Na Teresia Mhagama,
Imeelezwa kuwa, Mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu  mzunguko wa Pili, (Turnkey Phase III-Round II) utaanza kutekelezwa mwezi Februari, 2020 ambao utakamilisha lengo la Serikali la kupeleka umeme katika vijiji 12,268 ifikapo mwaka 2021.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya  Bunge ya Nishati na Madini kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi  ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu mwaka  wa fedha 2019/2020.

Katika kikao hicho aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, Menejimenti ya Wizara pamoja  Wenyeviti wa Bodi na Menejimenti za Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Dkt.Kalemani alisema kuwa, mradi huo utasambaza  umeme katika vijiji  1,822 ambavyo havikuwepo katika mradi  usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

Akitoa takwimu za usambazaji umeme vijijini, Dkt Kalemani alisema kuwa hadi kufikia mwezi Disemba 2015, jumla ya vijiji 2,018 vilikuwa na umeme na hadi kufikia Januari 10, 2020 jumla ya vijiji  8,408 vimepatiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 69.

Vilevile, alisema kuwa kutokana na miradi mbalimbali ya usambazaji umeme vijijini inayoendelea, inatarajiwa kuwa, kufikia mwezi Juni mwaka 2020, jumla ya vijiji 10,446 vitakuwa vimesambaziwa umeme.

Aidha, kuhusu wakandarasi wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, alisema kuwa, tayari wameshaandikiwa barua za kusudio la kusitisha mkataba na kampuni hizo zimepewa siku 60 za kurekebisha mapungufu la sivyo hatua zaidi za kimkataba zitachukuliwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, aliieleza Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme vijijini ukiwemo wa kusambaza nishati jadidifu katika maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa pamoja na visiwa.

Kuhusu mradi huo, alisema kuwa, Serikali kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini kwa kushirikiana na Serikali za Sweden na Uingereza umetoa ruzuku kwa kampuni binafsi 14 ili kuvipatia umeme vijiji 119 kutokana na vyanzo vya nishati jadidifu ambapo vijiji 95 vimepelekewa umeme.

Kuhusu kupeleka umeme visiwani, Maganga alisema kuwa, jumla ya visiwa 22 kati ya 196 vimesambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu na kwamba visiwa vyote vitasambaziwa umeme ifikapo mwaka 2021.

Aidha, kuhusu suala la usambazaji umeme kwenye Taasisi za umma, alisema kuwa, hadi kufikia Disemba 2015 jumla ya Taasisi 4,036 ziliunganishiwa umeme na hadi kufikia Disemba 2019 jumla ya taasisi 11,070 zimesambaziwa umeme.

Katika kikao hicho, Kamati ya Bunge iliipongeza Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo wa Julius Nyerere (MW 2115), aidha Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni mbalimbali yatakayoboresha Sekta ya Nishati nchini.
 Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya  Bunge ya Nishati na Madini kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi  ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu mwaka  wa fedha 2019/2020. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kushoto kwake ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja.
 Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika kikao na Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilicholenga kujadili kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi  ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu mwaka  wa fedha 2019/2020.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula akizungumza jambo katika kikao kati ya Kamati hiyo  na Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilicholenga kujadili kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi  ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu mwaka  wa fedha 2019/2020. Kushoto kwake ni Katibu wa Kamati hiyo, Felister Mgonja.
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiwa katika kikao na  Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani) kilichohusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi  ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu mwaka  wa fedha 2019/2020.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...