapiga kura kwa madai kuwa wagombea katika maeneo hayo wamepita bila kupingwa bado maeneo hayo ya kupigia kura vilionekana kuwa katika hali ya Amani na Utulivu.

Mitaa iliyotembelewa wakati wa zoezi la kupiga kura ni pamoja na kata ya Mbuyuni katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambayo ina Mitaa sita, ambapo mitaa mitano kati ya hiyo wagombea wake wa Kutoka Chama cha Mapinduzi CCM walipita bila kupingwa huku Mtaa mmoja wa Magulumbasi kuripotiwa kuwa na mpinzania kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambaye alichukua fomu lakini alikosa sifa baada ya kujaza fomu hiyo.

Issa Juma ambaye ni Mkazi wa Mtaa wa Mgonahanzeru chini ya mgombea Kerene Jackson Huzi amesema ana imani kwamba mgombea wao anafaa kutetea kiti hicho kwa kuwa amekuwa karibu katika kusaidia kero mbalimbali za wananchi katika kipindi chote alichokuwa madarakani.

Naye mgombea Nafasi ya Uenyekiti wa mtaa wa Mgonahanzeru Kerene Jackson Huzi ambaye amepita bila kupingwa amewasihi wagombea wenzake waliopita bila kupingwa kujitahidi kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Kwa mujibu wa Mratibu wa zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Morogoro Bw. Jacob Kayange , jumla ya Watu waliojiandikisha kupiga kura katika Mkoa huo ni 1,101,588 sawa na asilimia 79 ya wakazi wake. Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa na wasimamizi wa Uchaguzi huo baadae hii leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...