Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Watumishi wa sekta ya ardhi wa Halmashauri nne za mkoa wa Rukwa (Hawapo pichani) jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Rukwa. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Khalfan Haule na kushoto ni Kamishna Msaidzi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Thadei Kabonge.
Watumishi wa sekta ya ardhi katika Halmashauri nne za mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Rukwa jana

(PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

………………

Na Munir Shemweta, WANMM RUKWA

Makusanyo ya kodi ya pango la ardhi katika halmashauri za mkoa wa Rukwa yamemvuruga Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula baada ya kuelezwa kuwa hadi kufikia Desemba 2019 jumla ya shilingi milioni 148.2 zilikusanywa na halmashauri zote nne sawa na asilimia 7.9 .

Akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Rukwa jana ambapo alikutana na watumishi wa sekta ya ardhi, Dkt Mabula alishangazwa na namna maafisa ardhi wa halmashauri hizo wasivyofuatilia makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kiasi cha kuzifanya halmashauri hizo kukusanya kiasi kidogo cha fedha.

Alisema, haiwezekani ndani ya miezi sita halmashauri nne za mkoa wa Rukwa zikusanye asilimia 7.9 ya kodi ya pango la ardhi jambo alilolieleza kuwa linatia mashaka kama halmashauri hizo zitaweza kufikisha hata asilimia hamsini ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kwa mujibu wa Taarifa ya mkoa wa Rukwa iliyosomwa na Mrasimu Ramani wa mkoa wa Rukwa Kelvin Maungi, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri za mkoa huo zilikadiriwa kukusanya jumla ya sh 1,880,000,000.00 ambapo Manispaa ya Sumbawanga ilikusanya kiasi cha sh. 94,253,273.00, Halmashauri ya wilaya ya Nkasi sh. 16,494,189.00, Kalambo sh 1,793,550.00 na Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga sh 35,680,575.00 na hadi hadi Desemba 2019 jumla ya shilingi 148,221,587.00 zilikusanywa kwa halmashauri zote sawa na asilimia 7.9.

‘’Wakurugenzi wako busy na masuala mengine, mkoa mzima una silimia 7.9 ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi! ni aibu na hamuwezi kufikia asilimia 50 ya makusanyo naagiza wote mkafanye uhakiki wa wadaiwa wa kodi ya ardhi na muwapelekee ilani ili watakaokaidi wafikishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi’’ alisema Dkt Mabula.

Aidha, Naibu Waziri Mabula aliagiza kufikia Machi 2020 lazima kuwe na mabadiliko ya utendaji kazi kwenye sekta ya ardhi kwa halmashauri za mkoa wa Rukwa, vinginevyo atafikiria kama wakuu wa idara wanatosha kuendelea na nafasi zao na kusisitiza kama ni Mkuu wa Idara au Afisa Ardhi Mteule ataondolewa.

Dkt Mabula alisema mikoa yote aliyoitembelea kwenye ziara zake za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi imefikisha asilimia thelathini ya makusanyo ya kodi ya ardhi lakini mkoa wa Rukwa umemsononesha sana na kumuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda Thadei Kabonge atoe maelezo kuhusiana na utendaji kazi wa Wakuu wa idara kama wanafaa kushika nafasi zao.

Hata hivyo, Naibu Waziri Mabula alibainisha kuwa kulingana na taarifa zilizokuwa kwenye mfumo wa kielektronik Manispaa ya Sumbawanga ilitakuwa kukusanya Bilioni 6.7, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga milioni 20, Kalambo milioni 1.6 na Nkasi milioni 16 hiyo inatokana na halmashauri hizo kuwa na malimbikizo ya wadaiwa kodi ya pango la ardhi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...