Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Joachim Wangabo ametoa siku tano kwa wazazi kuwaandikisha watoto waliofikisha umri wa kuanza shule pamoja na kuwafikisha shuleni wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambao kwa mwaka 2020 wanafunzi 16,062 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika mkoa lakini hadi kufikia tarehe 24.1.2020 ni wanafunzi 11,149 pekee wameripoti ambao ni sawa na asilimia 69.41.

Aidha, katika kuhakikisha asilimia 100 inafikiwa amewaagiza watendaji wa Kata na vijiji mkoani humo kuwakamata na kuwashitaki kwa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 wazazi wasiofanya hivyo na kuongeza kuwa sheria hiyo ya mtoto iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inatamka wazi haki ya mtoto ikiwemo haki ya kupata elimu na kwa mzazi kutofanya hivyo ni kosa na adhabu yake ni kulipishwa faini au kufungwa jela ama vyote viwili kwa pamoja.

“Mimi natoa siku tano za wiki hii kwa wazazi wote ambao wana watoto hawajaenda shule mpaka sasa hivi iwe ni wa darasa la kwanza, wawe ni “form one” (kidato cha kwanza) baada ya siku hizi tano wakamatwe wafikishwe mahakamani hatutaki mchezo kwenye elimu, huyu mtoto ukimchezea chezea hivi huyu huyu ndio atatusumbua, kwasababu akitoroka shule anakimbia yamesmshinda ndio huyo anakwenda mitaani, unadhani watoto wa mitaani wanatoka wapi si wameshindwa shule huku, si wazaqzi wameshindwa kuwalea, wakamatwe wazazi wanashindwa kuwalea watoto wao wafikishwe mahakamani, watendaji wa vijiji watendaji wa kata kamateni wazazi hao” Alisisitiza.

Ameyasema hayo leo tarehe 27.1.2020 katika kikao kazi kilichohudhuriwa na watendaji wa vijiji na kata za Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo walioongozwa na makamu Mwenyekiti wa halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga akianza ziara yake ya siku nne ya kukagua idadi ya wanafunzi walioripoti shule pamoja na mindombinu iliyopo. 

Mh. Wangabo amesema kuwa mkoa kufanya vibaya kwenye elimu kunachangiwa na kuchelewa kupeleka watoto shule na kuongeza kuwa endapo tathmini inafanyika kwa wale wanaofanya vibaya kwenye mitihani yao utagundua ni wale wanaochelewa  kufika shule na kutahadharisha kuwa  wanafunzi wa kidato cha kwanza wapo katika kipindi cha mabadiliko kutoka kwenye ufundishwaji wa Kiswahili kwenda kwenye ufundishwaji wa kiingereza hivyo ni muhimu kwao kuwahi shuleni.

“Anatoka mazingira ya shule ya msingi anaingia ya sekondari , inapaswa mwanafunzi wa “form one” aanze mapema hata kabla ya shule kufunguliwa ili aaanze kuzoea zoea yale mazingira lakini hajafika mapema, shule imefunguliwa hayupo, mwezi mzima unapita hayupo shuleni , huyu hata “form two” unategemea atafaulu kweli?” Alihoji.

Halikadhalika, Mh. Wangabo amewataka watendaji hao kushirikiana na wenyeviti wa vijiji kuitisha mikutano ya vijiji na kuwaelimisha wazazi  juu ya umuhimu kumuwahisha mtoto mapema shuleni huku wakiwabainishia faida na hasara za kutofanya hivyo na kuwaeleza juu ya umuhimu wa kusomesha watoto kwa maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni 4,394 huku walioripoti ni wanafunzi 2,973 ambao ni sawa na asilimia 67.7 huku wakihitaji madarasa 18 ambapo madarasa 15 tayari yamefikia usawa wa linta huku Mh Wangabo akitoa ahadi ya kuchangia mifuko ya saruji 150 ili kuwezesha kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto) akishiriki ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari Uchile iliyopo kata ya Kasanzama, Wilaya ya Sumbawanga wakati alipokwenda kutembelea kujionea miundombinu ya shule hiyo ilivyo pamoja na hali ya kuripoti kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (hawapo pichani)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...