Daraja la reli ambalo linatumika kupitisha shehena ya mizigo inayopakiwa katika behewa na kisha moja kwa moja kuingizwa ndani ya meli. Daraja hilo la reli ambalo lipo katika Bandari ya Kemondo Bay ambayo kwa sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imeamua kuiboresha na siku za karibuni itaanza kutoa huduma.


Muonekano wa reli inayokwenda bandari ya Kemondo Bay ambayo ni maalumu kwa ajili ya kupitisha shehena ya mizigo inayosafirishwa kwa njia ya reli na kisha kupakiwa katika meli.
Meneja wa Bandari za Kanda ya Ziwa Morris Mchindiuza(kushoto) akielezea hatua mbalimbali za uboreshaji wa miundombinu katika bandari ya Kemondo Bay iliyoko mkoani Kagera.
Sehemu ya muonekano wa dara la reli katika bandari ya Kemondo Bay.TPA imeamua kuboresha reli hiyo inayoingia katika meli ili kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Kagera wanakuwa na uhakika wa kusafirisha mizigo yao kutoka sehemu moja kwenda nyingine.



Said Mwishehe-Michuzi TV

WAFANYABISHARA mbalimbali nchini na hasa wa Mkoa wa Kagera wameshauriwa kutumia usafiri wa meli na reli katika kusafrisha shehena za mizigo ikiwemo inayotokea Bandari ya Dar es Salaam kwani gharama za usafiishaji ziko chini ikilinganisha na usafiri wa malori.

Kauli hiyo imetolewa kipindi ambacho Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) kuwa na mpango mkakati wa kuendelea kuboresha miundombinu ya bandari katika maziwa makuu ambapo miradi mbalimbali imekamilika na mingine utekelezaji unaendelea.

Kutokana na uboreshaji huo wa miundombinu ya bandari, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini imetumia nafasi hiyo kutoa ujumbe kwa wafanyabishara kutumia bandari zilizopo nchini ikiwemo ya Bandari ya Kemondo Bay ambayo sasa iko tayari kufanyakazi kwa namna ile ile iliyokuwa iliyokuwapo miaka ya nyuma.

Akizungumza zaidi ,Meneja wa Bandari za Kanda ya Ziwa Morris Mchindiuza amewaambia waandishi wa habari waliopo kwenye ziara ya kutembelea na kushuhudia utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya bandari kuwa TPA katika Bandari ya Kemondo ambayo ni maarufu kwa meli za kubeba mizigo kuwa sasa imekamilika na hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara kuitumia kusafirisha shehena za mizigo ya aina mbalimbali.

"Mwito wetu kwa wafanyabishara wa Mkoa wa Kagera na mikoa mingine nchini waendelee kutumia bandari hii ya Kemondo kusafirisha mizigo yao.Ukweli kusafirisha mizigo kwa njia ya meli na reli ni salama na nafuu zaidi ukilinganisha na aina nyingine ya usafiri, ndio maana TPA tumeamua kuboresha miundombinu ya bandazi zetu ili kutoa huduma ya uhakika wakati wote,"amesema Mchindiuza.

Kuhusu bandari hiyo , amesema ilijengwa mwaka 1971 na kukamilika mwaka 1974 na kwamba lengo la bandari hiyo kwa wakati huo lilikuwa zaidi kusafirisha shehena za mizigo mbalimbali na hasa zao kuu lilikuwa kahawa lakini pia ilikuwa inahudumia abiria. Bandari ya Kemondo Bay ilikuwa ni kituo kikubwa cha kubeba mizigo ikiwamo mihogo, ndizi na maparachichi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa wingi kutoka katika eneo hilo.

"Pia mizigo yote iliyokuwa ikitolewa mkoani Mwanza kama vifaa vya ujenzi ikiwamo saruji pamoja na nondo Ilikuwa ikifikishwa hapa na baadaye kutawanywa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera pamoja na vitongoji vyake. Kwa takribani miaka 15 iliyopita Bandari ya Kemondo Bay ilikuwa inakwenda kwa kusimama na kusuasua na baadaye tukajikuta hatuna oparesheni zozote zinazofanyika kwenye hili,"amesema.

Ameongeza kuwa bandari hiyo ina sehemu mbili, kuna sehemu ya mwalo ambayo ipo pembeni pamoja na sehemu ya Bandari kuu na kwamba katika eneo hilo zilikuwa zinafunga meli kubwa kabisa lakini baada ya mdororo uliotokea meli kubwa nazo zikawa hazifiki.
 
"Katika eneo hili bado kukawa na mahitaji ya watu wanapokwenda visiwani na hivyo kukawa na boti ndogondogo ambazo zilikuwa pembeni mwa bandari. Mamlaka baada ya kuona uhitaji na pia ya hizi boti ndogondogo tukajenga eneo la uwezeshaji katika eneo hilo la pembeni ambapo tumejenga gati ndogo zinazoweza kuhimili boti ndogo kutia nanga.

"Katika kipindi ambacho huduma imesimama kwenye eneo hili Bandari ya Kemondo kule upande wa mwalo huduma zikawa zinaendelea kwa kuwa kuna boti ambazo zinatoka huduma katika visiwa kwenye eneo hili. Kwa kifupi baada ya TPA kuona hali hii inaendelea tukasema hapana, hivyo tumeamua kuboresha miundombinu ikiwemo ya kufufua njia ya reli inayoingia bandarini pamoja na daraja la reli,"amesema.

Amesema kuwa reli hizo zilikuwa zimefukiwa kabisa na kutoonekana lakini uboreshaji wa miundombinu katika bandari ya Kemondo sasa reli zinapitika vizuri na hivyo mizigo ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo itaweza kupitishwa katika bandari hiyo.

"Shilingi milioni 815 zilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo ambayo ilianza wiki tatu zilizopita na sasa iko mwishoni kumalizika na bandari kuanza rasmi kutoa huduma ya kusafirisha mizigo.Tuna imani kubwa bandari hii itakuwa ni kichocheo cha ajira katika eneo letu hili.Pia itamuwezesha mwananchi wa kipato cha chini wakiwemo wakulima kusafirisha ndizi na parachichi zao bila tatizo,"amesema.

Kuhusu matarajio yao, amesema bandari hiyo itaanza kazi kabla ya mwisho wa Desemba mwaka huu na tayari wanaye mteja ambaye wamekuwa wakifanya naye kazi tangu awali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...