Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya Mabango yaliyobebwa na wananchi wa eneo la Mtumba Dodoma walipoandamana hadi ofisi za Wizara kuwasilisha kilio chao cha kutopatiwa fidia ya maeneo yao ulipojengwa Mji wa Serikali Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tutubi Mangazini (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)






Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza mmoja wa wananchi wa eneo la Mtumba walioandamana hadi ofisi za Wizara kuwasilisha kilio chao cha kutopatiwa fidia ya maeneo yao ulipojengwa Mji wa Serikali Dodoma.

 
Baadhi ya wananchi wa eneo la Mtumba mkoani Dodoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) walipokwenda kuwasilisha kilio chao cha kutolipwa fidia ya maeneo ulipojengwa Mji wa Serikali Mtumba.
………………….

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewatuliza takriban wananchi 49 wa eneo la Mtumba Dodoma waliokuwa na hasira ya madai ya kutolipwa fidia maeneo yao ulipojengwa Mji wa Serikali.

Dkt Mabula aliwatuliza wananchi hao leo tarehe 11 Novemba 2019 jijini Dodona walipoandamana kuelekea ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi jijini Dodoma baada ya jitihada zao za kupatiwa fidia ya maeneo yao kushindwa kupatiwa ufumbuzi na ofisi ya jiji la Dodoma.

Dkt Mabula alisema, Wizara yake imeyapokea malalamiko ya wananchi hao na kuwataka kuwa na subira hadi hapo uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakapomalizika tarehe 24 Novemba 2019 na kupata viongozi watakaoshirikiana nao wakati wa zoezi la uhakiki wa mipaka na kubaini wamiliki halali wa maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Wizara yake haina uhakika na wamiliki wa maeneo hayo hadi hapo timu maalum itakapoenda kufanya uhakiki ambao kila mwananchi anayedai kuwa na eneo Mtumba athibitishwe sambamba na kujiridhisha kuwa maeneo hayo ni ya kwao kwa kuwa taarifa zinzonesha eneo wanalodai linamilikiwa na Jeshi.

‘’Suala la msingi hapa ni kutambua maeneo, maendelelezo yoyote katika eneo hilo yasiwatishe na cha msingi hapa ni kwenda uwandani kujiridhisha uhalali wa wamiliki’’ alisema Dkt Mabula.

Awali baadhi ya wananchi hao wameeleza kusikitishwa na jinsi wanavyozungushwa kupatiwa fidia za maeneo yao tangu mwaka 2016 jambo lililowafanya kuandamana hadi ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kuonana na Waziri mwenye dhamana ya ardhi.

Mmoja wa wananchi hao Jakson Simon alisema, anashangazwa na jinsi wanavyohangaika na fidia kwa muda mrefu wakati uhakiki ulishafanywa mara kadhaa na jeshi kwa ushirikiano na maofisa wa Jiji la Dodoma lakini linapokuja suala la kulipwa fidia hakuna utekelezaji wowote.

Mwananchi Mwingine Geofrey Stephano alisema, maelezo kuwa eneo walilokuwa wakilimilki ni la jeshi hawakubaliani nalo kwa kuwa wao hawana ugomvi na Jeshi kwa kuwa uhakiki wa awali ulifanywa na jeshi hilo na kuanisha mipaka kati ya maeneo yao na jeshi.

Kwa muda sasa baadhi ya wananchi wanaodai kumiliki maeneo ulipo Mji wa Serikali Mtumba wamekuwa wakidai fidia na wengine wakidai kiasi walicholipwa kama fidia ni kidogo jambo lililosababisha kuhangaika ofisi mbalimbali kudai haki yao na sasa kuamua kuandamana hadi ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dodoma kuonana na Waziri wa Ardhi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...