Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya watu wenye ulemavu ili wanufaike na mikopo inayotolewa na Halmashauri hizo.

Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga katika kongamano la asasi za kiraia (AZAKI) linaloendelea Jijini Dodoma.

Amesema watu wenye ulemavu wamekuwa hawatumii fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya ujasiriamali.

“Matokeo yake wanaishia kuishi maisha ya utegemezi na kuomba omba mitaani, ninajua kabisa watu wenye ulemavu hawawezi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha ikiwemo mabenki kutokana na hali yao, ndio maana serikali kwa kuliona hilo iliamua kutenga asilimia 2 kati ya 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi maalum yakiwemo ya watu wenye ulemavu,” amesema.

Ameeleza watu wengi wenye ulemavu bado hawajajitokeza vya kutosha kutumia fursa ya mikopo kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi hivyo wakurugenzi na maafisa hao wanatakiwa kutoa elimu ili waweze kujitokeza.

Amebainisha katika mwaka wa fedha 2018/19 Halmashauri nchini zilitenga jumla ya Sh. Bilioni 54.08  kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lakini mpaka kufikia Juni 30, mwaka huu kiasi cha fedha kilichokuwa kimetolewa ni Sh.Bilioni 42.06  ambapo vikundi vya watu wenye ulemavu walipata kiasi cha fedha Sh.Bilioni 3.87.

“Kwa mwaka wa fedha 2019/20 serikali imetenga kiasi cha fedha Sh.Bilioni 62.22 ambapo wanawake na vijana  wametengewa Sh.Bilioni 24.9 na watu wenye ulemavu wametengewa Sh.Bilioni 12.4,”amesema.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga akizungumza katika mkutano wa majadiliano kuhusiana na fursa za mikopo kwa watu wenye mahitaji maalum kwenye wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) inayoendelea jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...