Na woinde shizz, Arusha

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha imetoa miezi miwili kwa pande mbili za familia ya marehemu bilionea Erasto Msuya zenye mgogoro wa kugombea mali za marehemu kukaa meza moja ili kuondoa tofauti zao na kuleta mrejesho mahakamani hapo baada ya muda huo kupita.

Akitoa uamuzi huo leo Januari 28,2020 ,Jaji wa Mahakama hiyo anayesikiliza shauri hilo,Johannes Masara amesema kuwa mahakama hiyo imeridhia ombi la upande wa mleta maombi Ndeshukulwa Msuya la kuiomba mahakama hiyo kuondoa shauri lake la mirathi kwa muda ili familia hizo ziweze kukaa meza ya mazungumzo.

Amesema kuwa Mahakama baada ya kupokea ombi la mleta maombi imekubali pande hizo kuweza kukaa meza moja kupitia Mkuu wa wilaya ya Arumeru na imetoa miezi miwili kupata mrejesho.

Kesi hiyo ya Mirathi namba 66/2018 iliyopo ngazi ya rufaa mahakama kuu kanda ya Arusha ilifunguliwa na Ndeshukurwa Msuya mama wa marehemu bilionea Msuya akiiomba mahakama kumtengua Miriam Mrita mke wa marehemu kuwa msimamizi wa mirathi kutokana na kukabiluwa na kesi ya mauji ya WiFi yake iliyopelekea awe gerezani kwa muda mrefu na kushindwa kusimamia Mali za marehemu.

Akizungumza nje ya Mahakama Ndeshukurwa amesema kuwa uamuzi wa mahakama umetenda haki na umezingatia maslahi mapana ya pande zote mbili kwani anaamini jambo hilo linaenda kumalizika na watoto wa marehemu wataweza kupata haki yao ya msingi.

Amesema suala la maridhiano liliibuliwa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru,Jerry Muro na kuwataka ndugu hao waondoe kesi iliyopo mahakamani ili wakae mezamoja na kwamba angesaidia kusimamia meza ya mazungumzo ya famili hizo.

Hata hivyo upande wa wajibu maombi (Wajomba)hawakuwepo mahakamani hapo kwa madai kwamba wamefiwa na Dada yao mkubwa na kuwakilishwa na Mwanasheria wao Shilinde Ngalula.

Awali wakili wa upande wa wajibu maombi,Shilinde Ngalula,alipinga hatua ya mahakama hiyo kukubali ombi la kuondoa kesi hiyo kwa muda akiitaka mahakama iifute kabisa kesi hiyo na kusiwepo shauri hilo mahakamani wakati wa maridhiano nje ya mahakama.

Hata hivyo jaji Masara alikataa ombi hilo na kukubali ombi la upande wa waleta maombi la kuondoa kesi hiyo kwa muda bila kuifuta na kurejea meza ya mazungumzo na kwamba iwapo familia hizo hazitakubaliana watarejea mahakamani kuendelea na shauri hilo kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Ndeshukurwa anampinga Miriamu Mrita ambaye ni mke wa marehemu mwanaye kuwa msimamizi wa mirathi akidai kuwa ameshindwa kugawanya Mali za marehemu kwa wanufaika kwa kipindi cha miaka saba tangu kifo cha marehemu bilionea Msuya kilichotokea kwa kupigwa risasi zaidi ya 20 mwaka 2013 wilayani Hai ,mkoani Kilimanjaro.

Ndeshukurwa anadai kwamba Miriamu ambaye kimsingi ndiye msimamizi wa mirathi ,yupo gerezani mahabusu kwa muda mrefu akikabiliwa na kesi ya mauaji ya WiFi yake,hivyo hatua hiyo imepelekea baadhi ya Mali za marehemu kupotea huku watoto wa marehemu wakishindwa kupatiwa mgawanyo wa Mali hizo za marehemu baba yao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...