Shirika la Under The Same Sun kwa kushirikiana na mashirika wenza GNRC NA CEFA wamezindua mradi wa “HAKI YETU” awamu ya pili, ambao umelenga kupunguza ama kutokomeza kabisa matukio ya kikatili ambayo wamekuwa wakifanyiwa watu wenye ualbino.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Januari 19, 2020 kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na viongozi wa dini, ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akimwakilisha mkuu wa mkoa Zainab Telack. 

Mboneko amesema Serikali inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili mradi huo ufanikiwe kwa asilimia 100, pamoja na kutoa elimu ya kupinga matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, kuwaimarishia ulinzi na usalama, kuwapatia hifadhi na elimu katika shule ya Buhangija Jumuishi, pamoja na kufanya msako kwa wale wote wanaotekeleza mauaji na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

 Amesema bado kuna maeneo mengi katika jamii hayajafikiwa na elimu juu ya uelewa kwa watu wenye ulbino, kwa kutambua hao ni sawa na binadamu wengine, ambacho kinachowatofautisha ni rangi, huku akiahidi Serikali pamoja na wadau watashirikiana kwa pamoja kusambaza elimu hiyo ambayo itapunguza ama kutokomeza matukio ya ukatili na ubaguzi kwa watu wenye ualbino.

 “Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili wa mauaji ya watu wenye ualbino, kuimarisha ulinzi na usalama, kuwapa hifadhi, kufanya msako kwa wale wote wanaotekeleza mauaji dhidi yao ama kupanga njama, pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria,”amesema Mboneko. 

“Kutokana na jitihada hizi za kupinga matukio ya ukatili kwa watu wenye ualbino, katika mkoa wetu kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni hakuna tukio lolote lililotolewa taarifa linalohusu mauaji ya watu wenye ualbino, hivyo natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga wasiwafanye ukatili  watu hawa pamoja na kuwabagua, “Natoa rai pia kwa wazazi na walezi kutowaficha watoto wenye ualbino, bali wawa patie haki zao kama walivyo watoto wengine, ikiwamo kuwapeleka shule, pamoja na kuwapenda,” ameeleza. 

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ameziagiza halmashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mahitaji maalum ya watu wenye ualbino, pamoja na maofisa maendeleo kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwaunga kwenye vikundi na kuwapa mikopo, ili wapate kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

 Naye meneja mradi wa ‘HAKI YETU’ kutoka Shirika la Under The Same Sun Wakyo Musongo, amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa mitano kwa kushirikiana na mashirika matatu ambayo ni Under The Same Sun, GNRC NA CEFA, mikoa ambayo ni Simiyu, Kigoma, Mwanza, Geita pamoja na Shinyanga.

 Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba mwaka 2019, na sasa wameuzindua katika awamu ya pili mkoani Shinyanga ambapo utakoma Juni mwaka 2021, na utatekelezwa katika halmashauri ya Ushetu pamoja na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo watakuwa wakitoa elimu ya kupinga matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. 

Aidha amesema katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya pili kupitia warsha, maonyesho ya sanaa sehemu za wazi, semina, na vyombo mbalimbali vya habari, wanatarajia kufikia watendaji wa serikali 450, viongozi wa dini 400, wanafunzi 30,000, walimu 500, wenye ualbino 250, wananchi 26,000 pamoja na kupitia vyombo vya habari matarajio yao ni kufikia watu 4,000,000. 
  
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Haki Yetu unaotekelezwa na shirika la "Under the same sun" kwa kushirikiana na mashirika ya GNRC na CEFA hapo jana katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa shirika la "Under the same sun" Bi. Berthasia Ladislaus na wengine ni wafanyakazi wa shirika hilo, kulia ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya Dkt. Rashid Mfaume na timu kutoka shirika hilo.Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akitoa neno la uzinduzi wa mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack Mkurugenzi wa shirika la Under the same sun Bi. Berthasia Ladislaus akitoa neno la shukrani kwa Mkoa wa Shinyanga mara baada ya uzinduzi wa mradi wa Haki YetuMeneja mradi wa Haki Yetu Bi. Wakyo Musong'o akitoa taarifa ya malengo ya mradi kabla ya uzinduzi wa mradi huo Baadhi ya washiriki wa uzinduzi huo wakifuatilia matukio yanayoendelea, chini ni watoto kutoka shule ya msingi Buhangija katika Manispaa ya Shinyanga.(Picha zote na Marco Maduhu - Shinyanga)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...