Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga (katikati) akizungumza wakati akitoa ufafanuzi wa virufushi vipya vya Mfuko huo, katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari nchini, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kisenga, LAPF Tower, jijini Dar es salaam leo. 
Sehemu ya Wafariri wa vyombo mbalimbali vya habari, wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga alipokuwa akitoa ufafanuzi wa virufushi vipya vya Mfuko huo na mchanganuo wake, katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kisenga, LAPF Tower, jijini Dar es salaam leo. 

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewahamasisha Watanzania kujiunga kwenye vifurushi vya mfuko huo ambavyo vimetangazwa hivi karibuni ili kujihakikishia kupata matibabu kwa gharama nafuu ukilingana na kupata matibabu nje ya mfumo wa bima ambayo ni gharama kubwa.

Pia mfuko huo umetumia nafasi hiyo kueleza wazi kuwa , mfuko uko imara kiuchumi na haujatetereka kama baadhi ya watu wanavyopotosha kwa umma huku ukisisitiza kwa sasa umejikita kuzungumzia faida za kujiunga na mfuko huo kupitia vifurushi hivyo vipya ambavyo sasa kila anayehitaji atakuwa na nafasi ya kuchagua kifurushi cha aina gani.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Desemba 2, 2019 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga ameeleza kuwa badala ya watu kuendelea kubishana kuhusu vifurushi hivyo ni vema wakatumia muda huu kujiunga navyo kwani vinafaida kubwa.

Amesema kabla ya kuzindua rasmi vifurushi hivyo vipya ,  NHIF walifanya utafiti na kujiridhisha na vifurushi hivyo na kubaini Watanzania wengi wanahitaji na hivyo mfuko huo umejiandaa vya kutosha."Tulitarajia badala ya watu kulaumu vifurushi hivi ambavyo tumevitangaza wangefuhia.Ukweli tulichelewa na hatuna sababu ya kuendelea kuchelewa.Tunaomba wananchi wajiunge na vifurushi vya mfuko wetu."

Ameongeza kuwa kwa bahati mbaya baadhi ya hao ambao wanatoa kauli za upotoshaji kuhusu vifurushi hivyo wao wanatumia bima za afya katika kupata matibabu, na sasa wanachokifanya ni kuzuia wengine wasinufaike na uwepo wa mfuko huo.

Amefafanua kuwa kwa sasa waliojiunga na NHIF ni asilimia nane ya Watanzania , huku asilimia 25 wakiwa katika CHF na asilimia moja ndio waliojiunga na bima ya afya katika sekta binafsi, hivyo kuna kundi kubwa la wananchi ambalo halijajiunga na bima za afya na hilo ndilo ambalo wameliangalia na kuona kuna kila sababu ya kuhakikisha nao wanapata nafasi ya kunufaika na mfuko huo kwa kuanzisha vifurushi hivyo.

Amesema katika kuhakikisha wengi wanajiunga na vifurushi hivyo wamegawa katika makundi matatu ambayo kundi la kwanza ni Najali Afya, kund la pili ni Wekeza Afya na kundi la Tatu ni Timiza Afya. "Hivyo mtu mmoja mmoja, wawili au familia wanaweza kuchagua moja ya vifurushi hivyo na kujiunga kulingana na mahitaji.

Kuhusu uimara wa mfuko, Mkurugenzi Mkuu amefafanua wamekuwa na utaratibu wa kufanya tathimini kila baada ya miaka mitatu na tathimi ya mwisho ya mfuko imeonesha una uwezo wa kuhumia wanachama wake hadi mwaka 2024 bila kukusanya michango na iwapo watahusisha na mali walizonazo wanao uwezo wa kutoa huduma mpaka mwaka 2029.

 Akizungumzia umuhimu wa kujiunga na bima ya afya, amesema moja ni kuwa na uhakika wa matibabu huku akieleza magonjwa ambayo si ya kuambukiza yamekuwa yakitumia gharama kubwa katika tiba, na hivyo kwa anayejiunga anakuwa na unafuu kwani wanachama wenye afya imara fedha zao zinatumika kusaidia wanachama wenye kusumbuliwa na maradhi.

Ametoa mfano kuwa matibabu ya ugonjwa wa kansa kwa mwaka ni Sh.milioni 66.9 wakati kusafisha figo kwa mwaka ni bajeti yake ni Sh.milioni 35 na matibabu ya moyo ni Sh.milioni 12 ambazo kwa mtu hajajiunga inakuwa ngumu kumudu ukilinganisha na aliyejiunga na mfuko huo.


Hata hivyo amesema lengo la mfuko huo angalau kuwa na asilimia 20 ya Watanzania ambao watakuwa wamejiunga na mfuko huo katika kipindi kifupi kijacho na kuongeza iwapo wengi watajiunga itakuwa rahisi hata sheria ya bima ya afya inapokuja kukuta tayari wengi  wanatumia bima katika matibabu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...