Na Magreth Kinabo- Mahakama
Mahakama ya Tanzania imeokoa kiasi cha fedha Shilingi milioni 129 baada ya kuendesha mashauri kwa njia ya Mtandao (‘Video Conference’).

Kati ya fedha hizo, Mahakama ya Rufani Tanzania, imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi Milioni 95 katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2019 baada ya kuendesha vikao maalum kwa njia ya mtandao wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeokoa Shilingi milioni 34 katika kipindi cha mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo wakati akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria na Siku ya Sheria nchini, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema katika kipindi cha mwaka jana, Mahakama ya Rufani iliendesha vikao hivyo ambavyo vilivyofanyika kwa njia ya video conferencing kwenye vituo vya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tabora na Bukoba.

Alisema jumla ya maombi 60 yalisikilizwa na Majaji 18 wa Mahakama hiyo, ambapo kila Jaji alipangiwa kusikiliza maombi kati ya mawili na sita.

‘Gharama ya zoezi zima la kutumia video Conferencing ilikuwa shilingi milioni 5 ambayo ilihusisha gharama za Internet, pamoja na usafiri wa watumishi kwa ajili ya kwenda kuratibu zoezi hilo. ‘Gharama hizo zilijumuisha pia kuwalipa Mawakili wa kujitegemea wanaotakiwa kuwawakilisha wafungwa walio magerezani kwa makosa ya mauaji’, alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu alisema Mahakama hiyo ingetumia utaratibu wa kawaida ungegharimu Shilingi milioni 100.

Prof, Juma alifafanua kwamba kutokana kutumika kwa njia hiyo, Majaji walibaki jijini Dar Salaam lakini waliweza kusikiliza maombi, na kisha kurudi maofisini kuendelea na shughuli zao zingine.

Jaji Mkuu alisema mfumo huo, umefungwa kwenye vituo sita vya Mahakama Kuu katika kanda za Dar es salaam, Mbeya, na Bukoba pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (Lushoto).

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Mahakama ya Tanzania, zinaonyesha kwamba upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania kesi zilizosikilizwa zinazohusu Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa njia hiyo kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Julai 8, mwaka jana ni 375, yaliyotolewa maamuzi ni 371 na zilizobakia ni nne.

Wakati huohuo, kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Bi. Kabunyanja ilisema kwamba Mahakama hiyo katika kipindi cha mwak jana iliendesha kesi sita, zikiwemo za Uhujumu Uchumi kwa njia ya video conference, kesi tano, mashahidi walikuwa nje ya nchi na moja shahidi akiwa nchini.

Hivyo gharama iliyotumika kwa kesi zote sita ni Shilingi milioni 1.4 , ambapo utaratibu wa kawaida ungetumia ungegharimu Shilingi milioni 34 hivyo njia hiyo imeokoa kiasi cha shilingi milioni 34.

Aidha Kabuyanja aliongeza pia kesi zilizosikilizwa kwa njia hiyo kati ya Mahakama hiyo na Gereza la Keko kuanzia Januari 13, mwaka huu hadi Januari 22 mwaka huu ni kesi 25.

Akizungumzia matumizi ya TEHAMA, Jaji Mkuu aliwataka wananchi watakaotembelea mabanda ya Mahakama wakati wa maonesho ya Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria wapate fursa ya kujifunza ni kwa kiasi gani Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa ufanisi kwa matumizi hayo.

Mifumo mingine ya TEHAMA inayofanya kazi katika Mahakama ya Tanzania ni Mfumo ya Kielekitroniki wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (JSDS2), ambao ulizinduliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Februari 6, mwaka jana. 2019.

‘Itakuwa faida kubwa kwao endapo wananchi wataelewa utaratibu wa kufungua shauri kielekitroniki, kupokea wito kuhudhuria shaurini na hata kupata taarifa za shauri kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu,’ alisisitiza Jaji Mkuu.

Alitaja mifumo mingine inayotumiwa na Mahakama kuwa ni wa ramani ambao unaonesha Mahakama za ngazi zote, na taarifa za kila Mahakama na hali ya kila jengo la Mahakama nchini (Judiciary Map—JMAP). Mingine ni ule wa kuwatambua Mawakili wenye leseni wanaotoa huduma za Uwakili (TAMS) na majina ya Madalali wenye leseni hai.

Alisema mfumo mwingine ni ule wa kuhifadhi Hukumu za Mahakama (TANZLII), ambapo kupitia mfumo huo, hukumu 1,523 za Mahakama ya Rufani ziliwekwa hadi kufikia Disemba 13, 2019. Hukumu (maamuzi) za Mahakama za Mahakama Kuu Masjala Kuu na kanda za Mahakama Kuu yalikuwa mashauri 1,297, wakati Mahakama Kuu—Divisheni ya Ardhi mashauri yalikuwa 433, Mahakama Kuu—Divisheni ya Biashara 238, Mahakama Kuu—Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,72 na Mahakama Kuu—Divisheni ya Kazi 76. 
Jaji Mkuu wa Tanzania, prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu na Siku ya Sheria nchini itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. Mkutano huo imefanyika leo Januari 27, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mahakama ya Rufani Tanzania. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwaonyesha waandishi wa habari kitabu cha Mwongozo wa Utumiaji wa Huduma za Mahakama, ambapo taratibu zimewekwa kwa lugha nyepesi ili kumwezesha mwananchi kuelewa kwa urahisi. Katika mkutano huo Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu na Siku ya Sheria itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Eddie Fussi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...