Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema sekta ya fedha 
imekua na kuimarika, licha ya changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa 
zikijitokeza huku akitaja mambo nane ambayo yanastahili kuzatamwa kwa kina katika sekta hiyo.

Dk.Mpango amesema hayo leo Novemba 21,2019 wakati akifungua mkutano 
mkuu wa 19 wa sekta ya fedha nchini.Dk.Mpango amefungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk.John Magufuli.

"Napenda niwapongeze kwa dhati wadau wote wa sekta ya fedha kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa hadi sasa. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ameyaainisha vizuri, nitaomba nijielekeze kuwaomba washiriki wa kongamano hili watusaidie mawazo na mikakati ya kupiga hatua zaidi katika maeneo yafuatayo,"amesema.

Dk.Mpango amesema kwanza amewaomba watumie fursa hiyo kujadili kwa kina namna bora itakayowezesha taasisi za fedha kuwafikia wananchi wengi wa vijijini kwa gharama nafuu. Takriban asilimia 66 ya Watanzania wanaishi vijijini kwa kutegemea kilimo ambacho ndiyo chanzo kikuu cha kukidhi mahitaji ya chakula nchini na malighafi kwa ajili ya viwanda. 

"Hali halisi ni kuwa wengi wao bado hawajafikiwa na huduma za fedha (ikiwemo mikopo),"amesema Dk.Mpango.Amesema pili ni eneo la riba za mikopo bado ziko juu kiasi kwamba watu wengi wanashindwa kukopa na baadhi ya waliokopa kushindwa kurejesha. Hivyo, licha ya juhudi za kuboresha sekta hiyo ambazo Gavana amezisema,ameomba wadau 

wa sekta hiyo watoe mapendekezo ya mikakati ya kushusha riba ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu na hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi. Itafaa kongamano hilo libainishe mikakati mipya ya kupunguza na kudhibiti kiasi cha mikopo chechefu katika mabenki. 

Wakati jambo la tatu ni kwamba mikopo kwa sekta ya kilimo bado siyo ya 
kuridhisha, kwani imekuwa ikipokea chini ya asilimia 5 ya mikopo yote itolewayo na mabenki. Sekta hiyo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.3 kwa kipindi cha miaka 4 iliyopita ikilinganishwa na matarajio ya Serikali ya ukuaji wa asilimia 13.1 ifikapo 2025.

" Sekta ya kilimo ni muhimu siyo tu katika kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda, lakini pia kama nilivyokwisha sema ndiyo chanzo kikuu cha chakula na fursa za ajira kwa Watanzania walio wengi, lakini pia ndiyo sekta yenye uwezo wa kupunguza umaskini na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa. 

"Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mjadala wenu utaangalia namna bora ya 
kuzifanya taasisi za fedha kuongeza mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kilimo cha mazao, ufugaji, uvuvi na biashara husika,"amesema Dk.Mpango.
Pia ameungana na Gavana kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali kuboresha sekta ya fedha, ikiwemo kujenga Kanzidata za taarifa za wateja na utoaji wa vitambulisho vya Taifa. 

Hata hivyo ametoa rai kwa Mamlaka husika kuharakisha utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa upande mmoja na mabenki kwa upande wao kuhakikisha yanaboresha utoaji wa huduma za kifedha. Dk.Mpango amesema jambo la tano ni kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa 

miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway) ambayo itarahisisha usafirishaji na uchukuzi.Pia ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji kwenye mto Rufiji (2,115 MW) na maboresho ya sekta ya anga. Miradi hiyo inahitaji fedha nyingi 
kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje. 

"Hivyo, ni matarajio yangu mkutano huu utajadili na kutoa mapendekezo ya 
namna taasisi za fedha zinavyoweza kuchangia katika upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi hii ya kimkakati na ile ya sekta binafsi,"amesema.
Wakati jambo la sita ni kuhusu umuhimu wa sekta ya fedha katika ulipaji wa kodi. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, wastani wa makusanyo ya kodi kwa mwezi yalikuwa Sh. bilioni 850, lakini sasa ni wastani wa Sh.trilioni 1.3. 

"Kwa miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukikusanya wastani wa zaidi ya Sh.trilioni 1.5 kuanzia Julai hadi Oktoba 2019. Pamoja na kwamba sekta ya fedha imekuwa miongoni mwa walipa kodi wazuri.

"Napenda nitoe mwito kwa taasisi hizi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo ya malipo ya ukusanyaji wa kodi. Na kwa misisitizo, ni muhimu hili iendane na matumizi ya kielektroniki katika kufanya miamala,"amesema. 

Dk.Mpango amewakumbusha wadau hao kuwa kuna Mpango wa Taifa wa 
Kuboresha Mazingira ya Biashara na Mpangokazi wa utekelezaji wake 
umeshakamilika. Hivyo ametoa mwito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta ya fedha kushiriki kutekeleza Mpangokazi huo ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango akizungumza wakati akifungua mkutano wa uliokutanosha mabenki na Benki Kuu ya Tanzania BoT unaofanyika kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es salaam.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga akizungumza katika mkutano huo uliofanyika leo katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania BoT jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabenki (TBA) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa shukurani zake kwa serikali na Benki Kuu ya Tanzania BoT kwa usimamizi wake mzuri kwa taasisi za fedha nchini.
Baadhi ya washiriki wa mkutan huo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.
 
Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi za kifedha na mabenki.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...