Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimuonesha Mkuu wa wilaya ya
Uvinza mkoa wa Kigoma Mwanamvua Mrindoko jinsi Majalada ya Ardhi
yanavutunzwa katika halmashauri ya wilaya yake bila kufuata taratibu
wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika
mkoa wa Kigoma jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Afisa Ardhi wa
Halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma Manyama Makongo kuhusiana
na changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo jana
wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa
wa Kigoma.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoa maelekezo kwa Mkuu wa
wilaya ya Mpanda Lilian Matinga (wa pili kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa
halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Enelia Lutunguru baada ya kutoka
kukagua Masijala ya Ardhi ya Manispaa ya Mpanda jana wakati wa ziara
yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Katavi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na Mkuu wa wilaya
ya Mpanda Lilian Matinga alipowasili katika mkoa wa Katavi jana kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Katavi. Kushoto ni Mkuu
wa Mkoa wa Katavi Juma Homera.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya
Tanganyika mkoa wa Katavi Salehe Mhando alipoitembelea wilaya hiyo jana
akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi
katika mkoa wa Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera
akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula jana wakati Naibu Waziri alipofanya ziara ya
kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Katavi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akichomoa moja ya Majalada ya
Ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Mpanda jana akiwa katika ziara
yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa
Katavi. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
………………
Na Munir Shemweta, WANMM UVINZA
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameijia juu
halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma kwa kushindwa kuihudumia
idara ya ardhi na kusababisha watumishi wa idara hiyo kugharamia baadhi
ya vifaa ili kutekeleza majukumu yao.
Hali hiyo
ilibainika jana katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwa katika ziara yake ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa kigoma.
Akiwa katika
Masijala ya Ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Uvinza, Dkt Mabula
alibaini utunzaji majalada ya ardhi usiofuata taratibu huku baadhi ya
hati zikiwa hazijakamilishwa kwa ajili ya kuwapatia wamiliki wa ardhi
katika halmashauri hiyo tangu mwaka 2018.
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwajia juu watumishi wa sekta ya
ardhi katika halmashauri hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo
jambo alilolieleza kuwa linachangia uwepo migogoro ya ardhi sambamba na
kuwanyima wananchi fursa ya kupata hati.
Dkt Mabula
aliagiza hati zote ambazo taratibu zake zishakamilishwa ikiwemo wamiliki
wake kusaini hati hizo kupelekwa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi
Kanda ya Magharibi ndani ya wiki moja kwa ajili ya kukamilishwa na
kupatiwa waombaji.
Hata hivyo, baada
ya kuwajia juu watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Uvinza
ndipo Afisa Ardhi wa halmashauri hiyo Manyama Makongo alipomueleza kuwa
idara hiyo inashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosa vifaa
jambo lililosababisha kuamua kuchukua ‘Printer’ yake binafsi na
kuipeleka kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya kusaidia kazi za idara.
Hali hiyo siyo tu
ilimshutua na kumshangaza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi bali ilimsononesha kwa kuona watumishi wa sekta ya ardhi katika
halmashauri hiyo wanatumia fedha zao za mifukoni kuendesha ofisi jambo
alilolieleza kuwa halikubaliki.
‘’Hapa jitihada
za ziada zinahitajika, halmashauri ipo inashindwa kuihudumia idara ya
ardhi, halafu watumishi wanatumia fedha zao za mfukoni hili halikubaliki
lazima niwasiliane na Waziri Jafo kuhusiana na suala hili’’ alisema Dkt
Mabula.
Kwa mujibu wa
Naibu Waziri Mabula, idara za ardhi katika halmashauri nyingi nchini
zimekuwa kama watoto wa kambo kutokana na wakurugenzi wa halmashauri
kutozitengea bajeti ya kutosha jambo linalofanya idara kufanya kazi
katika mazingira magumu.
Katika hatua
nyingine Mkuu wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi Lilian Matinga na Kaimu
Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Enelia Lutungulu
wamewaokoa Maafisa Ardhi wa halmashauri hiyo wasitumbuliwe kutokana na
kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kutokamilisha utoaji
wa hati za ardhi kwa muda mrefu.
Walionusurika ni
Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Spear Mwalukasa
ambaye ilielezwa yuko katika mafunzo na Afisa Ardhi Ezekiel Bichuro.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
alisema kutokana na Maafisa hao kuzembea kukamilisha hati kwa muda mrefu
basi hawafai kuendelea na nafasi zao kwa kuwa wanakwamisha utoaji hati
ambao sasa unaweza kufanyika ndani ya mwezi mmoja pale taratibu zote
zinapokuwa zimekamilika.
Hata hivyo, Mkuu
wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga na Kaimu Mkurugenzi Enelia Lutungulu
waliwatetea kwa kueleza kuwa maafisa hao hawana muda mrefu katika idara
hiyo na makosa yanaweza kuwa yalifanywa maafisa waliopita.
Naibu Waziri
Mabula alielekeza maafisa hao kupewa barua za onyo kwa kuwa muda wa
miezi mitatu waliopo katika idara hiyo wangeweza kuonesha jitihada za
kukamilisha hati na kuagiza hati zilizopo zikamilishwe katika kipindi
cha mwezi mmoja.
‘’Ikifika tarehe
30 Januari 2020 hati ziwe zimeenda kwa wenyewe, haiwezekani mtu amesaini
tangu 2015 halafu mpaka sasa hajapatiwa hati yake, wapo wazembe
wachache wanaochafua Wizara lazima wapewe warning. Alisema Naibu Waziri
Mabula.
Naibu Waziri
Mabula pia alitembelea wilaya ya Tanganyika ambapo alionesha kutoridhika
na kasi ya ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi na
kuagiza halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kuongeza kasi katika
makusanyo sambamba na kupanga, kupima na kumilikisha viwanja kwa
wananchi.
Kwa mujibu wa
Afisa Ardhi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Penina Simon kiasi
cha shilingi milioni 18,069,179.40 kilikusanywa hadi kufikia nusu ya
mwaka wa fedha 2019/2020.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...