Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewataka  Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na wadhamini wao kufika mahakamani hapo na kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana kutokana na  kuvuka mipaka ya Tanzania bila kupata kibali cha mahakama na wadhamini wa wabunge hao kujieleza ni kwanini wasiondolewe kuwadhamini washitakiwa hao.

Amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas  Simba leo Januari 20,2020 kufuatia Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kuomba mahakama iwafutie dhamana washitakiwa hao kwa kukiuka masharti ya dhamana na kusafiri nje ya nchi bila kupata kibali.

Kabla ya kutolewa ombi hilo, mahakama iliwataka washitakiwa hao kujieleza kama kweli walisafiri nje ya nchi ambapo Mdee alikiri kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu na kwamba hospitali ya Agakhan iliandika barua kumtaka akafanyiwe matibabu na yeye aliiwasilisha kwa mawakili.

Alidai kuwa, Bulaya alimsindikiza kwenda nchini Afrika Kusini kwa sababu mazingira ya ugonjwa wake hayakumruhusu kusafiri pele yake huku Bulaya yeye akidai kuwa alikuwa na ruhusa ya mahakama kutokana na barua ya Agakhan ikimtaka kumsindikiza Mdee.

Baada ya maelezo hayo, Nchimbi alidai kutokana na uchunguzi wao wadhamini kuwa washtakiwa hao walisafiri bila kibali cha mahakama na kwamba wenye jukumu la kuomba ruhusa ya kusafiri si hospitali bali ni washitakiwa wenyewe na nyaraka za hospitali zinaambatanishwa kwenye maombi kama uthibitisho

Alidai Januari 13,2020 Wakili Hekima Mwasipu aliandika barua na  kwamba alipewa nafasi ya kuwasilisha hoja za wateja wake ambapo yeye alidai wateja wake wanaomba ruhusa ya kwenda nchini Kenya kwa ajili ya mkutano wa ndani wa chama na sio maombi ya kwenda nchini Afrika Kusini.

" Bulaya na Mdee walisafiri nje ya nchi bila kupata kibali cha mahakama kama masharti yanavyowataka, hivyo mahakama ikiona maombi hayo yanamsingi, iwaite na waeleze kwanini dhamana yao isifutwe kwa kuruka dhamana pia iwahoji wadhamini wao," amedai Nchimbi.

Novemba 20, mwaka jana mahakama iliwapa onyo kali  wabunge hao pamoja na  Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa kwamba  wakikiuka tena masharti ya dhamana watafutiwa.

Hakimu Simba alisema licha ya kwamba hakuridhika na maelezo yaliyotolewa na washitakiwa lakini hatua ya kuwafutia dhamana ni kali sana na hataki kufanya hivyo anataka kesi isikilizwe na iishe kwa wakati.

Novemba 15, 2019 mahakama hiyo  iliamuru wabunge hao wanne wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo kutokana na kukiuka masharti ya dhamana ambapo amri ya kukamatwa kwa wabunge hao ilitolewa  baada ya wabunge hao kutofika mahakamani hapo wakati kesi yao ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa bila kutoa taarifa yoyote na wadhamini wao pia kutokuwepo.

Mwaka 2018, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko walifutiwa dhamana na kukaa mahabusu kwa miezi mitatu baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Mbali na Bulaya na Mdee, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu,   Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Dk Vincent Mashinji.

Katika Kesi hiyo Mbowe na wenzake wanakabiliwa na  mashitaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari Mosi na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...