Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kulia) akimsikiliza mmoja wa akina mama wa Kijiji cha Nyantimba, wilayani Chato mkoani Geita, baadaya kuwasha umeme katika kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akipokea zawadi kutoka katika kikundi cha kimama wa kijiji cha Nyantimba wilayani Chato mkoani Geita, ikiwa ni zawadi yao kwa waziri huyo baada ya kufika kijijini hapo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(katikati) akikata utepe kuashiria kuwasha umeme katika kijiji cha Kanyindo wilayani Chato mkoani Geita.

*********************************

Na Zuena Msuya, Chato

Waziri wa Nishati, Dkt. Medadrd Kalemani amesema mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kwa sasa zimesababisha baadhi ya maeneo kukatika umeme mara kwa mara ama kukosa huduma huyo.

Dkt. Kalemani alitoa kauli hiyo, katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, wakati ziara yake ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini, ambapo pamoja na mambo mengine aliwasha umeme katika Vijiji vyaNyantimba na Kanyindo katika wilaya hiyo, Januari 22,2020.

Alisema kuwa mvua zinazonyesha zimeambatana na upepo mkali ambao husababisha baadhi ya miundombinu ya umeme kuangua na nyaya kuungua moto kutokana na kugusana, hivyo kusababisha hitilafu na maeneo mengi kukosa huduma ya umeme, akitolea mfano maeneo ya Jiji
la Dar Es Salaam na Mkoa wa Morogoro.

Dkt. Kalemani, alisema umeme unaozalishwa nchi kwa sasa ni mwingi na wa kutosha kukidhi mahitaji ya nchi na ziada, hivyo tatizo la kukatika kwa umeme ama kukosekana kwa huduma hiyo hakumaniishi kwamba umeme unaozalishwa hautoshi la hasha.

Sambasamba na hilo alisema kuwa, kutokana na hali hiyo wakati mwingine mafundi wanalazimika kuzima umeme katika baadhi ya maeneo ili kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibika.
“Hizi mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini zinasababisha nguzo kuanguka,nyaya kugusana na nyaya zikigusana zinaungua na kusababisha umeme kukatika katika baadhi ya maeneo,siyo kwamba umeme hautoshihapana, umeme upo mwingi na wakutosha mahitaji yetu”, alisema Dkt. Kalemani.

Aliwataka wananchi kuwa wavumilivu na kuvuta subira pamoja na kutoa ushirikiano kwa sekta husika wakati Serikali inaendelea kukarabati na kuimarisha miundombinu ya umeme nchi nzima ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

Akizungumzia suala la usambazaji wa umeme vijijini, Dkt. Kalemani alitoa mwezi mmoja kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)kuwaunganishia umeme wananchi wote wa Kata ya Nyalutembo wilayani Chato mkoani Geita waliopo katika mpango wa kuunganishiwa umeme na ambao wamekwisha lipia.

Kata hiyo ya Nyalutembo yenye vijiji vinne ambavyo baadhi ya wakazi wake wamelipia huduma ya umeme lakini mpaka sasa bado hawajaunganishwa kutokana na sababu mbalimbali.

Aidha aliwataka wananchi hao, kulipia shilingi 27,000 tu, ili kuunganishiwa umeme, pia wasikubali kutozwa gharama za nguzo, LUKU wala nyaya kwakuwa gharama hizo tayari zimelipwa na serikali.
Kata hiyo inaunganishiwa umeme na TANESCO, ikiwa ni mpango wa wake wa kusambaza umeme vijijini kwa gharama nafuu kama ilivyo kwa Wakala
wa Nishati Vijijini (REA).

Wakazi wa maeneo hayo walitakiwa kuongeza kasi kulipia huduma hiyo na kutandaza nyaya katika nyumba zao, hata kama miundombinu imepita mbali na makazi yao na kwamba wasisubiri nguzo ziwafikie kwa kuwalengo la serikali ni kuwafikishia umeme wananchi wote katika nyumba zao na kwa bei nafuu.

“Wananchi nawasisitiza kulipia gharama, na kutandaza nyaya katika nyumba zenu, msisubiri nguzo hii siyo kazi yenu, ni kazi ya serikali kuwaleta nguzo katika maeneo yenu, sasa nyie changamkieni fursa na muwe tayari ili siku mkifikiwa iwe rahisi na haraka kuunganishiwa”,
alisisitiza Dkt. Kalemani.

Aliwaeleza wanakijiji hao kuwa, watumie umeme huo kwa manufaa na kujiletea maendeleo kwa kuanzisha viwanda vidogo na biashara mbalimbali zenye kuinua vipato vyao tofauti na ilivyokuwa kabla ya kupataumeme.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...