Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Usirika Dkt. Titus Kamani akiongea na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Hivi karibuni Jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu Bw. Athanas Mutwe akiongea na watumishi wa Tume wakati wa Kikao cha Watumishi hivi karibuni
Kaimu Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akisisitiza jambo wakati wa kikao na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Jijini Dodoma
 Bi. Veneranda Mugoba mtumishi wa Tume akichangia mada iliyokuwa ikiendelea wakati wa kikao cha Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Jijini Dodoma 
Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao cha Watumishi na Viongozi wa Tume.
Kikao kikiendelea


Sekta ya Ushirika imetajwa kuwa moja ya maeneo muhimu ambayo yana fursa kubwa katika kushiriki na kuendeleza Uchumi wa Tanzania kupitia maendeleo ya Viwanda ili kuifikisha nchi katika Uchumi wa kati ifikapo 2025.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Titus Kamani wakati wa kikao cha Watumishi wa Tume kilichofanyika Jijini Dodoma hivi karibuni. Dkt. Kamani alieleza hayo alipokuwa akifafanua vipaumbele vya kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ni pamoja na kuhakikisha kuwa ajenda ya viwanda inakuwa ni miongoni mwa masuala muhimu katika mipango na mikakati ya Taasisi hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti huyo alieleza Sekta ya Ushirika katika harakati za kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuendeleza viwanda ni wakati muafaka sasa kwa kila mtumishi kuangalia namna bora anavyoweza kuja na ubunifu wa namna bora ya kusaidia kuongeza thamani ya mazao ya wakulima. Viwanda hivyo vikichakata mazao mbalimbali ya Kilimo, uvuvi, madini na mengine. Akiongeza kuwa viwanda hivyo vianzishwe kwa kuzingatia masuala yanayoleta changamoto sana katika Sekta ya Ushirika akitolea mfano eneo la vifungashio vya mazao eneo ambalo bado lina uhitaji mkubwa nchini.

“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuchangia mawazo na utekelezaji wa maeneo ya kuendeleza, kuanzisha au kuboresha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. Hivyo kuongeza mnyororo wa thamani,” alisema Dkt. Kamani

Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na watumishi wa Tume katika kikao hicho alisema baada ya Vyama 4,413 kukaguliwa na Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika hivi karibuni Tume ichukue fursa hiyo kuendelea kuboresha taswira ya Sekta ya Ushirika kwa kutumia matokeo ya kaguzi zilizofanyika kwakuwa kaguzi hutoa picha na muelekeo wa utendaji.

Aidha, Dkt. Ndiege alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa weledi na kutumia taaluma zao vizuri katika kutimiza wajibu na majukumu yao ili Tume iweze kutekeleza wajibu na matarajio makubwa ya wananchi na wanaushirika nchini.

Kaimu Mrajis aliongeza kuwa watumishi waendelee kuwa wabunifu kubuni miradi mipya, njia bora za utendaji ili huduma za Ushirika ziendelee kuwa bora na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za Ushirika katika maeneo mengi zaidi. Mrajis alishauri watumishi kuendelea kuibua tafiti na mawazo ya kuendeleza na kuanziasha viwanda vitakavyotumia malighafi kutoka vyama vya Ushirika. Akieleza kwa kufanya hivyo tutaisaidia Serikali kwa kuongeza ajira na kukuza pato la Taifa.

“Tuongeze hamasa na elimu ya Ushirika kwa wale ambao bado hawajajiunga na Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na Ushirika ili kupitia Ushirika wananchi waweze kupata maendeleo kwa urahisi pamoja na kunufaika na viwanda kupitia Sekta ya Ushirika. watumishi niwaombe muendelee kuandika mapendekezo mbalimbali yenye lengo la kutafuta ushirikiano na wadau wa maendeleo ili tukuze na kuendeleza viwanda vya Ushirika, alisema Dkt. Ndiege ” 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu Bw. Athanas Mutwe akiongelea masuala ya kiutumishi katika kikao hicho alisema Watumishi ni kiungo muhimu sana chenye mchango mkubwa katika kuendeleza Sekta ya Ushirika na hatimaye kufikia Tanzania ya Viwanda. Bw. Mutwe aliwataka watumishi hao kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma kwa manufaa yao binafsi na Taifa lote.

“Niwaombe watumishi wote kila mmoja wetu kuzingatie maadili ya utumishi wa Umma, tufanye kazi tukijua tumepewa dhamana ya kusimamia rasilimali na sekta muhimu ya Ushirika,” alisema Mutwe 

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilitoa fursa kwa watumishi wa Tume kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Ushirika nchini ili kuongeza tija na ufanisi zaidi wa Sekta hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...