Na Karama Kenyunko, globu ya jamii.

MKURUGENZI,  wa Kampuni ya Jaluma General Supplies Limited,  Lucas Mallya (42) na wenzake nane wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka 28 ikiwemo ya kukwepa kodi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 31.57.

Mbali na Mallya washitakiwa wengine ni Emmanuel Peter  (25), Mkurugenzi wa Happy Imports Assosiates, Happy Mwamugunda, Prochesi Shayo, Prokolini  Shayo (49), Godfrey Urio, Nyasulu Nkyapi, Tunsubilege Mateni na Nelson Kahangwa

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa leo Januari 28, 2020 na  wakili wa Serikali,  Faraja Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, mfawidhi, Godfrey Isaya, imedaiwa  kati ya Januari Mosi, 2015 na Januari 7, 2020 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa walitenda makosa ya kuongoza genge la uhalifu.

Imedaiwa kuwa, Juni 3 mwaka jana, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Mallya akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Jeluma General Supplies Limited, alitengeneza nyaraka za kodi za kielektroniki ikionesha imetengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia Juni 3,2019, Mallya aliwasilisha hati ya kughushi kuonesha kuwa stempu za ushuru za  kielektroniki  ni halisi wakati wakijua si kweli.

Kayika shtaka jingine imedaiwa Januari 7, mwaka huu  huko Chang'ombe wilayani Temeke,  Mallya alipatikana na rola 93 za stempu za ushuru za kielektroniki zenye thamani ya Sh 80,516,000 zilizochapishwa bila mamlaka ya Kamishna wa kodi.

Aidha imedaiwa Januari Mosi 2016 na Desemba Mosi 2019, kwa makusudi mshitakiwa huyo alitengeneza stempu za ushuru za kughushi na kuisababishia serikali hasara ya Sh 15,241,075,169 huku ikidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi 2016 na Desemba 31, mwaka jana , Mallya alitengeneza stempu za kodi rola 93 na kukwepa kodi ya  Sh 15,241,075,169.

Pia inadaiwa Mallya alijipatia  Sh 15,241,075,169 huku akijua kuwa fedha hizo ni mazalia ya makosa ya kukwepa kodi.

Pia wakili wa Serikali, Zacharia Ndaskoi, alidai Januari 3, mwaka huu maeneo ya Mbezi Makabe, Peter alikutwa ha rola nne za stempu za ushuru zenye thamani ya Sh 1,104,000 zilizochapishwa bila kibali cha Kamishna wa kodi huku mshtakiwa Mwamugunda akidaiwa Januari 3, mwaka huu akiwa Mkurugenzi wa kampuni  ya Happy Imports Associates bila kusajiliwa na Kamishna, aliingiza katoni 413 za bidhaa inayoitwa Drostay Hof Wine  zenye thamani ya Sh 24,780,000.

Mwamugunda anadaiwa pia kukwepa kodi ya Sh 9,584,401,393  baada ya kuingiza katoni hizo za bidhaa za vilevi na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha baada ya kushindwa kulipa kodi pamoja na kutakatisha fedha hizo.

Aidha, mshtakiwa Proches na Prokolini wanadaiwa Desemba 19, mwaka jana hukoTabata, walisambaza bidhaa zilizowekwa  stempu za kughushi ambazo ni katoni 749 za Robertson Wine 75CL zenye thamani ya Sh 98,670,000, Drostdy Hof 37.5CL katoni 594 zenye thamani ya Sh 12,002,000, Four Cousins 75 CL katoni 14 zenye thamani ya 16,240,000 na Amarula 75 CL katoni 58 zenye thamani ya Sh 12,120,000 zote zikiwa na thamani ya 139,032,000 bila kufuata kanuni za uwekaji stempu.

Pia washitakiwa hao wanadaiwa kushindwa kulipa kodi ya Sh 38,827,267, na ya Sh 2,359,342,542.07 pamoja na kuisababishia serikali hasara ya fedha hizo kwa kusambaza bidhaa zilizowekwa stempu za kughushi.

Mshtakiwa Urio anadaiwa kuwa akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya GMU  Group  Limited kati ya Januari Mosi 2015 na Desemba 31,2018 kwa nia ya kukwepa kodi aliwasilisha taarifa za uongo TRA na kukwepa kulipa kodi ya Sh 4,265,882,773 na kwamba aliisababishia serikali hasara hiyo na kutakatisha fedha hizo ikiwa ni zao la kukwepa kodi.

Aidha, washtakiwa Mateni na Kahangwa wanadaiwa Januari Mosi 2015 na Desemba 31, 2018 huko Mbezi Africana wakiwa Mhasibu na Mkaguzi wa Hesabu walitengeneza taarifa za uongo za mapato za Kampuni ya GMU Group Limited kwa mwaka 2015, 2016 na 2017 kwa nia ya kupata faida.

Pia wanadaiwa walimsaidia Urio kuandaa taarifa za fedha za Kampuni hiyo kwa mwaka 2015,2016 na 2017 kwa lengo la kujipatia faida na kwamba walimsaidia Urio kujipatia Sh 4,265,882,773 wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kukwepa kodi.

Mshtakiwa Nkyapi anadaiwa alishindwa kulipa kodi ya Sh 89,673,373 na kushindwa kutoa risiti za kielektroniki baada ya kupokea malipo ya Sh 98,670,000 ya Prochesi na Prokolini kwa mauzo ya katoni 759 ya Robertson Wine 75 CL.

Pia anadaiwa aliingiza bidhaa za vinywaji vikali zenye thamani ya Sh 95,100,297 bila kusajiliwa na kuisababishia hasara ya Sh 89,673,373  kwa kuingiza bidhaa ambazo hazijasajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na kutakatisha fedha.

Hata hivyo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Fabruari 12, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote wamerudishwa rumande.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...