Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipongezana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo Novemba 14/2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo. Novemba 14/2019 . Wengine kutoka kulia, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Teguest Mengtsu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwaaga wananchi baada ya kuzindua mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela baada ya uzinduzi wa mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya Tanzania Bwana Benedikti Konga. wakati alipotembelea maonyesho ya uzinduzi wa mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo Novemba 14,2019.PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

…………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia tarehe 17 – 23 Novemba, 2019 litaanza zoezi la kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo ametoa onyo kwa yeyote atakayevuruga zoezi hilo kuwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Vikundi vya ulinzi wa jadi au vya ulinzi binafsi au vya mashabiki wa vyama vya siasa havitaruhusiwa kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni au maeneo ya uchaguzi.”

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Novemba 14, 2019)alipozindua Wiki ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasioambukiza sambamba na Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza

Waziri Mkuu amesema kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Polisi, Mgambo wenye sare na Maafisa wanaosimamia ulinzi vitatumika kuhakikisha kunakuwepo na utulivu wakati wa kampeni na uchaguzi.

Kadhalika,Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na Serikali imejipanga vya kutosha kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kubadili tabia na mwenendo wao wa ulaji wa vyakula kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda.

Waziri Mkuu amesema kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe; kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu; kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na mafuta. “Tujipange kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na uharibifu wa mazingira na tabianchi.” 

Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki. “Katika eneo hili, niweke msisitizo kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluh Hassan.

“Tuendelee kuhamasisha kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja ambavyo husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi. Tutumie vikundi vya joggingvilivyopo kwenye kata na mitaa au vijiji vyetu ili kupata mwendelezo wa jitihada zao.

Amesema Halmashauri zote zihakikishe zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi katika kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi pia watumie maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi.

“Kwa upande wa wanafunzi kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe wanakimbia mchaka mchaka ili waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo litawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza.”

Amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio kwenye jamii na ulimwenguni kote, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2016 zinaonesha kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016. 

“Taarifa za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kuwa, pamoja na changamoto hizo za kiafya, magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri sana nyanja nyingine za maisha. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka 20, kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya zitafikia Dola za Marekani trilioni 47.”

Waziri Mkuu amesema fedha hizo zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka 50. Kwa nchi za uchumi wa kati na chini, magonjwa hayo yatagharimu mataifa hayo Dola za Marekani, trilioni saba katika kipindi cha 2011 hadi 2025. 

Amesema gharama hizo zinatokana na kuongezeka kwa gharama za huduma za matibabu na upotevu wa nguvukazi unaosababishwa na maradhi hayo, mfano, makadirio yanaonesha kuwa gharama za huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya afya. Ugonjwa wa kisukari pekee utagharimu zaidi ya Dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya afya duniani.

Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha magonjwa ambayo hayawezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Aliyataja magonjwa hayo kuwa ni pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho, kinywa, masikio, pua na koo. “Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote za kimaisha.”

Waziri Ummy alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa milioni 4.2 mwaka 2018, ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.

Kwa upande wao, wadau wa masuala ya afya wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza kiwango cha bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 31 hadi sh. bilioni 270.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...