KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao, imelitaka Jeshi la Polisi kumuhoji, kumchunguza na kumchukulia hatua za kisheria Mshauri Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo Seif Sharif Hamad kwa kauli zake za uchochezi alizotoa kwa kuwahamasisha wafuasi wake watumie silaha za jadi kuanzisha vurugu visiwani hapa.

Hatua hiyo inatokana na kiongozi huyo kutoa matamshi mbele ya vyombo vya habari kwa kuwataka viongozi na wanachama wa ngazi zote za chama chake kwa maeneo ya mijini na vijijini kwa upande wa Unguja,Pemba kuzilinda ofisi zote za chama chao na kutoruhusu
kuchukuliwa kwa ofisi hizo.

Katika mkutano huo ambao aliufanya juzi kwenye ofisi ya chama hicho mjini Unguja Maalim Seif alisema wamevumilia vya kutosha na kwamba sasa wanasema basi kutokana na kuwa ni muda mrefu wamevumilia kutokana na maslahi ya nchi lakini wameona wenzao hawako tayari
kuilinda amani.

Maalim Seif alisema wako tayari kumwaga mboga wenzao wakimwaga mchuzi na kwamba alisema chama cha CUF kwa upande wa Pemba kimeanza kujaribu kutaka kuvamia ofisi za ACT-Wazalendo kwa lengo la kuzichukua na kuzifanya ofisi za chama chao kwa madai ni ofisi zao.

Akizungumza jana na vyombo vya habari Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa ya CCM,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao,alisema kutokana na kauli za Hamad ambaye aliyotoa katika vyombo vya habari ni lazima jeshi la Polisi lichukue hatua za haraka za kumthibiti kiongozi huyo kabla nchi haijaingia katika machafuko.

Katibu huyo amelaani taarifa hiyo ya Maalim Seif kuwa inalenga kuvuruga hali ya amani na mshikamano wa wananchi na kuirejesha Zanzibar katika machafuko ya kisiasa.

Aliongeza kuwa katika taarifa hiyo ya Maalim Seif alimtaja Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally kuwa moja ya mikutano yake ya ndani iliwahamasisha viongozi wa CCM kuratibu mipango ya vurugu,jambo ambalo si kweli kwani kiongozi huyo alifanya ziara yake kwa lengo la kuimarisha chama katika kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020.

Pia,Katibu huyo alisema taarifa alizotoa Maalim Seif za kumtuhumu Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru kuwa ziara yake za visiwani Zanzibar imelenga kuhamasisha Vurugu na kwamba jambo hilo ni la upotoshaji na si za si za kweli.

Alisema Maalim Seif ni mwanasiasa aliyetawaliwa na ubinafsi pamoja na ukatili wa kupindukia kutokana na kuwa furaha yake ni kuona damu za wananchi wa Zanzibar zinamwagika bila hatia na kwamba ndio maana kila anapoona hali ya amani inaimarika visiwani hapa yeye anaanzisha vurugu kwa kusudi.

Katibu Catherine, alimtaja Maalim Seif kuwa ni bingwa wa migogoro toka wakati wa Rais wa awamu ya pili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) Marehemu Mzee Aboud Jumbe Mwinyi ambapo Maalim Seif alitengeneza mgogoro akiwa ndani ya CCM na
hatimaye akatimuliwa.

Aliongeza kuwa maisha ya kisiasa ya kiongozi huyo wa upinzani Maalim Seif yametawaliwa na usaliti,uongo,chuki binafsi na hata katika uchaguzi wa kwanza Tanzania uliofanyika katika kipindi cha mwaka 1995, aliibuka na kudai ameshinda wakati akijua hakuwa
na uwezo huo.

Katika maelezo yake Catherine, alisema Maalim Seif aseme ukweli wa kuwa ameogopa ujio wa Katibu Mkuu Dk.Bashiru Zanzibar kuja kufunga mitambo ya kufanikisha uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema kuwa hakuna wa kuizuia CCM kushinda katika uchaguzi huo kwani tayari imemaliza kazi na kwa sasa inajipanga kwa ushindi mkubwa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Pia,alisema ushindi huo utatokana na Utekekelezaji Mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, alivyoimarisha Nyanja mbalimbali za kiuchumi,kisiasa,kijamii na kimaendeleo.

Katibu huyo Catherine, alisema Dk.Shein amekuwa ni kiongozi wa mfano ambaye ni mwadilifu, mchapakazi, mwenye hekima na shujaa wa kuasisi maendeleo.

“ Maalim Seif eti anasema kuwa Dk.Shein anawagawa wananchi hilo si kweli kwani Rais wetu amefanya mambo mengi ya maendeleo yanayowanufaisha wananchi wote hata huyo Maalim Seif anayebeza na kumtukana Rais wetu pia naye ananufaika na maendeleo haya,”
alisema Catherine.

Hata hivyo Katibu Catherine alimuonya Maalim Seif, alihamishie mgogoro wa chama cha ACT-wazalendo na CUF akaupeleka CCM kwani taasisi anayopambana nayo si ya kiwango chake.

Pia alihoji taarifa aliyotoa ambayo alidai kuwa takwimu za ACT- Wazalendo kukubalika Zanzibar kwa asilimia 64 na CCM kukubalika kwa asilimi 34, kuwa zimefanywa na taasisi gani kupitia vyanzo gani vya uhakika kwani hizo ni takwimu za uongo zinazotumiwa na Maalim Seif.

Alisema kwa takwimu hizo ambazo hazikuzingatia uwepo wa vyama vingine vya kisiasa ambavyo vina usajili na wanachama nchini kama vile ADA,TADEA, TLP,CHADEMA na CUF ni takwimu za kupuuzwa.

Catherine alisema kila siku zikienda Maalim Seif anaendelea kufilisika kisiasa ndio maana akapewa nafasi ya ushauri ndani ya Chama Cha ACT-Wazalendo kinachojipanga kushindana na CCM huku Zanzibar hakina hata balozi wala Diwani.

Pamoja na hayo Katibu huyo, aliwambia wafuasi wa Maalim Seif kuwa makini na kiongozi huyo ambaye amekisaliti chama alichokianzisha cha CUF hivyo hawezi kushindwa kusaliti ACT-Wazalendo.

Catherine alisema maalim Seif hana sifa za uongozi kwani uongozi ni wito na unatoka kwa mwenyezi mungu lakini kiongozi huyo amekuwa akilazimisha kupata nafasi hiyo kupitia njia haramu.

Alisema siasa za maji taka zimepitwa na wakati na viongozi wa kisiasa wanaondelea na siasa hizo watadhibitiwa na Vyombo vya Dola.

Catherine alisema CCM itaendelea kushindana kwa sera,hoja,na utendaji wa kazi na sio marumbano na porojo kwani wananchi wanahitaji maisha bora.

“Dk.Shein ametekeleza Ilani ya CCM kwa kununua boti za kisasa,majengo ya kisasa, huduma za afya bure,elimu bure, barabara za lami zipo kila sehemu na mengine mengi …lakini
ukimuuliza Maalim  Seif kafanya nini hata kisima kimoja cha maji hajachimba,”alisema.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao akizungumza na Vyombo vya Habari Ofisini kwake Kisiwandui Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...